Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoifanya lakini wananchi wa Jimbo la Hai wameniambia nimshukuru kwa sababu nadhani ni Jimbo pekee nchi hii limetembelewa Na Mheshimiwa Rais mara tano, juzi alikuwa pale kwetu kwa ajili ya kuzindua Royal Tour na alizungumza na wananchi pale tunamshukuru sana na kila akija anatuachia miradi kedekede tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya na mimi pongezi zangu zinaambatana na ahadi yako kwamba magari yanayokuja na pale Hai tutapata gari moja ya Polisi na wewe ni mtu rahimu huwezi kusema uwongo. Pamoja na Naibu Waziri nakupongeza lakini nakupongeza uliniahidi hapa kwamba utatusaidia nyumba za Polisi pale Hai na asubuhi umerudia kuniahidi, kwa hiyo na wewe nakupongeza nikiamini ahadi hiyo utateikeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapongeze pia uongozi wa usalama pale kwetu nikianza na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Katibu Tawala Dada yangu Ndugu Pendo Wela lakini pia pale kwetu umetuletea OCD mzuri sana anafanyakazi nzuri nakupongeza sana. Baada ya hayo naomba nijielekeze kwenye hoja iliyoko mezani na nianze na Jeshi la Zimamoto.

Mheshimiwa Spika, ukisoma humu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri utaona namna ambavyo fedha zimepelekwa kwa uchache sana kwenye Jeshi la Zimamoto lakini fedha za maendeleo zimepelekwa kwa asilimia Sifuri (0%) kuanzia Februari mpaka hapa tulipo hii ni hali mbaya sana iliyoko kwenye Jeshi la Zimamoto.

Mheshimiwa Spika, niliwahi kushauri hapa na leo naomba wanielewe, kwamba Jeshi hili la Zimamoto jamani kazi hii imewaelemea tutafute namna nyingine na siyo vibaya tukarudi kule tulipotoka, mwaka 1985 ilikuwa TAMISEMI, Jeshi la Zimamoto kazi ya zimamoto na uokozi ilikuwa inafanywa chini ya TAMISEMI, lakini mwaka 1982 kazi hii ilipelekwa Halmashauri mimi nashauri tuende kule na ninashauri kwa sababu tunaona namna ambavyo Jeshi hili limeelemewa. Hivi tukiuliza wana magari mangapi ya kuzima moto na ndiyo core objective ya kazi yao. Sasa kama ile kazi ya msingi tu vifaa hawana!

Mheshimiwa Spika, pale kwetu Hai tuna watumishi watatu tu, hawana gari hawana kifaa chochote, maskini wa Mungu wamekodishiwa pale kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ndiyo wanakaa pale hawana ofisi, pamoja na kutokuwa na ofisi wameomba pikipiki mbovu pale Halmashauri, tunataka tuwatengenezee hiyo mbovu ndiyo watumie. Yule Afisa anajitahidi anafanyakazi nzuri juzi tumepata tukio la moto pale kwa Sadala, akaenda kufundisha wananchi pale kuzima moto kwa kutumia vumbi! Sasa kweli kwa nini tusikubali kwamba jamani tumeelemewa? Turejeshe Halmashauri ambao wana nguvu waweze kufanyakazi hii.

Mheshimiwa Spika, najua Makamanda pale wananiangalia kwamba baada ya kurudishwa Halmashauri sijui tunaenda wapi! Bado ninyi ni Polisi kuna Majeshi mengine mtaenda huko, lakini ninyi mtafanyakazi ya kuratibu jambo hili.

SPIKA: Mheshimiwa Mafuwe, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Nusrat Hanje.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba anachokizungumza ni sahihi sana na ukizingatia...

SPIKA: Ngoja ngoja, unajua hata mwanzo nilikuvumilia hiyo sentensi siyo kazi yako kujua yeye anasema uwongo ama sahihi, wewe nenda mueleze taarifa kwa sababu ukisema ni sahihi maana yake kuna mtu labda mwingine anazungumza ambayo siyo sahihi. Kwa hiyo wewe nenda mpe taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kipindi cha karibuni hapa kumetokea kuungua kwa masoko makubwa kwenye Halmashauri ambazo zina uwezo wa kununua facilities za kwao za kuzima moto. Kwa hiyo ni kitu ambacho ni valid kabisa tunatakiwa Halmashauri zipewe uwezo huo, zipewe mamlaka zinunue zenyewe. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ninaipokea na mimi naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba sasa ifike mahali tufanye tu-review tena mfumo huu na wakubali tu wenzetu hawa inawezekana hiki ninachokishauri waende waboreshe zaidi kuona namna ambavyo tunaweza tukawa kweli na jeshi la zimamoto la hakika. Hebu fikiria eneo la Hai ambapo kuna uwanja wa ndege wa Kimataifa hakuna Wilaya ile haina gari, haina hata pikipiki, kwa hiyo ni vema wakapokea ushauri huu.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri, lakini sasa hizi nyumba Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kunijibu hapa kwamba tukachangishane tuanze ujenzi kule kujenga nyumba za watumishi hii na yenyewe siyo sawa jamani tunachangishana kwenye maboma tunachangishana kwenye kila kitu, kwenye hili mimi niombe Serikali itusaidie. Hai hatuna nyumba tuna watumishi 150 hakuna nyumba mpaka ya mkuu wa kituo wanapata taabu sana kwenye kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, pia kwa ujumla kuhusu stahiki za watumishi hawa kwa maana ya Majeshi yote, tuangalie namna ya kuwafanya wawe na mazingira bora Polisi na yeye ni mtu. Mimi naangaliaga mara nyingi sana ukipita barabarani wale ma-traffic wanasimama juani muda mrefu sana lakini wanaenda kujishikiza kwenye magari yao hebu tutafuteni utaratibu, hata kama ni kutengeneza mobile vinyumba ambavyo wanaweza kupeana wakati wanabadilishana shift, mmoja akapumue pale nao watu. Wadada wa watu wanaingia kule Jeshini wakiwa weupe wanatoka weusi kwa sababu ya jua, mimi naomba na wenyewe tuwatazame. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho niombe kwa umahsusi wake…

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)