Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nitumie nafasi hii nami kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kwenye Wizara hii na kwa mchakato mzima ambao tumeushuhudia wa kupitia upya Sera ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Geita Mjini Serikali ilikopa takribani bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA na Serikali ikafanya mchakato wote, ikatuletea Mkandarasi Skyway, akaanza kazi. Naamini Serikali ilitumia vyombo vyake kufanya due diligence, na katika mchujo mkubwa ikatuletea Mkandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa ambazo Mheshimiwa Waziri alizipata wa wakati huo, aligundua kuna kasoro na akasimamisha ujenzi kwa takribani miaka miwili. Amekuja kuruhusu ujenzi kuanza, yule Mkandarasi wa awali akaondolewa.Mkandarasi wa awali akiondolewa, alikuwa anadaiwa na wananchi wa Geita takriban Shilingi bilioni moja na laki saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina tatizo na kasoro za mkandarasi kwasababu Serikali ndiyo iliyomleta. Shida yangu ni kwamba Serikali ilitimiza wajibu wake wa kufanya due diligence, ikaleta mkandarasi kwa wananchi wa Geita ajenge Chuo cha VETA kwa fedha za mkopo bilioni 14 halafu Serikali hiyohiyo baadaye ikagundua anakasoro lakini ikawaacha wananchi wa Geita wakiwa na madeni wanadai bilioni 1.7 ikabadilisha mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya juhudi nyingi nimezungumza na Waziri aliyekuwepo, nimezungumza na Waziri Mkuu, nimezungumza na Waziri wa sasa, lakini Serikali inakaa pembeni kuonesha kwamba haihusiki. Sasa, mimi nilitaka kutumia hotuba yangu hii, leo Serikali inisaidie kujua wananchi hawa wanalipwa nani? Imebadili mkandarasi aliyekuja amekuta chini kuna matofali, amekuta chini kuna kokoto, chini kuna mchanga ametumia vilevile walivyo-supply wananchi wa Geita lakini Serikali inasema tulikuwa tumelipa mpaka vilivyo chini ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema ukweli, tumekuwa Serikalini, tunafahamu utaratibu, kwamba mkandarasi analipwa kwa ku-raise certificate, certificate ni ya kazi iliyofanyika. Mheshimiwa Waziri umemtuma Naibu Waziri amekuja lakini majibu ni kwamba mkandarasi yule alishalipwa zaidi ya kazi iliyokuwa imefanyika. Sasa wananchi wangu wa Geita wanalipwa na nani? Wanadai zaidi ya bilioni 1.7; mkandarasi amebadilishwa huku chuo kikijengwa kwa force accounts.

Mheshimiwa Naibu Spika, sioni ni kwa namna gani Serikali inatakiwa ikae pembeni kuhusiana na suala hili. Sisi hatukumtafuta yule mkandarasi, aliaminiwa na Serikali akaletwa kama Serikali hadai mkandarasi hadai maana yake ni kwamba huyu mtu alikuwa ana guarantee ameweka benki; zipo pesa, kazi ilikuwa kubwa, lazima wananchi wale walipwe. Wananchi wa Geita hawapaswi kuachiwa maumivu hayo kutokana na shangwe waliyokuwa nayo ya ujio wa Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili Mheshimiwa Waziri; tulifanyiwa presentation ya Ujenzi wa Chuo cha VETA; kinachojengwa sasa hivi ni majengo tofauti ambapo chini kuna matofali juu kuna fabrics sijui fabricated. Lakini, lengo la Chuo Cha VETA katika Mji wa Geita ni ku- capture soko la vijana wanaomaliza shule ili wafanye kazi kwenye migodi mikubwa inayozunguka eneo lile. Na focus yetu ilikuwa ni kuwa na Chuo cha VETA unique kutokana na wingi wa machimbo ya madini katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika leo baada ya mkandarasi mwingine kuja ni majengo ya aina tofauti, ni kubadilika kabisa kwa kitu kilichokuwa presented pale, na aliyekuja ni kukamilisha tu kama anakamilisha majengo yawepo lakini kazi inayofanyika ni tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri awahakikishie wananchi wa Geita, kwanza chuo kinachojengwa kiwe ni kilekile kwa mahitaji yaleyale ya ku-capture mahitaji ya soko la vijana wa maeneo yale ambao wanahitaji utaalamu kwa ajili ya madini na hakuna mabadiliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili; awasaidie wananchi wa Geita kuhakikisha kwamba chuo kinakamilika na wananchi wale, kama yule mkandarasi hadai Serikali iwasaidie wananchi wale kupata malipo yao, kwa sababu hawakujipeleka pale ,mkandarasi aliletwa na Serikali kama ambavyo wakandarasi wengine wanaletwa na Serikali haiwezi kuvua wajibu wa kuhakikisha wanachi wake wanapata haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza kwa nafasi, ahsante sana. (Makofi)