Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii, nami nitachangia katika maeneo mawili; eneo la lishe shuleni na eneo la hedhi kwa maana ya watoto wakike kukosa shule kwasababu ya hedhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea kuboresha elimu tunaongelea mambo yafuatayo: -
Mitaala jambo ambalo Serikali linaendelea nalo hivi sasa kwa hiyo nawapongeza, madarasa, madawati jambo ambalo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amelifanya kwa kiwango kikubwa na wote tumeshuhudia, vitabu, umeme, maji safi na salama, walimu, suala zima la TEHAMA shuleni tumesikia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba wanalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yote haya ili yaweze kuwa na tija ni lazima watoto wetu wanavyokuwa kwenye shule wapate chakula shuleni ni changamoto kubwa sana. Kwanza anafika shuleni hajala, halafu ashinde kutwa nzima shuleni akiwa anasoma huku akiwa na njaa. Wataalam wameshathibitisha kwamba njaa inamuathiri mtoto kuelewa, inamuathiri mtoto kuchanganua yale anayofundishwa na hatimaye inaathiri pia ufaulu wa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa WFP walikuwa wamefanya tathimini ya hali ya lishe kwenye shule duniani kote. Kwa hapa Tanzania ripoti yao ya mwaka 2020 ilionesha ya kwamba ni takribani watoto 500,000 mpaka 1,000,000 tu ambao wanapata uhakika wa lishe shuleni. Kwa maana hiyo idadi kubwa ya watoto bado hawapati lishe shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nilichangia mwaka jana naninarudia tena mwaka huu. Ijapokuwa nawapongeza Wizara kwa kuzindua mwongozo wa lishe shuleni lakini mwongozo ule hauna mpango wa jinsi gani ambavyo utatekelezeka na wala mwongozo ule hauna bajeti ya namna gani ambavyo suala hili litatekelezeka.
Mheshimiwa Naibu spika, Kwa hiyo, mimi ningependa kuishauri Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; kama ambavyo Serikali inapanga mipango mbalimbali na kutafuta wadau kama vile Benki za Maendeleo na Wadau kutoka nchi za maendeleo wafanye hivyo pia katika hili eneo la lishe shuleni. Mwaka jana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alihutubia kwenye mkutano wa UN Food Systems kule New York. Moja ya matokeo ya mkutano ule ilikuwa ni kuanzisha kitu kinachoitwa school meals coalition. Na coalition ile inapanga kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 kila mtoto kwenye shule atakuwa anapata angalau mlo mmoja wenye lishe bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana Desemba 2021 Global Partnership for Education (GPE) wametoa Dola milioni 580 kwa ajili ya kusaidia nchi za kutoka Barani Afrika kuimarisha lishe shuleni. Katika mpango huo Tanzania haijapata mgao.
Kwa hiyo, mimi ningependa kuwa challenge Wizara ya Elimu tuone namna gani na sisi tunanufaika kwenye haya maendeleo mbalimbali ya kidunia. Isitoshe mwenyekiti wa hivi sasa wa GPE ni Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete. Kwa hiyo, kwa nini tusimtumie maana mwenyekiti wa mpango huo wa GPE ni Rais wetu mstaafu? Sisi Tanzania iweje hatunufaiki na jambo hilo? Desemba 2021 wametoa Dola milioni 580, nchi za wenzetu kama Nigeria nakadhalika wamepata Tanzania haijapata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vivyo hivyo tukija kwenye USAID in Foreign Aid kwenye upande wa agriculture kwenye Serikali ya Marekani mwaka 2021 wametoa Dola milioni 248 kwa ajili ya lishe shuleni, na kila nchi imepata Dola milioni 25 za kuimarisha lishe shuleni, Tanzania haijapata mgao, kwa nini? Na window ya hivi karibuni ya kuomba ufadhili huo USAID ilikuwa ni mei 6, 2022, wiki iliyopita tu; zote hizi ni grants. Kwa hiyo mimi niwaombe Wizara ya Elimu ibebe ajenda hii ya lishe kwa uzito mkubwa kwa sababu yote haya tunafanya ikiwa watoto hawafundishiki kwa sababu ya njaa tunafifisha jitihada kubwa za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa TAMISEMI kwenye kitengo chao cha lishe wanasema kwamba katika kila darasa la watoto 45, 15 hawafundishiki. Sasa kama 15 hawafundishiki kwanini baadaye tunakuja kulalamika ufaulu umeshuka tunalaumu mitaala, tunalaumu walimu ilhali watoto wetu wanashinda njaa hawana lishe shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana nami hata kipindi hiki cha Bunge tulipokuwa kipindi cha Ramadhani tulifupisha muda ili kukidhi, kwa sababu mtu ukishinda na njaa akili haiwezi kufikiri salama, sasa tunategemeaje watoto shuleni waweze kuelewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi kwa mara ya pili tena na kwa masikitiko makubwa bado sijaona political will ya kutoka kwa Wizara ya Elimu kubeba ajenda ya lishe; hususani ukizingatia ajenda ya lishe ni moja ya ajenda za kipaumbele za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tangu akiwa Makamu Rais na hata sasa akiwa Rais ameendelea kusemea umuhimu wa ajenda ya lishe. Kwa hiyo, mimi naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapo hitimisha aje na mpango mahsusi wa kuhusu Serikali inapanga kufanya nini ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha lishe shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye eneo langu la pili. Mwaka 2021 NIMR wamefanya tafiti ya kuona ninamna gani ambavyo suala la hedhi linakosesha elimu watoto wetu wa kike. Kwa haraka haraka tafiti ile ilionesha watoto kuwa wengi wa kike hasa wa vijijini wanakosa shule kwa sababu yakuwa kwenye hedhi; na moja ya sababu ni kwamba hawawezi kumudu gharama za kununua pedi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi najiuliza; Wizara ya Elimu ina programu mbalimbali ambazo zinahusiana na masuala ya water sanitation and hygiene ambako jambo la hedhi linaingia pale, wanashindwa vipi kuingiza mkakati au kuja na programu ya kuhakikisha watoto wanaotoka kwenye kaya maskini wanapata taulo za kike ili wasikose shule kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika eneo hili naomba nipendekeze, kwamba tunayo TASAF ambayo ina jukumu la inahudumia kaya maskini; hivi kwanini kwenye TASAF tusiangalie, kwamba watoto wanaotoka kwenye kaya hizi maskini kuwe kuna intervention ya kuwawezesha wapate taulo za kike ili watoto hawa wa vijijini wanaotoka kwenye kaya maskini wasikose shule kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwezi mtoto anakosa siku tano mpaka saba kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi, na Serikali imeweka jitihada kubwa ya kuhakikisha kwamba mtoto wa kike apate elimu, wakati jambo la kibailojia, jambo ambalo si sababu amesababisha yeye mwenyewe linamfanya akose shule akiwa kwenye hedhi.
Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu, hii ni mara pili pia nachangia suala hili kwenye Bunge lako Tukufu, bado sijapata majibu yanayoeleweka kuhusiana na Serikali itakuja na mpango gani kuhakikisha kwamba mtoto wa kike hakosi shule kwa sababu ya hedhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi baada ya kusema hayo nasisitiza tena, kwamba Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kuna lishe shuleni, Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba mtoto wa kike hakosi shule kwasababu ya hedhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana na endapo sitaridhika na majibu ya Serikali nitashika shilingi ya mshahara wa Waziri. Ahsante.