Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mungu kutujalia sote tukawa wazima hapa ili kujadili bajeti hii ya Katiba na Sheria kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, napenda sana nianze kwa kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika pamoja na wasaidizi wako kwa jinsi mnavyoliendesha Bunge letu hili la Bajeti kwa ustadi na umahiri na uhodari.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na mchango wangu kwa ruksa yako nichukue nafasi hii kumpongeza Mama yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopambana kuhakikisha kwamba Tanzania yetu hii inashamiri kiuchumi, uhusiano wa kimataifa na ustawi wa Tanzania yetu. Vilevile kusimamia utawala wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa Katiba na Sheria na Msaidizi Waziri, pamoja na watendaji na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii. Na kwa dhati kabisa nampongeza AG, Dkt. Feleshi kwa jinsi anavyokuwa makini na kushirikiana na sisi muda wote, he is never missed kwa kweli, AG ni kiboko yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kuzungumzia kuhusu utendaji na maboresho kwenye Mahakama. Pongezi za Serikali kwa hatua ya kuboresha Mahakama. Kusema kweli Mahakama za kileo. zimejengwa, Mahakama za kwa mfano Mahakama Kuu Shirikishi Arusha ni Mahakama ya kupigiwa mfano, facilities zote za kisasa, za ki-digital, za kimaendeleo yote. Maana hata kama utataka kwenda washroom basi utatamani usitoke kwa jinsi ya hali ilivyokuwa nzuri pale Arusha.

Mheshimiwa Spika, na vilevile tumeweza kuona kwamba, nchi yetu inakwenda kama vile supreme courts za Marekani. Jengo letu la supreme court litakapokamilika hapa Dodoma litakuwa ni jengo la mfano kabisa. Nashukuru sana, kwa kuwa kazi nzuri inafanywa pia chini ya usimamizi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna maendeleo makubwa sana. Bado kama wilaya 19 tu ndizo hazijapata majengo ya kileo. Sisi wenyewe na kamati yetu tumeshuhudia majengo ya kisasa kabisa ambapo hata mtu ukipelekwa huko hukumu itakayotoka unaweza ukaridhikanayo. Ukitizama siku za nyuma Mahakama zilivyokuwa utafikiri vijumba vya ndege, lakini sasahivi wilaya zote zimepata Mahakama nzuri na furniture za kileo. Unakwenda unapambana na ki-dock kile anachowekwa mtumiwa, mninga safi kabisa, ni kazi nzuri sana imefanyika. Samani za kileo na nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, lakini maboresho kwenye Mahakama yameweza kustawi zaidi kwa vile imetolewa huduma nyingine inayosema, Sema Na Mahakama Saa 24, ambapo watu wataweza kupeleka malalamiko yao na kujua status ya kesi zao na mambo yao mbalimbali. Kwa hivyo haya nasema ni maendeleo makubwa kwa sekta ya Mahakama ambapo mtu atapiga simu saa 24 na ataweza kupata maelezo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande huu wa uboreshaji masuala ya Mahakama ni kweli fedha iliyotumika, wanasema wazungu ni value for money, tumeweza kuona sasa fedha iliyotumika ni kweli. Kwa sababu, kwa mfano Mahakama ile ya Mwanga ni ya kileo kabisa; kwa hivyo, tunapongeza jitihada hizi zinazofanywa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nataka sasahivi niizungumzie Ofisi ya Mashitaka ambayo ni kilio kikubwa kwa kuwa imekuwa inapata fedha kidogo za kufanyia kazi zake. Kama tulivyosikia kwenye ripoti, kwenye ofisi hii kuna upungufu wa ofisi 125 ambazo haziko. Na tunaona jinsi watu wanavyopata malalamiko ya kucheleweshewa uchambuzi katika kesi zao na hivyo kubaki mahabusu kwa siku nyingi. Kwa hivyo, Serikali haina budi kuongeza fedha na kuongeza watendaji ili waweze kufanya shughuli hizi za ofisi ya mashitaka ziende kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ninataka kuzungumzia ni Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kilichopo Lushoto. Chuo hiki kina mchango mkubwa kwa sekta ya sheria nchini, tumeona. Na mpaka sasahivi ni chuo ambacho hata majaji wapya wakiapishwa wanakwenda kule kupigwa msasa. Hata hivyo, chuo hiki kina majengo machakavu sana, miundombinu yake si mizuri na si friendly hasa kwa wale watu wenye mahitaji maalum. Kwa hivyo, tungependa Serikali ifikirie kuongeza fungu pale kukiboresha hiki kiwe cha kileo zaidi, ikiwezekana cha namna yake kwa Afrika.

Mheshimiwa Spika, mabweni yamechoka sana. Tunayahitaji, tungependekeza kwa sababu, wanafunzi pale ni wengi na hivyo wanalazimika kwenda kupanga mitaani. Kwa hivyo, ni bora pakafikiriwa kuongezwa hostels mpya ili wanafunzi wapate malazi. Pamoja na hayo tunapongeza tumeweza kushuhudia jingo la hostel ya wavulana zuri sana ambalo linakidhi hata hawa watu wenye mahitaji maalum. Kwa hivyo, napongeza jitihada hizi zinazofanywa, na nalazimika tena kumpongeza sana mtendaji mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante, anafanya kazi nzuri. Prof. Elisante yeye ni mtendaji, yeye ni mhamasishaji, yeye vilevile ni kila kitu. Thank you very much Professor. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ningependa kwa ujumla wake Serikali iongeze mafungu kwenye mambo hayo mawili. Chuo hiki cha usimamizi huku Lushoto na Mkurugenzi wa Mashitaka.

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi hayo ndio yangu. Ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)