Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii ya Madini. Kwanza kabisa nampongeza sana Waziri pamoja na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. Kwa niaba ya wananchi wote wa Mkoa wa Manyara namshukuru sana Rais, Mama yetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia maombi ya soko la madini kubaki pale Mererani. Kwa nini tunasema kwamba, soko la madini libaki pale Mererani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wanagawanya Mkoa huu wa Manyara kutoka Mkoa wa Arusha, waliangalia vigezo vingi sana na ndiyo maana Wilaya ya Simanjiro imeendelea kubaki Mkoa wa Manyara badala ya Mkoa wa Arusha kwa sababu kijiografia Wilaya yetu ya Simanjiro iko karibu sana na Mkoa wa Arusha, lakini waliangalia ni vigezo gani au ni shughuli gani za kiuchumi zinazoweza kubeba mkoa kwa mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Manyara, mkoa wetu unabebwa na madini ya Tanzanite; mkoa wetu unabebwa na shughuli za kilimo; na mkoa wetu unabebwa na Hifadhi ya Wanyama ya Tarangire. Hivyo basi, busara ya Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Mheshimiwa Benjamin William Mkapa waliona kabisa ni muhimu suala zima la madini ya Tanzanite yabaki eneo la Manyara. Hivyo basi, tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kubakiza soko hili katika eneo la Mererani na tunaendelea kuwaomba libaki pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali ni kwamba, lile soko la eneo la Tanzanite City limeshatengwa, mfumo wa maji umekamilika, mfumo wa umeme umekamilika, barabara zimechongwa, lakini bado kazi ya ujenzi haijaanza. Kuna uzio umewekwa pale wa bati, lakini hayo mabati yameanza kudondoka. Tunaomba kujua, ni lini Serikali itaenda kuanza ule ujenzi mara moja ili kuwatoa hofu wafanyabiashara wa Mererani? Kwa hiyo, Waziri anapokuja kuhitimisha, naomba sana atueleze, ni lini ujenzi utaanza pale ili wafanyabiashara wafanye kazi zao wakiwa na matumaini makubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, soko hili kuwa pale Mererani inatusaidia kuendeleza Mji wa Mererani, inasaidia vijana wengi kupata ajira pale Mererani, na kusaidia mapato makubwa kubaki katika Mkoa wa Manyara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la wageni kufika Mererani usalama wao umeboreshwa sana. Kwanza wageni wengi wanatua katika uwanja wa ndege wa KIA ambapo ni kilometa 20 tu kufika Mererani. Kwa hiyo, wafanyabiashara wa madini wa Mererani wanaendelea kuomba kwamba soko hili libaki pale, lakini Serikali itukamilishie mara moja ujenzi huu ili soko lile liweze kufanya kazi kwa ubora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi la pili. Wamama wengi katika eneo lile la Mererani wanajishughulisha sana na uchimbaji wa madini. Wako wamama wanamiliki migodi na wako ambao ni wachimbaji wadogo wadogo. Changamoto wanazokutananazo wamama hawa ni ukosefu wa mikopo. Naiomba Serikali sasa ione namna ya kuwawezesha akinamama, wale wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kujishughulisha kikamilifu na waweze kujikwamua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini tunasema haya? Shughuli ya madini ya Tanzanite upatikanaji wake kwanza kwa sababu hawana vifaa vya kutambua kwamba eneo hili ndiyo kuna madini, hiyo inawakosesha wamama wengi wanapoteza hela nyingi wakiwa wanachimba yale madini halafu hawafanikiwi. Serikali ione namna ya kuwapatia vifaa na wataalam pamoja na mitaji ili wale wamama wanapochimba madini yale wawe na uhakika wa kupata madini na waweze kujinyanyua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la usafiri. Katika lile eneo la ukuta wa Mererani ambalo tunasema geti la Magufuli, tuna usafiri wa bodaboda mle ndani; tuna wamama ambao wanafanya biashara ya Mamantilie, tuna wamama ambao wanabeba matunda kichwani wakiwa wanaenda kuwauzia wachimbaji wadogo wadogo mle kwenye eneo la ukuta, lakini changamoto kubwa ni bodaboda zinazotumika mle ndani, wanalipishwa shilingi 2,000 kuwapeleka na shilingi 2,000 kurudi; wanapoingia tu getini, kitu ambacho kinasababisha wale akinamama wanashindwa kufanya zile biashara ili kujikwamua kiuchumi kwa sababu wanatumia zaidi ya Shilingi 8,000 hadi shilingi 10,000 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali ione namna ya kuongea na wamiliki wa usafirishaji, yaani magari, ili magari yaruhusiwe kufanya kazi kule ndani ya ukuta; wamama hawa waweze kupata usafiri ili waweze kujikwamua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, naiomba Serikali; kuna hawa wafanyakazi wa migodi ambao wanafanya mkataba kati ya wamiliki wa migodi pamoja na wale wafanyakazi wa migodi. Wale wafanyakazi wa migodi wana changamoto nyingi sana.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri hili anafahamu ni kwa namna gani wale wachimbaji wadogo wadogo ambao wanazama kwenye mashimo wanakosa haki zao za msingi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. REGINA N. QWARAY: Muda umeisha? Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)