Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Pia naomba Hansard itambue kwamba jina langu kamili ni Rashid Abdalla Rashid, na sio Rashid A. Rashid. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza niseme, naisifu na naipongeza hotuba hii ya Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini nataka nijielekeze kwenye Wilaya yangu ya Mkoani kuhusiana na suala zima la Jeshi la Polisi na hasa kwenye miundombinu ya majengo.
Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ya Mkoani ina Vituo vinne ambavyo ni Kengeja, Mtambile, Mkoani na Shidi. Nataka nikwambie kwamba vituo hivi vilianza kujengwa toka mwaka 1926. Vituo hivi vimechoka na kwa kweli havifai kabisa kufanya kazi kwenye Jeshi la Polisi, yaani wafanyakazi wa Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Mkoani wana mazingira magumu sana. Naamini Mheshimiwa Waziri anatambua ubovu na uchakavu mkubwa wa vituo hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Kituo kikuu ambacho ni Ofisi ya Polisi Wilaya ya Mkoani, kwa kweli hali ni mbaya mno; hii imegeuka kama gofu. Yaani ina mipasuko ambapo miti ile ambayo inaota kwenye viambaza imeota. Mvua hizi zinazoendelea kunyesha kule Zanzibar sasa hivi ukweli ni kwamba askari hawana mahali pa kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu ni kwamba bajeti ni nyingi kuna bajeti zaidi ya miaka 70 iliyopita haijawahi kugusa Wilaya ya Mkoani kwenye ukarabati wa majengo. Namwomba Mheshimiwa Waziri afanye anavyofanya, lakini katika vituo vinne hivi, kwenye Wilaya ya Mkoani tupate kituo kimoja, kijengwe angalau kiwe na hadhi ya Jeshi la Polisi kama lilivyo Jeshi lenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ya mwaka 2021 uliopita, niliomba hapa na nikaahidiwa kwamba linachukuliwa na litafanyiwa kazi, lakini cha kushangaza ni kwamba kwenye bajeti hii Wilaya ya Mkoani haikuguswa. Vile vile niseme kwenye jambo hili kuna Kituo cha Polisi Kengeja, hiki ndio ambacho kimeoza kabisa, hakifai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, miezi kama nane iliyopita, mahabusu wa pale walivunja na wakakimbia, na walikuwa na kesi mbaya kabisa. Cha kushangaza, matokeo ya kukimbia mahabusu wale, ni kuwahamisha Polisi wote walioko kwenye Kituo kile na kuleta wengine, lakini hakuna hatua madhubuti zilizofanywa za ujenzi au ukarabati wa kituo kile. Naomba Mheshimiwa Waziri alione hili na ajue kwamba hali ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine kuna watumishi wa Polisi kutoka Tanzania Bara na wengine kutoka Tanzania Zanzibar. Watumishi hawa wamehamishwa tangu mwaka 2020. Watumishi hawa bado hawajapatiwa stahiki zao. Kwa kweli haipendezi. Ni watumishi wanaolitumikia Jeshi kwa uzalendo kabisa, lakini tunashindwa kuwapatia hata zile stahiki zao za uhamisho. Wako waliotoka Pemba kuja huku na waliotoka huku kwenda kule, lakini hakuna suala la uhamisho ambalo limefanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna watumishi wa Jeshi la Polisi ambao kipindi kifupi tu kilichopita nadhani sote tuliona, walifanya kitendo kimoja cha kiungwana sana cha kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 2.2 lakini hata barua ya pongezi hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunakumbuka hapa Mwalimu baada ya vita vile vya Uganda wanajeshi walipokuja hapa aliwapa ahsante. Wanajeshi hawa tuliona fedha nyingi walikusanya lakini hata barua ya pongezi hakuna, hili jambo halipendezi. (MakofI)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RASHID A. RASHID: Mheshimia Spika, naona kengele imelia, lakini pia niseme kwamba juzi nilimwona IGP Sirro Arumeru akihimiza ulinzi shirikishi na watu wakachangamka sana… (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa. (Kicheko)
MHE. RASHID A. RASHID: Mheshimiwa Spika, haya naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)