Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kweli kwa kunipa nafasi hii lakini kwa hakika nitakuwa mchoyo wa fadhila bila kukupongeza sana leo asubuhi umefanya jambo kubwa katika Taifa la kuruhusu mjadala ambao una maslahi makubwa katika Taifa letu. Hongera sana, tumepata salamu nyingi kutoka kwa Watanzania kwamba Bunge sasa linakwenda kuishauri Serikali na kwa muda muafaka na tunategemea maagizo yako yatatekelezwa. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kaka yangu Masauni kwa namna ambavyo anasimamia Wizara hii, lakini pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha uwepo wa usalama wa nchi yetu kama walivyokasimiwa madaraka na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, kama hakuna usalama hakuna maendeleo. Kwa hiyo, nilitaka niseme hayo tunayoshauri lengo letu ni kuhakikisha usalama wa Tanzania na kwa hakika waweze kufanya kazi zao vizuri. Mfano mdogo ni huu wa juzi uliotokea wa panya roads wameweza kuharibu sana amani ya wananchi katika maeneo ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, nitakwenda haraka haraka kwenye mchango wangu. Nianze kwanza kwenye eneo hili ambalo nalisema la Kituo cha Polisi pale Ikungi, ni kituo ambacho amekieleza Mheshimiwa Sangu Ndugu yangu, kimeanza ujenzi katika miaka saba iliyopita. Hapa ndani ya Bunge hili nimeuliza maswali siyo chini ya matatu kuulizia kituo kile; na majibu yamekuwa ni yale yale. Kama haitoshi kwenye Kituo cha Polisi kinachotumika sasa hivi, ni kituo ambacho unaweza kusema ni kama stoo, siyo Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, niombe sana nimeona imetajwa ndani ya bajeti na tuliongea na Mheshimiwa Masauni, alishafika pale mwaka 2018 akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Nimwombe sana, leo nisipopata majibu ya kutosheleza kwa hakika kwa mara ya kwanza nitashika shilingi ili nipate ufafanuzi wa kutosha kuhusu Kituo cha Ikungi pamoja na vituo vingine nchini, nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha vituo hivyo vinajengwa na kuweka hadhi ya Jeshi la Polisi ambao wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa vyombo vya usafiri tumeambiwa hapa Wilaya ya Ikungi ina kilometa za mraba 5,800, ni wilaya kubwa lakini ina magari mawili ambayo ni chakavu sana. Leo ukihitaji leo waende waka-attend tukio lolote, wanaweza kwenda wakati kabla hawajarudi wanaambiwa tukio lingine limetokea; kwa hiyo, hawawezi kuwahi matukio mbalimbali. Hiyo, kama haitoshi mimi kama Mbunge niliwahi kuwachangia pale nikawasaidia pikipiki mbili ili kupunguza makali hayo. Nilishamwomba Mheshimiwa Waziri atupatie gari katika mgao wa magari hayo, naomba hata angalau atuongezee gari lingine moja ili kumfanya OCD aweze kufanya kazi vizuri na watu wake.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili ni OC ya mafuta. Tunategemea nini tunapokuwa tunaamini, tunawawekea ration ndogo sana ya mafuta kwa mwezi, unategemea huyu OCD atafanyaje kazi kilomita 300 kwenda na kurudi kila siku kwa matukio, itakuwa ni ajabu sana, kusema unaruhusu aka-attend matukio wakati hujamwezesha. Niombe sana Mheshimiwa Waziri tuwaongezee bajeti ili hawa polisi wenzetu waweze kufanya kazi yao vizuri na kuweza kuokoa Watanzania pamoja na mali zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu ni mafao. Polisi wetu wanafanya kazi nzuri, wanafanya kazi kwa uzalendo mkubwa na kama ulivyosikia mishahara yao ni midogo, lakini inapofika wamestaafu sasa mafao yao hawayapati kwa wakati. Hivi inashangaza sana mtu amefanya kazi sana zaidi ya miaka 30, siku anastaafu unaanza tena kumwomba vielelezo vya kudai mafao yake; hili siyo sawa. Niombe sana Serikali iweze kuona namna ya kuwasaidia wazee wetu hawa waweze kuendelea kuishi vizuri na wengine wanapostaafu wanakufa haraka kwa sababu wanachelewa kulipwa mafao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana, lakini baadaye nitakuja; nitashika shilingi. (Makofi)