Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jioni hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Masauni na Mheshimiwa Sagini kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kushika nafasi kuongoza wizara hii. Tunawatakia kheri vijana wenzetu katika kuupiga mwingi na kuhakikisha ndoto ya Mama Samia inafikiwa vizuri katika kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina takribani mambo saba ninataka nichangie mchana huu lakini kwa sababu ya muda nitachangia haraka haraka. Nitayaa-highlight lakini naamini Waziri na wasaidizi wake wizarani watayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, Jambo la kwanza linahusu madai ya askari wastaafu. Kwa kifupi ninaposema askari nitakuwa namaanisha askari wote waliopo kwenye majeshi yaliopo Wizara ya Mambo ya Ndani, pia itakuwa inahusu makamishna na maafisa wote wanaohusu waliopo chini ya majeshi yalioko Wizara ya Mambo ya Ndani ili nirahisishe kutokana na muda. (Makofi)

Mheshimiwa spika, sasa madai ya askari waliostaafu; hapa naongelea sana sana madai yanayohusu fedha za uhamisho lakini pia kuna madai ya wale waliostaafu fedha za nauli na usafirishaji wa mizigo. Kwa hiyo Waziri na wasaidizi wako nawaomba mkalifanyie kazi hizi Wizarani ili wale askari wote waliostaafu waweze kupatiwa madai haya ili wapunguze manung’uniko huko mtaani kwa kulitumikia Taifa letu kwa muda mrefu. Kwamba, sasa wamestaafu lakini hawajalipwa fedha zao za kusafirisha mizigo na nauli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili; ni madai ya askari wote waliosimamishwa kazi na hatimaye baadaye kutokana na uchunguzi au kufuatana na kutatuliwa kwa changamoto walizokabaliana nazo wanaporudishwa kazini; pia pamoja na madai ya baadhi ya askari ambao bado wapo kazini, ambao walisimamishwa kazi na baadaye kutokana na procedures za kimaadili wakaonenaka hawana shida na kurudishwa kazini. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba pia hili jambo mliangalie. Hii ni kwa sababu tumekuwa tukipata malalamiko huko majimboni ambapo baadhi ya wazee wetu wanatuomba kwamba tusaidieni kupeleka documents; kwamba wanasema mimi nilisimamishwa kazi, na baadaye nikarudishwa, lakini bado malimbikizo yangu ya ile mishahara ambayo nilikuwa nimesimamishwa kazi haijailipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu; Mheshimiwa Waziri naomba ulifuatilie na wasaidizi wako mlitatue…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Ngassa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Ngassa; kwamba katika orodha ya madai anayoorodhesha pia kuna askari wa jeshi la polisi, magereza lakini hata wale wa traffic; unakuta wanaamishwa kituo kimoja kwenda kingine hawalipwi fedha za kuhamishwa tena wanaamishwa tena hawalipwi tena. Kwa hiyo hayo yote Serikali iangalie iweze kuwalipa on time. (Makofi)

SPIKA: Nimeona jina lako hapo unachangia hilo halipo kwenye hoja yako unayochangia. Waheshimiwa Wabunge muda wa kuchangia ni mfupi sana kwa hiyo, unaposimama kumpa mwenzio taarifa angalia ule muda wake pia. Kwa sababu taarifa ikitolewa ukiwa na muda mrefu ni sawa, ukiwa mfupi kidogo inaleta changamoto.

Mheshimiwa Ngassa unaipokea taarifa hiyo.

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naipokea taarifa naomba niendelee kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nililotaka kuchangia ni suala la madai ya wazabuni na watoa huduma. Mheshimiwa Waziri ukifuatilia kwenye vikosi vyetu mbalimbali, vikosi vya mbwa, vikosi vya farasi huko utaangalia kuna baadhi ya wazabuni walitoa huduma wana madai. Kwa hiyo naomba jambo hili mlifuatilie pia muweze kuwalipa.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, ningependa kulichangia mchana huu ni makazi ya askari polisi, na hivi karibuni pia nilichangia, lakini naendelea kusisitiza kwa sababu nyumba za askari wetu baadhi zimekuwa katika hali isiyo nzuri sana. Tunaomba wizara mlipe kipaumbele mzifanyie maboresho ili askari wetu waweze kuishi maeneo safi na salama kwa ajili ya usalama wa familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tano ningeomba kulichangia mchana huu ni kuhusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Kwa sasa kuna mradi mkubwa ule wa bomba la mafuta linalotoka Uganda kwenda Tanga, kuna wilaya 24 ambazo tunaomba Jeshi la Zimamoto na Ukoaji wazifanye kuwa wilaya za kimkakati na watupatie gari za zimamoto. Hii ni kwa sababu hili bomba la mafuta linapopita litakuwa ni moja ya risk katika maeneo yetu. Kwa hiyo tutakapokuwa na lile gari hata litakapotokea jambo lolote basi tuwe na uhakika wa kudhibiti janga ambalo litatokea kwa ajili ya wananchi. Kwa hiyo Wizara ya Mambo ya Ndani naomba jambo hili mlizingatie sana; ikiwemo Wilaya ya Igunga ambako bomba la mafuta linapita kwenye takribani kata nne hivi tupate gari moja; na ni kwa sababu kuwa pale sasa hivi pia tuna ofisii ya zimamoto na Jeshi la Uokoaji na tuna afisa pale na wasaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, jambo la sita ambalo ningependa kulichangia mchana huu ni suala la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa. Mheshimiwa Masauni nadhani unakumbuka tulipokuwa wizarani miaka ya nyuma pale tulikuwa tukipambana katika kuinasua taasisi hii, na sasa upo kwenye Wizara. Ninakushauri mambo mawili unayoweza kufanya ili kuisaidia taasisi hii. Jambo la kwanza; Mheshimiwa Waziri ahakikishe bajeti wanayopangiwa na Serikali inakwenda yote ili waweze kuendesha operation zao vizuri. Jambo la pili na la msingi ni kuhakikisha kuwa anasimamia katika kuhakikisha vitambulisho vya Taifa; kwa maana ya zile hard copy, kwamba zinatoka na kuwafikia wananchi. Kwa sababu sasa hivi changamoto kubwa wanayokutana nayo wananchi kule ni wengi kuwa na namba lakini unakuta…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, kengele imegonga. Uliongea hapo mwishoni ulikuwa umeshazima kisemeo chako umesemaje?

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)