Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Kwa sababu ya muda hatutaweza kutoa ufafanuzi wa michango yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameiwasilisha, lakini niwaahidi kwamba tutaichukua na tutaifanyia kazi na mengine tutaweza kuwasilisha majibu yake kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, katika michango ya Waheshimiwa Wabunge hasa hasa imejikita katika maeneo makubwa matatu, eneo la kwanza ni kuhusiana na changamoto ya mazingira ya askari wetu ambayo wanafanyia kazi, lakini lingine linahusu mazingira pamoja na vifaa ama zana za kufanyia kazi. Waheshimiwa Wabunge wengi wameonesha kuguswa kwao na jinsi ambavyo askari wetu wa vyombo vyote vya usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wanavyoishi katika mazingira ambayo ni duni, vituo vya kufanyia kazi hususani Vituo vya Polisi, Magereza na kadhalika, vikiwa katika hali mbaya na maeneo mengine havipo kabisa. Pia katika masuala yanayohusu vyombo vya usafiri, mitambo mbalimbali ya kisasa ya kufanyia shughuli zao zikawa nyepesi zaidi na mengineyo.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la pili ambalo Waheshimiwa Wabunge wameligusa zaidi ni eneo la weledi wa askari wetu. Kwa hiyo linagusa masuala ya umuhimu wa mafunzo, vifaa vile vile vya kufanyia hayo mafunzo stahiki ya askari wetu na mengineyo ambayo kwa ufupi nitayafafanua baadaye.
Mheshimiwa Spika, lingine la tatu ni suala la uadilifu, ambapo hapa linahusisha mambo mengi ikiwemo suala zima la kuwa na mifumo ambayo inaweza ikasaidia kupunguza ubadhirifu hususani kwenye kukusanya maduhuli, lakini pia katika eneo la enforcement kwenye suala la kusimamia sheria na eneo la mafunzo halikadhalika linaingia hapa. Sasa haya ndio maeneo matatu ambayo nimeona nichukue muda huu wa dakika 10 ulizonipatia kuweza kuyatolea ufafanuzi kwa haraka haraka.
Mheshimiwa Spika, nianze na hili eneo, lakini kabla sijazungumza nataka niwakumbushe suala moja. Nilipokuwa nasoma hotuba leo asubuhi, nilieleza kitu kimoja kikubwa sana na nina hakika Waheshimiwa Wabunge watakikumbuka, nilieleza kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mara hii amefanya mapinduzi makubwa ya kibajeti katika vyombo vya usalama vilivyopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Nikatoa takwimu kuna ongezeko la fedha nyingi sana. Kwenye fedha za maendeleo zimeongezeka kwa wastani wa zaidi ya Sh.112,942,900,000, lakini katika eneo linalohusu matumizi mengineyo na kwenye kuna zaidi ya Sh.80,000,000,000 zimeongezwa kwa mara ya kwanza chini ya utawala wa Mama Samia Suluhu Hassan. Hii ni dhamira yake ya dhati na mapenzi yake aliyokuwa nayo makubwa kwa vyombo vyake vya usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais ambayo leo Waheshimiwa Wabunge hapa wakipitisha bajeti hii tunakwenda kuona changamoto hizi walizozungumza kwa kiasi fulani zinaanza kupatiwa ufumbuzi, pamoja na mambo mengine ambayo nilieleza asubuhi yanayohusu ubunifu.
