Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nami naomba niseme machache kutokana na yale ambayo yamezungumzwa, lakini zaidi nitajikita kwenye hili jambo la NEMC, jambo la Mazingira kwa ujumla na jambo la Muungano ambalo ni sehemu ya zao lililotuleta hapa baadhi yetu wengi.

Mheshimiwa Spika, mchangiaji mmoja nadhani wa mwanzo aligusia suala na NEMC na akasema kwamba NEMC wamekwenda, wameshafanya assessment na wameshatoa vibali, lakini bado wameweka zuio; na kibaya zaidi wameweka zuio kwenye baadhi ya miradi hasa miradi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka niseme katika hili kwamba NEMC ni taasisi ambayo inasimamiwa na inafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zote. Kama tutafika wakati NEMC tutaona mahali ambapo tutakwenda kuparuhusu pafanyike, ikiwa skuli, ikiwa kiwanda, ikiwa mgodi, ikiwa chochote kikiwa kinaelekea kuharibu mazingira, kuchafua mazingira ambayo baadaye yanakwenda kuathiri maisha ya watu. Hapa ni lazima kwanza tujue namna ya kufanya kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi tu kuruhusu kwa sababu tu watu wanataka wafanye, kwa sababu mwisho wa siku mazingira yale yakiathirika, athari na lawama zinakuja kwa Serikali, hasa NEMC kama ambavyo imezungumzwa. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hili jambo tuwaachie NEMC waendelee kufanya harakati zilizopo kwa mujibu wa taratibu. Tukifika wakati tukaona sasa usalama wa wananchi upo vizuri, tutaruhusu tuone namna ambavyo itawezekana.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala la fedha za miradi ya mazingira hasa kwa upande wa Zanzibar. Fedha zinakwenda; na kwa sababu tunasema, kinachofanyika tunakiona katika pande zote mbili za Muungano. Kwa maana Zanzibar tunapokwenda kukagua tunaona miradi; na Bara pia tunapokwenda kukagua tunaona miradi, na utaratibu wa fedha unatoka kwa mujibu wa taratibu zote.

Mheshimiwa Spika, hapa nataka tutoe wito. Changamoto iliyopo ni kwenye usimamizi na utekelezaji wa miradi hii. Ni kweli sisi ni sehemu ya wajibu wa kusimamia miradi hiyo, lakini tunao wenzetu tunaoshirikiana nao wakiwemo Halmashauri na wenzetu wa upande wa pili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa tunataka tutoe wito kwa wenzetu wote ambao tunashirikiana nao, kwa sababu suala la uhifadhi wa mazingira, tunashirikiana Serikali zote mbili. Kwa hiyo, Halmashauri wafanye wajibu wao na wengine wanaosimamia hili watekeleze wajibu wao ili nasi tujue namna ya kufanya katika suala hili.

Mheshimiwa Spika, pia kuna suala la changamoto ya Muungano. Sidhani kama tunaweza tukadumu kwenye Muungano kwa zaidi ya miaka 50, halafu ikawa changamoto ni nyingi kuliko mafanikio. Nikiwa naamini kwamba Muungano huu una mafanikio mengi sana kuliko changamoto, na kwa sababu changamoto nyingi au hizo ambazo inaitwa kero, nyingi tayari zimeshasawazishwa, zimeshatatuliwa. Zilizobakia zote, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, niwaambie Watanzania wote kwa ujumla, sasa hivi tupo kwenye harakati za kuweka vikao katika pande zote mbili za Muungano ili lengo na madhumuni, tuhakikishe kwamba changamoto zinazotatiza katika Muungano zinamalizika na zinatatulika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi tukasema tunaenda katika Muungano huu tusiwe na changamoto. Lazima tutakuwa nazo kwa sababu tunaohusika na tunaokubaliana ni binadamu, lakini tunapoona kuna changamoto na tukiona hii inakwenda kutatiza na kuliweka Taifa mahali pabaya, tunakaa, tunakutana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaambie Waheshimiwa kwamba, hata hizo changamoto ambazo bado tunazo, Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tayari tumeshakaa, tunaendelea kukaa na tutakaa kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto zote ambazo zinagusia katika Muungano, ili katika miaka tunayokwenda, tukarithishe vizazi vijavyo Muungano ambao hauna changamoto.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.