Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii angalau ya dakika chache nami niweze kuzungumzia mambo ya maji Jimboni kwangu Handeni Mjini.

Mheshimiwa Spika, mara ya mwisho wananchi wa Handeni Mjini kupata mradi wa maji ilikuwa ni mwaka 1974, na mradi ule ulikuwa ni wa miaka 20 life span yake. Hiyo ndiyo kusema kwamba tuna miaka karibia 30 wananchi wa Handeni hatujawahi kupata mradi mkubwa wa maji. Sasa nimesimama hapa leo kutoa shukrani zangu nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita kwa namna ambavyo ameiangalia Handeni kwa jicho la kipekee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa shukrani hizo kwa kaka yangu, ndugu yangu, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu wake, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Eng. Sanga. Niendelee kusema kwamba Wizara hii ya Maji kwa sababu inagusa matatizo makubwa sana ya Watanzania, kwa kweli inastahili kuwa na watu wa aina ya viongozi tulionao hapo kwenye hiyo Wizara. Ingekuwa ni kwa uwezo wangu, na kwa sababu sisi ndio washauri wa Serikali, tunashauri Waziri huyu aendelee kuwepo kuwepo pale aendelee kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa mara ya kwanza wananchi wa Kata ya Kwamagome, wamepata mradi pale Kwamagome unaopeleka maji Kwamagome na Hedi. Kana kwamba haitoshi, nilipokwenda Ofisini Wizarani, tumeongezwa fedha ili wananchi wa Lusanga, Sasioni, Lolopili na Mji mpya nao wapate maji. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa usikivu wako.

Mheshimiwa Spika, nashukuru zaidi kwa mara ya kwanza kwa historia ya nchi yetu Kata ya Malezi wamepata mradi wa maji wa Shilingi 324,000,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuomba katika kipindi hiki, Mheshimiwa Waziri mradi huu natamani sana tukauzindue kwa pamoja, twende pamoja tukauzindue na ule mradi wa Mabanda ambao wewe siku ile ulipokuja, usiku ule tulipokunywa maji pale, ulipiga simu tukiwa pamoja kwa Mheshimiwa Rais na usiku ule ule alikubali kutoa shilingi 671,000,000 ambazo zimejenga tenki kubwa sana pale Mankinda. Tunapeleka maji kata yote ya Mabanda na tunapeleka maji Kijiji cha Mankinda Kata ya Konje na tunayapeleka maji pale Wanyamakazi. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kata ya Kojamba tulipata Shilingi bilioni 1.96 ili kuchimba bwawa kubwa pale Kwinkambala, mkandarasi akatuzingua na sisi tukamzingua mara nne yake. Hivi ninavyozungumza, mkandarasi alishafukuzwa. Nitoe wito kwa Wabunge wenzangu, Mkandarasi akizingua site, tusingoje Serikali. Sisi wananchi tuna mamlaka ya kuwakataa wakandarasi ya ovyo ovyo. Kwa hiyo, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, ulikuja pale na umeshaweka utaratibu ndani ya wiki mbili kama ulivyoahidi kwamba tunakwenda kupata mkandarasi mwingine pale Kwinkambala. Kwa maana hiyo bado umeendelea kutusikiliza wananchi wa Handeni Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ametupa mradi wa shilingi 857,000,000, kinachimbwa kisima kikubwa pale Ndelema kuyapeleka maji Kwinkambala wakati tukiendelea kusubiri ujenzi wa Bwawa kubwa lile la Kwinkambala.

Mheshimiwa Spika, zaidi naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kufanikisha mradi huu wa miji 28. Mradi huu umezungumzwa hapa Bungeni kwa takribani miaka sita iliyopita. Wito wangu kwenye mradi huu, dola milioni 500 mkopo tunaochukua Serikali ya India, Benki ya Exim, miaka sita iliyopita milioni 500 ingeweza kufanya kazi kubwa zaidi kuliko leo. Kwa hiyo, kama process za mradi huu zimeshakamilika, chonde chonde mradi uanze.

Mheshimiwa Spika, mwisho nimalizie, Waswahili wanasema kushukuru ni kuomba tena. Wananchi wa Handeni Mjini wamenituma niombe tujengewe bwawa pale Mandela Kata ya Kwenjugo, pia tujengewe bwawa pale Kata ya Mabanda Bwawa la Kwamkole. Tukishakuwa na Bwawa na Kwinkambala tukawa na Bwawa la Mandela na tukawa na Bwawa Kwamkole, tafsiri yake ni kwamba tutakuwa na source nyingi za maji kwa Jimbo letu la Handeni mjini plus haya maji ambayo yanatoka kwenye huu mradi wa HTM yanayotoka Mto Ruvu kule Pangani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo napenda nitoe shukrani za dhati kwa Engineer Yohana Mgaza, Meneja wa HTM. Vile vile nitoe pongezi zangu za dhati kwa Engineer Hosea Mwingizi. Mheshimiwa Waziri hawa watu naomba wasihamishwe Handeni, wawepo waweze kutusaidia kwenye haya mapambano ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, nakushukuru sana kwa fursa hii. Ahsante sana, wananchi wa Handeni wakae mkao wa kula, tunakwenda kuiandika historia ya Handeni Mjini kupitia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na ndugu yangu Waziri Aweso.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakushukuru sana. (Makofi)