Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwapongeza Viongozi wa Wizara hii wote kwa namna ambavyo wamekuwa wakipambana kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Spika, kabla sijajikita kwenye hoja ya msingi, nilitamani kuomba kwa Wizara suala la mpaka wa Tunduma waliangalie kwa karibu na ikiwezekana tunaomba watupe Wilaya Maalum ya Kipolisi katika Mkoa wa Songwe kulingana na mahitaji ambayo yapo na kiwango cha uhalifu ambacho kimekuwa kikiendelea kuongezeka kadri siku zinavyokwenda. Pia Kituo cha Polisi cha pale ni chakavu, kidogo na hakina hadhi ya kuwepo mpakani. Nalo hilo naomba waweze kutupa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kumwomba Waziri atusaidie magari ya Zimamoto na gari la Utawala wa Zimamoto kwa Mkoa wa Songwe. Kwa sababu tunafahamu barabara ya Tanzam ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania. Hivi karibuni tumekuwa tukiona moto ukiendelea kuwaka barabarani na mwisho wa siku usafirishaji katika ile barabara haupo kwa sababu hakuna hata njia za mchepuko katika ile barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, napenda nirudi kwenye hoja ya msingi ya Jeshi la Magereza. Tumeona wamewasilisha taarifa nzuri, lakini sijaona sehemu ambayo wamewaongelea wafungwa kwa namna ambavyo wanastahili huduma za kibinadamu katika maeneo wanapokuwa pale Gerezani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kabisa moja ya haki za msingi za binadamu ni haki ya kuishi na pia kuhifadhiwa utu wake. Tumekuwa tunafanya ziara mbalimbali katika Magereza, hali ya magodoro Magerezani siyoo nzuri. Kwa mtu yeyote ambaye amefika Gerezani, ameingia akafanikiwa kuona hali halisi kule ndani, hali ya magodoro siyo nzuri. Nami ninarejea kwenye haki ya kuishi, kwamba mtu anastahili kupata chakula kupata matibabu lakini pia kulindwa afya yake iendelee kuwa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawafahamu kabisa wanaoishi Magerezani ni ndugu zetu, ni sehemu ya jamii hii yetu na mwisho wa siku wanapotoka wanarudi kwetu. Wanapokwenda ndani kule wanalala kwenye magodoro ambayo ni chakavu yamechoka hatujui wamelalia watu wangapi ni risk kwa afya ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia bajeti hii nilitamani kuomba jambo moja, kama hawawezi kuwanunulia magodoro, wawaruhusu wanunue magodoro waingie nayo. Ninarudia kuliongea hili kwa uchungu kwa sababu hali ya malazi ya wenzetu kule ndani siyo nzuri. Sisi leo hii hatujijui, wengine tulishafika tukaingia mpaka Central, lakini hatujui kama siku moja mtu unaweza ukaingia ukalala mle. Hali ya malazi siyo nzuri, ni machafu, hayafai kwa afya ya binadamu. Wanapotoka kule watarudi na maradhi, watatuambukiza sisi pia huku kwenye jamii. Mwisho wa siku tutakuwa na jamii ambayo inaendelea kuwa na maradhi, inapambana na magonjwa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninataka kusema nini? Tuna wafungwa karibu 32,000 ambao Serikali kama kweli ikiamua kujitoa kuwahudumia kwa upande wa malazi, kama ambavyo inaweza kuruhusu wakanunua chakula…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo inaweza ikaruhusu wakatibiwa na watu wao wa nyumbani…

SPIKA: Mheshimiwa Neema Mwandabila, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nilikuwa nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Neema Mwandabila, maana yake sisi wengine ni wahanga, Gerezani tumekaa zaidi ya miezi minne, mitano. Unakuta hakuna magodoro, watu wanalala kwenye viroba na wengine wanalala chini kwenye cement hadi wanapata michubuko ya sehemu za mwili wao. Kwa hiyo, nampa tu taarifa kwamba asiombee aishie tu Central asije akaenda Magereza. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Neema Mwandabila, unaipokea taarifa hii?

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yake na ninamwomba Mwenyezi Mungu aninusuru katika hili.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema nini? Serikali kama kweli inatambua kwamba jamii ile iliyopo kule ni ndugu zetu, kwa kiwango cha Shilingi 50,000/= kumgharamia mfungwa malazi ambao kwa ujumla wake inakuja kama Shilingi 1,600,000,000/= wanaweza kufanya. Kwa sababu ya majukumu ambavyo yamekuwa ni mengi na sasa hivi tuna janga hili la mafuta, tuwaombe wabadilishe au watengeneze utaratibu wa hawa wafungwa na mahabusu.

Mheshimiwa Spika, tunajua mahabusu sio mfungwa, hana hatia mpaka pale Mahakama itakapo-prove kwamba huyu ana hatia, ndiyo ataanza kutumikia kifungo. Imagine umekosa, haijajulikana kama umekosa, umekamatwa, umepelekwa kule, unakwenda kupitia hali ile; kwanza unapata msongo wa mawazo, lakini ndiyo hivyo afya inaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu, kwa kuyaangalia hayo kwa namna ambayo ni ya kipekee, waone namna ya kutengeneza utaratibu kama walivyotengeneza kwenye chakula na kwenye mavazi ya mahabusu. Pia katika hili waone kwamba ipo haja ya kutengeneza utaratibu wa wafungwa, kama hana uwezo wa kununua, atatumia yale yale atakayoyakuta, lakini kama ana uwezo, utengenezwe utaratibu ambao ni wa kiusalama.

Mheshimiwa Spika, niliuliza hapa kipindi fulani ika-trend ikaonekana kama ni kitu cha ajabu, nikasema hawa hawajui hali iliyopo kule. Laiti wangejua hali iliyopo Magereza, suala la kwenda Magereza kama wadau namba moja wa kusaidia changamoto ya magodoro Magerezani ingeweza kusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, nisiseme mengi, pia naomba katika suala la mavazi, wale watu mavazi wanayovaa ni chakavu... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)