Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba ya Wizara ya Maji tunayoijadili. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameturuzuku uhai na ameendelea kutuongoza.

Mheshimiwa Spika, nitangulie kusema naunga mkono hoja hii. Natangulia kuunga mkono hoja hii kwa sababu ya kazi kubwa inayofanyika. Nataka nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jinsi alivyoonesha nia ya dhati ya kuhakikisha tunaondokana na tatizo la maji kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwapongeze Waziri na timu yake Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tumeanza kuona mabadiliko ya jinsi tunavyoshughulikia sekta yetu ya maji. Miaka miwili mitatu iliyopita tulikuwa tukija hapa tunalalamika jinsi ambavyo fedha zinapotea kwenye miradi ambayo haioneshi manufaa. Kwa kiasi kikubwa hili tumeweza kulidhibiti, hongereni sana Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili niwashukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji ndani ya Wizara hii kwa jinsi ambavyo mmetukimbilia watu wa Mkinga. Nimekuwa nikipiga kelele katika Bunge hili kwa tatizo la maji katika Wilaya ya Mkinga na kuna wakati nilisema kama kuna Wilaya katika Mkoa wa Tanga yenye tatizo kubwa la maji ni Mkinga, mmeanza kutuelewa tunawashukuru. Watendaji wote wakubwa wa Wizara mmefika Mkinga kuja kuona tatizo na ninyi mnajua kwamba, tatizo Mkinga ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie kwa mwaka huu tatizo limekuwa kubwa zaidi tofauti na mlivyokuwa mnalifahamu. Mabwawa yetu ambayo walao yalikuwa yanatusaidia, mabwawa matano yamekauka, kwa hiyo wananchi wetu wa Kata zile ambazo mlikuja kuzitembelea walikuwa na shida kubwa ya maji kwa sababu mabwawa yalikauka, walikuwa hawana uwezo wa kupata maji tena. Kwa hiyo, tunapoona jitihada hizi za timu yako kuja kwenye Jimbo kuandaa na kutengeneza mradi ule wa kutoka Mto Zigi mpaka kule Horohoro na kwa ahadi ile mliyotupa kwamba, mwezi wa Sita mradi ule unaanza, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba ahadi ile iwe kweli. Mwezi wa sita tuliokubaliana mradi ule uanze. Vijiji vile 24 vitakavyoguswa na mradi huu viweze kupata maji. Tuweze kufungua ukanda ule wa bahari wa Mkinga ili hoteli na shughuli za kiuchumi ziweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, malengo ya Sustainable Development Goal yanaiweka sekta ya maji kwenye lengo Namba Sita, ambayo tunasema tunajielekeza kwenye upatikanaji wa clean water and sanitation. Na kwa nini tumeweka lengo hili kama dunia? Ni kwa sababu ya changamoto kubwa ya kidunia iliyokuwa inaonekana kwamba watu Bilioni 2.6 walikuwa hawana uhakika wa maji. Watu Milioni 1.63 watoto wenye umri wa miaka mitano wanapoteza maisha kila mwaka kwa sababu ya tatizo hili. Dunia ikaamua kwamba maji sasa iwe ni human right. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiliacha hilo lipo lile la kawaida ambalo kila siku tunaambiana, maji ni uhai. Tumesema hivyo tumezoea-zoea tunaona ni jambo la kawaida tu, lakini vilevile maji ni ulinzi kwa nchi. Tunaziona nchi zinapigana vita kwa sababu ya maji, kwa hiyo sekta hii hatuwezi kuipuuza hata kidogo. Waziri kwenye takwimu zako umetuambia lengo letu ni kufikisha aslimia 85 ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini, ukurasa wa nane. Leo hii tumefikia asilimia 74.5 bado tuna safari. Katika eneo ambalo halipaswi tushindwe kufikia malengo ni kwenye sekta ya maji. Nawaomba Wabunge wenzangu tufanye kila linalowezekana Wizara hii iweze kupata fedha za kutosha tuweze kuondokana na tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri mlipokuja kutembelea miradi yetu Mkinga tulikwenda kule Mwakijembe. Bwawa lile lilishindwa kuendelea, tuliingia kwenye mgogoro na Mkandarasi tukaenda kwenye arbitration. Tangu mwezi Disemba arbitration imeisha, tuna kigugumizi gani cha kuhakikisha tunampata Mkandarasi mwingine wa kuweza kutekeleza mradi ule? Huu ni mradi ambao umesimama kwa miaka mitatu Mheshimiwa Waziri. Ni mradi ambao upo kwenye Kata ambayo haina mradi wowote wa maji ya bomba. Tuna mabwawa mawili kule, tuna bwawa la Mwakijembe ndiyo hoi, tuna Bwawa la Mbuta.

Nimekuja wiki iliyopita tumekaa tumezungumza, tulisema tukamilishe ujenzi, tumefikia hatua nzuri, lakini kuna certificate pale. Umeniahidi kwamba hivi karibuni Milioni 90 zile zitapatikana, naomba zipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana kuna kazi ile ya kukamilisha ujenzi wa kuweka zege na kwenye utoro wa maji ili bwawa lile lisije likapasuka tikapoteza fedha zote tulizozifanya. Mvua sasa zimeanza, sio nyingi kihivyo, lakini tukichelewa zikija mvua kubwa Bwawa lile likapasuka kazi yote tuliyoifanya itakuwa haina maana. Naomba tulifanyie kazi jambo hili kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru kwa miradi ya Gombero na Mhinduro. Taarifa nilizonazo ni kwamba, negotiations zimekamilika. Tunaomba tuweze kumuita kwa haraka yule Mkandarasi tuingie mkataba ule ili kazi ile ianze. Ninawashukuru kwa mradi wa mapatano nimeambiwa mradi umeshasainiwa, kuna Saini kama moja tu imebaki, naomba tusaini kwa haraka ili mradi ule nao uweze kufanyiwa kazi, huku kwenye miradi hii ndiko chanzo cha Mto Zigi, wao bado wanayatazama maji yanakwenda kunywewa Tanga. Tunaomba tuwakamilishie miradi hii ili na wao waone thamani ya kulinda vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, nichukue fursa hii kuwashukuru kwa miradi ile ya UVIKO, tunashukuru kazi kubwa imefanyika. Nitumie fursa hii kuwashukuru wenzetu wa Nyota Foundation, tulipopata tatizo kubwa lile la ukame mabwawa kukauka walitukimbilia wakatuchimbia visima vitano. Walituchimbia kisima pale Horohoro kijijini, wametuchimbia kisima Horohoro border, wametuchimbia visima viwili Maforoni, wametuchimbia kisima Mwakikonge na bado wanaonesha nia ya kuendelea kutusaidia. Tunawashukuru sana, nachukua fursa hii kuwashukuru kwa niaba ya wananchi wa Mkinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wakati nikishukuru kwa ajili ya uchimbaji huu wa visima, nikushukuru kwa nia nzuri mliyoifanya kwenye bajeti ya mwaka huu ya kuidhinisha visima vitatu kwa Kata ya Mwakijembe na kule Horohoro. Masikitiko yangu ni kwamba…

SPIKA: Sekunde 30 malizia, kengele imeshagonga.

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, imechukua mwaka mzima kuweza kupata mkandarasi wa kuchimba visima vile. Kama inawezekana twendeni tukawape hawa Nyota Foundation na timu yao visima vile vichimbwe tuweze kuondokana na tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru. (Makofi)