Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kupata uhai na leo hii kupata nafasi ya kuwasilisha bajeti ya Wizara kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali yaliyopangwa katika mwaka wa fedha ujao. Nitakuwa na eneo dogo la kuzungumzia, ni maboresho mbalimbali ambayo tunaendelea kuyafanya kama Wizara kwenye maeneo mbalimbali hasa ujenzi wa miundombinu kama Mahakama, kuimarisha ofisi za watendaji wetu kama ofisi ya DPP na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kimsingi kwanza niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu kwanza wametoa kama appreciation kwa Wizara katika kutekeleza wajibu wake na wamekiri kabisa kwamba wanaona kazi zinazofanywa na Wizara yetu. Nawashukuru sana sana kwa eneo hili na kadri uwezo wa kifedha utakavyoendelea tutaendelea kujenga uwezo mkubwa zaidi wa kuboresha miundombinu ambayo kimsingi maboresho yoyote ya miundombinu yanasababisha utoaji wa haki usiokuwa na mashaka.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama, tunao mkakati wa mpaka ifikapo mwaka 2025 kwa nchi nzima, tutakuwa tumeweka miundombinu mizuri sana. Mahakama zile ambazo ni mahakama jumuishi ambazo zipo kwenye level kuanzia Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufaa kwa sasa zipo sita, lakini mpango ujao tunategemea kuweka karibu mahakama tisa nyingine zenye sura ile.

Mheshimiwa Spika, vile vile katika ngazi za Wilaya hadi kufikia mwaka 2025, tunategemea Wilaya zote nchini zitakuwa na majengo mapya kwa zile wilaya ambazo hazina majengo kabisa tutakuwa tumekamilisha kabisa uwekaji wa miundombinu ya mahakama.

Kwa upande wa Mahakama zile za Mwanzo mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba mpaka ifikapo mwaka 2025, Makao Makuu yote ya Tarafa kwa nchi nzima, tutakwenda kuweka mahakama mahali ambapo huduma hii haijafika. Kwa hiyo haya ni makubwa ambayo tunakwenda nayo.

Mheshimiwa Spika, vile vile upande wa DPP kweli kuna uhaba mkubwa kama Waheshimiwa Wabunge walivyoliona na kwa kadri fedha zitakapopatikana tunataka kukimbiza ujenzi wa ofisi kwa sababu ofisi hii itakapoimarika, ni uhakika wa kutosha kwamba na Mahakama ule ufanisi utaonekana kwa uwazi mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa, kwa sababu Mahakama haiwezi kukamilisha shughuli bila ushirikiano na DPP na vyombo vingine.

Mheshimiwa Spika, vile vile upande wa Wakili Mkuu wa Serikali naye kumuimarishia ofisi ili aweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Kwa hiyo jambo la kuimarisha miundombinu ni jambo muhimu sana na sisi tunapokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge wote na maboresho yataendelea kulingana na jinsi ambavyo tunaendelea kupata fedha au vitendea kazi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lipo eneo lingine ambalo limeguswa na Waheshimiwa Wabunge hapa ni marekebisho ya sheria mbalimbali. Kuna Mheshimiwa ameeleza kwamba tupitie sheria mbalimbali hasa za vyama hivi kuangalia jinsi ambavyo wanaweka usawa wa kijinsia haya yote tunayapokea kwa sababu ni lazima yachakatwe.

Mheshimiwa Spika, ni wito tu kwa vyama na vyenyewe kwa sababu sheria yenyewe imetoa uhuru mkubwa sana, ni utekelezaji tu na usimamizi wa vyama vyenyewe binafsi kwenye utekelezaji wao, kwa sababu ukiangalia Chama cha Mapinduzi hakina uhaba wa akinamama katika ngazi mbalimbali za uongozi. Kwa hiyo unaweza ukaona labda ni mapungufu tu katika baadhi ya vyama ambavyo vinatakiwa vifungue milango kwa akinamama kupata ile haki sawa, hakuna mahali ambapo sheria imewanyima haki ya kugawana madaraka katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, hivyo niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na tumepokea maelekezo yao na tutakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)