Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nimpongeze Profesa Mkenda kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Nitazungumzia eneo moja tu, eneo linalohusiana na tafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameizungumza vizuri sana katika ukurasa wa 11, lakini vile vile akasherehesha katika ukurasa wa 66. Nampongeza na naipongeza Wizara kwamba imevuka malengo yake katika idadi ya tafiti ambazo ilikuwa imejipangia, tafiti 129 lakini wakaenda kufanya tafiti 143.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nianze mchango wangu kwa kumwangalia Mwanafalsafa mmoja, aliishi miaka mingi sana. Huyu bwana alikuwa na umri wa miaka 70 na aliyazungumza maneno fulani hivi kati ya mwaka 1072 alipozaliwa, yeye alifariki mwaka 1142. Yeye anasema nini katika upande wa utafiti. Anasema na naomba nitumie lugha ya Kiingereza:

“The world will come to prove the researches shall become a crucial factor to moving the world to prosperity”.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa alikuwa anasema, dunia itakuja kuthibitika au kuthibitisha kwamba tafiti ndizo zitakuwa ni majawabu katika kuondoa au kutafuta hali njema za watu duniani na maendeleo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikajaribu tena kwenda mbele zaidi, kuna msomi mmoja kutoka Ugiriki, huyu anaitwa Atanasis Valevanidis kutoka Chuo Kikuu cha Athens kinachoitwa National and Kapodistrian. Huyu bwana anasema nini? Huyu bwana naye alifanya utafiti juu ya nafasi ya Vyuo Vikuu katika kufanya tafiti zinazotafuta majawabu ya maisha ya watu katika nchi zao na maendeleo yao. Hivyo anathibitisha na kusema

“Dunia sasa imekubaliana kuwa research and development kuwa ni nyenzo muhimu sana katika kuipeleka nchi yoyote including Tanzania, nchi yoyote katika kutafuta majawabu ya matatizo yao”.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaona ni kwa jinsi gani vyuo vikuu vimekuwa ni chanzo kikubwa sana cha ufanyaji wa tafiti. Sasa hapa kuna swali moja ambalo napenda kujiuliza.

Ukiangalia katika Vyuo Vikuu vya nje ambavyo nitatoa mfano, Chuo Kikuu cha Manchester; Chuo Kikuu cha Manchester ni moja katika vyuo vikuu ambavyo vinajisifu sana, vinajitanua sana, katika masuala ya research; wenyewe wameshafanya research za maji salama kwa watu maskini kama sisi kwenye nchi zinazoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, researches zile zikifanyika zinakwenda kuwa-commercialized lakini vilevile zinakwenda kutumiwa. Wamefanya research nyingi sana. swali linalokuja ni kwamba sisi hapa tunapopata matatizo Vyuo Vikuu vyetu vinatutoa katika matatizo? Tulipata hapa matatizo ya Corona, kama siyo kama Mheshimiwa Shekilindi kutusaidia, vyuo vikuu vyetu vilikuwa vimekaa tu kimya ukiondoa COSTECH nafikiri walifanya kazi fulani hivi. Sasa ninapojaribu kusema, nataka hili nimuulize Profesa, wakati akihitimisha; nimeangalia University of Dar es Salaam hakika wanafanya kazi kubwa sana, lazima tuwapongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika site yao pale wanakuonesha ni jinsi gani research muhimu sana za kisomi, zinazotafuta majawabu katika matatizo tuliyonayo; matatizo ya kisayansi, kilimo, energy na ya kimaskini, lakini najiuliza ni research ngapi Mheshimiwa Profesa Mkenda wanakwenda kuzitumia? Ni ngapi zinatumiwa au zimebakia katika shelves? Ukichukua hata zile za undergraduates, wengine wanakuja na topics za maana kabisa. Je, kuna extension zozote zile za research ambazo zinafanywa au watu wakishafanya research zimewekwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia moja ya kazi ya Wizara hii kubwa kabisa ni tafiti; wenyewe hii ni katika moja ya kazi zao na ni kazi ya kwanza. Ningependa Tanzania hii, iweze kuthamini masuala ya researches, lakini vile vile Serikali iweze kupanga fedha za kutosha kuweza kufanya tafiti hizi. Ndiyo maana baadhi ya maamuzi yetu yanakwenda kuwa na matatizo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, researches hizi zitatusaidia hata policy makers kujua wanatengeza policy za aina gani, sera za aina gani kuisaidia nchi. Bila ya kufanya tafiti tunaweza tukakuta, kama tulivyofanya wakati Fulani, silipendi jambo hili lakini nalisema kwa sababu ya uchungu, tuliuza nyumba za Serikali, si mnakumbuka? Tuliuza nyumba za Serikali, tulifanya tafiti kweli kwamba kile kitendo cha kuuza nyumba za Serikali kilikuwa na manufaa kwa Taifa hili? Utafiti ungekuwa umefanyika mapema na ukatoa majawabu kwamba kuuza nyumba za Serikali kuna faida, hakika ingeweza kutusaidia kujua tunachokifanya kinatusaidia ama hakitusaidii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba naunga mkono hoja hii, lakini nitafurahi sana kumsikia Profesa akileta majawabu ya aina ya tafiti zilizofanywa Tanzania na zile ambazo zimeweza kuisaidia nchi hii. Ahsante sana. (Makofi)