Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niwe Mbunge wa kwanza kuchangia katika hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani Engineer Masauni. Mimi mchango wangu ningependa zaidi nijikite katika lile suala linalohusiana na hali ya usalama barabarani kama ilivyo katika ukurasa wa 15 na 16.

Mheshimiwa Spika, suala hili limenifanya nichangie kwa sababu nilikuwa nikiangalia takwimu ambazo Mheshimiwa Waziri amezileta si takwimu nzuri. Hii ni kwa sababu kumekuwepo na ongezeko, vifo pamoja na ongezeko la majeruhi ya wananchi ambao sisi tunawawakilisha humu Bungeni. Nikiangalia, sisi Kinondoni kwa mwaka 2020 tumeonekana kuongoza. Idadi yetu ya watu ambao waliopata ajali ni ajali 353 ni kubwa kuliko wilaya nyingine ama mkoa mwingine wowote.

Mheshimiwa Spika, hii ni hatari hasa ukiangalia kwamba wanaoumia sana sana ni vijana wetu na watu wetu ambao wanaishi katika maisha ambayo lawlessness kama wanavyowaita Waingereza, hasa ukiangalia pale Dar es Salaam. Sasa vitu kama hivi haviwezi vikaendelea kuwepo. Na hata ukiangalia Mheshimiwa Waziri mwenyewe anakubali kwamba ajali zinaongezeka.

Mheshimiwa Spika, ajali zinaongezeka ukiangalia takwimu; hivyo na mimi ningependa nijielekeze hasa kuhusu hawa waendesha boda boda; na ninapenda Waheshimiwa Wabunge wasifikiri kwamba mimi ninapiga vita biashara ya boda boda, hapana, napenda biashara ya boda boda iendelee, lakini ningependa iendelee kwa kufuata kanuni na sheria tulizojipangia. Sheria hizi ni kama ile Sheria ya Law Traffic Act ya Mwaka 1973.

Mheshimiwa Spika, nimefanya utafiti na nimezunguka sana, nimekwenda kwenye Taasisi yetu ya Takwimu (National Bureau of Statistics), nimekwenda traffic Makao Makuu nimepata taarifa, lakini vile vile nimekwenda kwenye hospitali yetu ya Mwananyamala kuangalia idadi ya watu ambao wanapata ajali. Sasa, leo nikaja nikashangaa nilivyoona takwimu nyingine inayotolewa na Wizara. Hakika haya maeneo yote ambayo ni maeneo ya Serikali, mifumo ya utoaji wa tarakimu ni matatizo Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, takwimu hazioani hata. Ukiangalia takwimu zinavyoonyesha ni kwamba watu wa Bureau of Statistics wao wanasema kwa kutoa mfano, kwamba kwa mwaka 2020 taasisi inasema ajali za pikipiki zilizotokea nchini zilikuwa 505. Lakini ukienda Traffic kwenyewe wanakwambia 404 na hizo karatasi ninazo. ukiangalia hata takwimu za vifo haziendani.

Mheshimiwa Spika, ningeshauri kwamba Serikali ije na mfumo wa kupata takwimu zake sahihi ambazo zitakuwa relied upon, tutazitegemea. Kwa sababu bila ya kuwa takwimu sahihi unaendaje kutafuta solution, unakwendaje kutafuta majawabu kwenye matatizo ambayo sasa hivi yanaonekana kuongezeka. Hilo ni jambo langu la kwanza, ningemuomba Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia.

Mheshimiwa Spika, lakini kingine ambacho kimenishangaza kidogo ni pale ninavyoona takwimu za piki piki Kinondoni ajali 64. Nikiangalia, mimi ninakaa Kinondoni na ninavyotembea mule haipiti siku mbili au tatu utakuta mtu kagongwa na kuna mwingine amefariki; lakini takwimu itakwambia 64. Ina maana kila baada ya siku sita ama wiki ndiyo ajali moja inakuwa reported. Haiwezekani kwa mji kama Kinondoni ambayo ina kilomita 1,663 na piki piki ziko nyingi kiasi kwamba ukiendesha gari Kinondoni; na maeneo mengine hata hapa Dodoma; utashangaa kuona kwamba kuna matatizo makubwa. Kwa mfano, kupita taa nyekundu ni kitu cha kawaida, kwenda no entry ni kitu cha kawaida, kujaza abiria; piki piki inatakiwa iwe na mtu mmoja kwa mujibu wa Sheria lakini; wanakuwepo watu zaidi ya wawili kwa maana ya mishikaki, mjini tunaita mishikaki natoa mfano tu, hiyo yote inakatazwa katika hii Sheria. Lakini utafiti wangu nilioufanya kule traffic wanasema...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja, malizia mchango wako.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nilifikiri dakika kumi. Anyway, ninachoomba cha msingi ni kwamba Mheshimiwa Waziri aharakishe ule Muswada ambao mnataka kuuleta kwa minajili ya kufanya marekebisho katika Sheria ya Road Traffic ya Mwaka 1973, iharakisheni. Kwa sababu huo Muswada nimeuona, upo, basi uharakisheni kwa sababu hata adhabu zinazotolewa hazitoshelezi. Tumepunguza adhabu ya shilingi 10,000 hapa, adhabu hii inafanya watu waendelee kufanya makosa. Naomba Serikali ifikirie upya adhabu ambazo zinaweza zikatumika ili kuweza kuwa deterrent…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakushukuru.