Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali yayote namshukuru Mwenyezi Mungu kuturuzuku uhai na afya njema. Pia napongeza kazi nzuri inayofanyika na Wizara hii muhimu na naona viongozi wake wapo mahiri; na hata kazi hiyo imejionyesha hasa wanaposimamia miundombinu. Sisi kama kamati tulitembelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya miradi ya ujenzi tumeona kule Arusha Technical, kule MUST Mbeya na kwingineko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri ambaye tulikuwa naye kwenye ziara; kwa kweli ni mahiri yeye kweli ni quantity surveyor mzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo kazi ya mitaala inayofanyika na Wizara hii. Mitaala hii nasisitiza ilenge kuandaa vijana wetu kwenye ufundi stadi pamoja na kilimo, biashara na vinginevyo ambavyo vitawawezesha vijana hawa kumudu maisha badala ya kuendelea kutegemea kusubiri ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najikita Mkoa wa Lindi; Mkoa wa Lindi vijana wale wanahitaji elimu ya fani mbalimbali. Pale Lindi Manispaa tuna Chuo cha VETA pale Mitwero, lakini chuo kile kinakabiliwa na uhaba wa wakufunzi kiasi kwamba hata malengo yanayotakiwa kufundishwa pale vijana wanakosa. Hivyo basi, tunaomba Wizara ifike muda mwafaka wawapatie wakufunzi pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kule Nachingwea kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa tuna chuo kidogo cha ufundi. Chuo kile kinawezesha vijana wanachingwea, Liwale, Ruangwa na kwingineko kote Mikoa ya Lindi na Mtwara kupata ujuzi wa ufundi stadi. Hata hivyo, chuo kile ni kidogo. Hivyo tunaomba Wizara ya Elimu ishirikiane na Wizara ya Ulinzi kukipanua chuo kile ili kitoe mafunzo kwa watu wengi na kwa stadi mbali mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana wakati wa Bunge la Bajeti niliuliza swali kuhusu uzio wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, na nikapata jibu zuri tu, kwamba fedha zimetengwa. Lakini hadi leo ninavyozungumza bado fedha hazijaenda na bado kazi haijafanyika. Sasa imefikia muda sasa naomba fedha hizo zipelekwe pale kwa ajili ya ujenzi wa uzio ili kuhakikisha usalama wa vijana wetu wanaosoma chuo cha uwalimu Nachingwea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mpango wa Chuo Kikuu Dar es salaam kujenga tawi kule Mkoa wa Lindi, pale Lindi Mjini; lakini hadi sasa hivi kasi yenyewe inavyokwenda bado si nzuri. Naomba kwa Wizara hii, chonde chonde, shughuli ile iharakishwe ili vijana wa Mkoa wa Lindi na kwingineko wapate elimu ya fani mbalimbali ili nao waweze kujiajiri kwaajili ya kumudu maisha na kuondoa umaskini unaokithiri katika maeneo yale. Ninaomba sana, sana katika Wizara hii waangalie elimu kwa eneo la pembezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)