Mheshimiwa Spika, katika suala la mafunzo ambalo lina mchango mkubwa sana katika kuimarisha weledi na uadilifu wa Askari wetu, hili na lenyewe limetendewa haki. Kwa mara ya kwanza katika historia, baada ya muda mrefu, leo hii Askari Polisi kama nilivyozungumza asubuhi, wametengewa bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 16.6 kwa ajili ya kwenda kwenye mafunzo bila ya kukatwa hata senti tano. Hili ni jambo ambalo kwa kweli linahitaji sana kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kuweza kuwaona Askari wetu na hiki kilio chao cha muda mrefu kuweza kukipatia ufumbuzi. Ni imani yangu sasa hii itasaidia kujenga uwezo wa Askari wetu na kuimarisha vile vile morale ya Askari hawa katika kutekeleza majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika bajeti hii vile vile fedha hizi ambazo mmeziona zimeongezwa zimegusa katika maeneo yanayopelekea kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuzuia uvunjifu wa ukusanyaji wa mapato hayo. Kwa mfano, katika maeneo ambayo yametajwa, nampongeza sana Mheshimiwa Deus Sangu, amezungumzia kuhusiana na suala la mfuko wa tuzo na tozo; bahati mbaya kwa sababu ya muda siwezi kueleza.
Mheshimiwa Spika, katika jambo moja ambalo tunachukua hatua ya kibajeti, ni kuhakikisha kwamba sasa tunakuja na mfumo ambao utakuwa ni madhubuti katika kusimamia mfuko wa tuzo na tozo, badala ya utaratibu wa sasa hivi ili kuepusha kukutanisha binadamu ambao mara nyingi inaweza kuchochea mazingira fulani ya rushwa. Kwa hiyo, moja katika jambo ambalo tunafanya katika bajeti hii ni ku-address tatizo la Mheshimiwa Deus Sangu kwenye hilo tatizo la tozo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine la mifumo katika bajeti hii linakuja kuangaliwa kutokana na kazi nzuri ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, ni eneo la kwenye masuala ya kinga na tahadhari za moto kwenye Jeshi la Magereza. Kumekuwa na kwenyewe kuna mianya fulani ya upoteaji wa fedha katika kutoa elimu na kwenda kufanya ukaguzi. Maeneo haya yameangaliwa na tunakuja sasa na mifumo ambayo itasaidia kupunguza upotevu huo.
Mheshimiwa Spika, mifumo hii siyo tu katika masuala ya maduhuli na kadhalika, lakini hata katika kuimarisha utendaji kazi wa Askari wetu. Leo hii watu wamekuwa wakilalamika kuna msongamano Magerezani, lakini moja katika sababu hiyo ni ucheleweshaji wa upelelezi; na wakati mwingine ucheleweshaji wa upelelezi huo unaweza kuwa unachangiwa na kutokana na vitendea kazi duni.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, leo katika bajeti hii tumeweza kuweka fedha za kuridhisha kwenye kitengo cha Finance cha Jeshi la Polisi ili tuweze kuhakikisha kwamba tunasaidia kuongeza weledi katika kukusanya taarifa za kipelelezi na taarifa hizo ziweze kutumika kwa ufanisi zaidi katika kutoa maamuzi ya wahalifu ama kwenye kesi zinazoendelea Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, mambo ni mengi, hata katika mfumo wa kiintelejensia na mengineyo. Naomba niende haraka haraka kwa sababu ya muda, nisije nikaacha na mengine nisiyaguse.