Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nijadili hili suala la dharura. Nimpongeze sana mtoa hoja kwa kutoa hoja hii ninaamini sasa sisi kama Bunge tunaenda kuishauri vizuri Serikali ili iweze kuchukua hatua. (Makofi)

Kama alivyosema Mheshimiwa Musukuma, kwamba sasa hivi mafuta yamepanda. Ukiangalia kwenye baadhi ya majimbo huko vijijini; kwa mfano kule ambako hakuna sheli (vituo vya mafuta sasa hivi kule mafuta yanauzwa zaidi ya shilingi 5,000. Jambo hili ni hatari kwa kuwa tunajua mafuta yanapopanda bei kila kitu kitapanda bei. Tunavyozungumza leo, jana kusafirisha cement kutoka Tanga kwenda Mwanza, hapo nyuma walikuwa wanasafirisha kwa tani moja shilingi 130,000 lakini tunavyozungumza leo tani moja ya cement kusafirisha kutoka Tanga kwenda Mwanza imepanda mpaka shilingi 160,000 ambapo inaenda kupandisha mfuko wa cement kwa shilingi 1,500 jambo hili ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishauri sasa Serikali kwa mambo mawili; jambo la kwanza ni kufanya hatua za dharura, kutafuta fedha kwa ajili ya kupeleka ruzuku kwenye mafuta ili walau tuweze kupunguza gharama za mafuta. Tukiweka ruzuku pale maana yake gharama ya mafuta inapungua, na ikishapungua hizi gharama za mafuta zitapunguza gharama za vitu vingine ambavyo sasa vitapanda bei.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, ninajua wazi kwamba tuna tozo nyingi ambazo tumeweka kwenye mafuta kwa ajili ya nchi na kwa ajili ya bajeti tuliyoipitisha. Lakini sisi ndio Wabunge na sisi ndio tuliyopitisha bajeti, hivyo kuna haja sasa ya kuangalia baadhi ya tozo tuweze kuziondoa kwa wakati wa dharura kwa hii miezi miwili; kwa maana ya mwezi wa tano na mwezi wa sita, tuzipunguze takribani kuanzia shilingi 400 mpaka shilingi 500 ili tuwe na unafuu kwenye mafuta. Tukiyafanya haya yataleta unafuu wa maisha kwa wananchi wetu, hamna namna ambayo tunaweza kufanya kwa sababu maisha ya kwetu tunayajua huko vijijini yanategemea mafuta; bila mafuta maisha hayaendi. Kwa sababu gani, kwa sababu leo cement itapanda, nondo zitapanda, sabuni zitapanda kila kitu kitapanda kwa hiyo, lazima tuchukue hatua za tahadhari za haraka ili kunusuru hili janga kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba sasa nami kuunga mkono hoja na tuweze kutafuta fedha za dharura tuweze kunusuru suala hili la dharura katika nchi. Ahsante sana. (Makofi)