Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Esther Edwin Maleko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa pongezi kwa Wizara hususani kwa Waziri wetu na Naibu Waziri lakini pia na watendaji wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika sekta hii ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imefanyakazi kubwa ya kujenga shule nchini Tanzania na sasa kila mahali leo tuna shule. Tuna idadi ya shule takribani 24,000; hizi ni shule nyingi sana. Katika shule hizo shule za msingi ni 17,000 na shule za sekondari ni 7,000. Ninakipongeza sana Chama changu Cha Mapinduzi kwa kazi hii nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi wanaobebwa katika hizi shule tulizonazo tuna takribani wanafunzi milioni 14. Si hivyo tu, kati ya hawa wanafunzi kwenye shule hizi milioni 14 milioni 12 wapo katika Shule za Msingi na milioni mbili katika shule za sekondari. Hapa tunajiuliza swali la msingi, kama wanaandikishwa wanafunzi milioni 12 katika Shule za Msingi lakini wanaokuja kwenye Shule za Sekondari ni milioni mbili, huu upungufu mkubwa hivi katikati hapa hawa wanafunzi wanakwenda wapi? Ni swali la kujiuliza nani lazima Serikali iweze kufuatilia ili tujue upotevu huu wa hawa wanafunzi ambao wanaanza milioni 12 lakini wanakuja kufika Sekondari milioni mbili; tatizo linakuwa wapi tuweze kupambana na tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, leo elimu yetu ya Tanzania haimuandai mhitimu kuja kujiajiri au kuajiriwa; hiyo ni changamoto kubwa sana. Leo vijana wengi wanahitimu lakini hawa vijana wanapata wapi ajira? Wakati hakuna maandalizi mazuri ya wao kwenda kujiajiri au kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninashauri kuliko Serikali kupoteza mamilioni ya fedha kusomesha wanafunzi hawa na mwisho wakahitimu na bila kuwa na elimu ambayo au kwenda kuweza kujiajiri inakatisha tamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo ninashauri kwamba mitaala iendane na wakati huu uliopo tuibadilishe mitaala yetu iendane na wakati huu uliopo. Lakini si hivyo tu…(Makofi)

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa taarifa kwa muongeaji kwamba na hao wanafunzi wenyewe bahati nzuri wanasema kama inawezekana waangaliwe somo la Kiswahili kama nchi nyingine wanavyokuza lugha zao iwe ni somo la darasani kwa sababu si elimu ambayo wanakwenda kuifanyia kazi. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Malleko, taarifa hiyo.

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; naomba niendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninauliza hivi kuna haja gani kwa Serikali kupoteza mamilioni ya fedha kusomesha wanafunzi lakini hatima yake wanafunzi hao wanaenda kubaki nyumbani hawana ajira, hawawezi kujiajiri inakuwa ni mzigo kwa Tanzania. Hili bomu tunalolitengeneza baadaye litatulipukia sisi. Kuna vijana wengi sana ambao wamehitimu lakini hawana ajira, hawawezi kujiajiri kwa sababu hawajafanyiwa maandalizi hayo tangu wanaanza hizi shule za msingi, sekondari na mpaka wanapoenda kuhitimu katika vyuo vikuu. Kwa hiyo, ninaomba sana Serikali yetu iweze kuwasaidia wahitimu hawa kupambana na changamoto za maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo vijana wengi ambao wamekosa ajira wengi wanakimbilia kwenda kujiajiri kwenye bodaboda; lakini kipato wanachopata ni cha kujikimu kwa wakati ule tu, kwa siku hiyo tu, na si kitu ambacho kinaweza kuwasaidia na kuwajengea uwezo au kuwasaidia kuendeleza maisha yao. Wanaishia kupata chochote kidogo ambacho kitawasaidia kujikimu kwa siku hiyo na kesho asubuhi waende kutafuta sehemu nyingine ya kuweza kuongeza kipato chao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Serikali yetu iangalie elimu kwa sababu elimu ndicho kitu kikubwa ambacho kinaweza kuwasaidia watanzania kutoka pale walipo kwenda mahali pengine. Elimu hii kama haitazingatiwa kuwasaidia hawa watu ambao wanaenda kuhitimu waweze kujiajiri ajira leo ni shida. Kwa hiyo, tutengeneze mazingira ya vijana hawa wakihitimu waweze kwenda kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, mchango wangu wa leo ni huo. (Makofi)