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo lilizungumzwa ni hoja ya stahiki za Askari. Ni hoja ya msingi, lakini nataka nitoe mfano mmoja kwa haraka haraka. Katika bajeti hii tuna zaidi ya shilingi bilioni 1.56 ambazo zinatumika kwa ajili ya kulipa wastaafu. Kwa hiyo, utaona kwamba safari hii changamoto ya wastaafu kulipwa stahiki zao inapatiwa ufumbuzi kwa kuongeza fedha ya kiwango kikubwa katika bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo katika bajeti hii ya Mama (naiita) imefanya hoja za Waheshimiwa Wabunge ziweze kupatiwa ufumbuzi ni kwenye suala zima la kuimarisha mazingira ya makazi ya Askari wetu, mazingira ya vituo vyetu vya Polisi, mazingira ya vifaa vya kufanyia kazi, mazingira ya mitambo, Magereza yetu; yote haya mkiangalia kitabu cha bajeti mtaona kuna hatua kubwa sana imepigwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, naomba nirudie kwa haraka haraka kwenye mambo ambayo nadhani tumeyagusa. Nikiangalia kwenye eneo la ujenzi wa Askari, tumekuja na mpango kabambe wa miaka 10 wa kukabiliana na changamoto ya makazi ya Askari. Katika mpango huo ambao utaanza mwaka 2022/2023 mpaka 2031/2032 mpango huo wa miaka 10 tunatarajia kujenga nyumba zaidi ya 51,780 za Askari. Tukifanya hivyo maana yake changamoto ya makazi ya Askari tutakuwa tumeipatia ufumbuzi kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kana kwamba hiyo haitoshi, katika mpango wetu huo tunatarajia kujenga ofisi 44 za Makamanda wa Mikoa; ofisi 12 za Wakuu wa Vikosi; Ofisi 135 kwenye ngazi ya Wilaya; na zahanati na kadhalika. Kwa hiyo, hayo ni mambo ambayo ni makubwa sana, ingawa kuna mambo mengine ambayo tunajaribu kuyafikiria, sikutaka kuyazungumza kwenye bajeti kwa sababu ni masuala ambayo wakati muafaka utakapofika tutayazungumza.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya kuwaonesha Waheshimiwa Wabunge dhamira ya dhati ya Serikali katika kukabiliana na changamoto hizi za makazi, changamoto za vituo vya Polisi na kadhalika, tuna mipango mingine mbadala; na moja katika mpango ambao nataka niudokeze sasa hivi kwa haraka haraka, niliuzungumza katika hotuba asubuhi kwamba tunadhamiria kuimarisha mashirika yetu ya uzalishaji mali ili yaweze kufanya kazi kibiashara.
Mheshimiwa Spika, mashirika haya yaliundwa kwa dhamira ya kusaidia kutatua changamoto za vyombo hivi. Kwa sasa hivi tumekuja kwa mpango madhubuti na mkakati thabiti wa kufanya mashirika haya yajiendeshe kibiashara. Ni imani yangu katika muda siyo mrefu sana, tutaona matunda makubwa ya contribution ya mashirika haya katika kutatua changamoto za Askari ikiwemo za makazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mambo ni mengi ambayo nadhani katika kipindi kijacho tutaona mabadiliko makubwa sana ya vyombo vyetu hivi vya usalama kuanzia ujenzi wa Magereza, vituo vya zimamoto, ofisi za Uhamiaji na kadhalika. Hata magari haya ambayo yamezungumzwa, nina hakika katika bajeti hii tumefanya kwa kadri bajeti inavyoruhusu kwa mfano Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia kuhusu changamoto ya Jeshi la Magereza katika kupeleka mahabusu; ingawa tumetenga fedha katika bajeti hii kwa ajili ya kununua magari 32 ikiwepo magari 10 kupeleka mahabusu.
Mheshimiwa Spika, kwa kupitia mikakati hii ambayo nimeieleza, maana yake sasa tunakwenda kuzungumzia magari ya kutosha kwa Magereza kupeleka mahabusu, tunakwenda kuzungumzia kutatua changamoto nyinginezo ikiwemo na msongamano wa wafungwa Magerezani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili eneo la zana; ninapozungumzia hoja ya msongamano wa wafungwa ambayo imezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge; moja ya sababu kubwa inachangiwa na hivi vifaa vya kufanyia kazi ama zana za kufanyia kazi ama vitendea kazi ikiwemo Magereza yetu. Kwa hiyo, tuki-address hoja ya ujenzi wa Magereza, lakini wakati huo tuna mikakati mingine ambapo hili nimeona nilizungumze kipekee kwa sababu limeguswa sana na Waheshimiwa Wabunge la msongamano wa wafungwa, kwa hiyo, kuna mikakati mingine ya kipekee ambayo haihusiani na miundombinu peke yake, ni kama Serikali tunavyofanya.
Mheshimiwa Spika, moja katika mikakati hiyo ni kutumia sheria zetu. Tuna sheria kama nne ikiwemo sheria ya EML, ya kifungo cha nje; kuna Sheria ya Parole, kuna Sheria ya Uangalizi, kuna Sheria ya Huduma ya Jamii. Vile vile nataka nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, amekuwa akitumia mamlaka yake ya kikatiba kupunguza msongamano wa wafungwa kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka uliopita peke yake tumeshuhudia zaidi ya wafungwa 9,730 wakiachiwa huru kupitia msamaha wa Mheshimiwa Rais. Kupitia hizi sheria nne nilizozitaja hapa, kuna wafungwa wengi ambapo kila mwaka wale ambao tutakuwa tumejiridhisha wamerekebika tutaendelea kuwaachia ili kupunguza msongamano wa mahabusu Magerezani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika tunaendelea kufanya utaratibu wa kushirikiana na mamlaka nyingine. Kwa mfano, tuna utaratibu ambao tunashirikiana na Ofisi ya DPP, Ofisi ya TAKUKURU ya kuharakisha ama kuhamasisha ushirikiano kwa kushughulikia mashauri ya kesi jinai. Katika kufanya hivyo, Kamati hii inapita katika Magereza kuweza kupitia na kuangalia uwezekano wa aidha kuwaachia wale mahabusu wanaostahili kuachiwa.
Mheshimiwa Spika, hili jambo ni muhimu kwa sababu tunapozungumzia msongamano wa wafungwa haugusi katika eneo la wafungwa peke yake, sehemu kubwa vile vile ina mchango wa mahabusu. Kwa hiyo, tutaangalia njjia ambazo tutatumia kutatua changamoto ya msongamano wa wafungwa, lakini kwa utaratibu huu tunakwenda kutatua tatizo la msongamano wa mahabusu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hiyo ni miongoni mwa mikakati ambayo tunafanya. Pia katika eneo hili, tunaendelea kufanya mambo makubwa sana katika bajeti hii. Nilizungumza kwamba sasa katika Magereza yetu…
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, dakika tatu, malizia.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ambayo ilizungumzwa kuhusiana na ajali za barabarani na hususan ajali za bodaboda na hoja ya takwimu. Naomba nikiri kabisa, kama ambavyo hotuba yangu nilivyoisoma asubuhi, imeeleza kwamba kuna ongezeko kidogo la ajali za barabarani, ingawa nilieleza hatua ambazo kama Serikali tumechukua. Tokea hatua hizo tumeanza kuzichukua, tumeona kuna upungufu wa ajali barabarani. Ni imani yangu kwamba tukiendelea kusimamia mikakati ambayo tumeipanga, tutaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani.
Mheshimiwa Spika, tatizo la vijana wetu wa bodaboda linagusa maeneo mengi na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limeendelea kufanya jitihada kubwa za kupambana na ajali za vijana wa bodaboda. Ajali za bodaboda mara nyingi zinachangiwa na vijana hawa kutokufata sheria. Kwa hiyo, kuna hatua za kujaribu kutoa elimu kupitia kwenye vijiwe vyao, kupitia kwenye stendi mbalimbali wanazokaa, kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kufuata sheria za barabarani ili kuhakikisha kwamba wanasimamia sheria kwa wale ambao sasa baada ya kupewa elimu bado wanaendelea kukiuka sheria za barabarani.
Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi kama ambavyo nimezungumza katika hotuba yangu, ni kwamba sasa chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan, tunataka kufanya vyombo vyetu vya usalama vifanye kazi kisasa. Hivyo tuna mpango katika bajeti hii ya mwaka 2023 kupitia Bunge lako Tukufu kama ambavyo nimelieleza asubuhi, ni kwamba tuna mpango wa kuweka mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa uvunjifu wa sheria. Kuna project kwa lugha ya Kiingereza wanaita safercity (Miji salama) ambayo itahusisha uwekaji wa Kamera za barabarani na mitambo ya kisasa ya kubaini uvunjifu wa sheria ikiwemo uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.
Mheshimiwa Spika, hayo ni miongoni mwa mambo ambayo tunadhani tukiyafanya kwa pamoja yatasaidia sana kuweza kupunguza ajali za barabarani kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa hoja.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.