Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji jioni hii. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi, nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Juma Aweso kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuendelea na jahazi la kubeba dhamana ya kuhakikisha tunapata maji Watanzania. Nimpongeze dada yangu Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi naye pia kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuendelea kumpa msaada Mheshimiwa Waziri. Nimpongeze Ndugu Injinia Anthony Sanga Katibu Mkuu wa Wizara naye kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwa mtendaji mkuu wa hii Wizara pamoja na Naibu Katibu Mkuu wake dada yetu Kemikimba. Tuwatakie heri, Mwenyezi Mungu awasimamie katika utendaji kazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge nadhani mtaungana na mimi moja ya Wizara ambayo inatupa ushirikiano wa karibu sana ni Wizara ya Maji inayoongozwa na Mheshimiwa aweso. Mmekuwa karibu sana, lakini pia mmekuwa watu wenye kutuitikia kwa haraka sana tukiwapigia simu mnapokea, tukiwatumia message mnatujibu na hata tukiwaomba appointment mnatupa nafasi ya kutuona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo pia, niwapongeze wasaidizi wenu wa karibu sana ambao kwa sisi Wabunge wamekuwa wakitupa ushirikiano pale Wizarani nikianza na CPA Joyce Msilu ambaye amekuwa akitupa sana ushirikiano, huyu ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji. Makatibu wako wote wawili Gibson George pamoja na Jafari Athuman na wenyewe wanatupa sana ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wale akinamama secretary pale wasaidizi wako ofisini kwa kweli utawafikishia salamu zetu, siwafahamu majina wapo wawili pale, tukifika mara nyingi wanatupokea vizuri na wanatukirimu. Wakati mwingine hata tukija kama tuna njaa Mheshimiwa baada ya vikao vya saa 07:00 huwa wanatuweka vizuri pale. Hata kama kuna ka-OC kakuongeza Waziri walinde zaidi wale akinamama na Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowapongeza wasaidizi wako katika ngazi ya mkoa na wilaya nikianza na Mhandisi Lameck Kapufi ambaye ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tabora, lakini pia Engineer Hussein Nyemba ambaye ni Meneja wa Mamlaka ya Maji Igunga. Mkurugenzi Mtendaji, kijana ambaye anaupiga mwingi sana, lakini pia na Meneja wa RUWASA Mhandisi Marwa Mulaza pamoja na wasaidizi wao wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waswahili wanasema waswahili wanasema usiposhukuru basi hauna shukrani. Nilitaka kwenda na ule msemo wa Mheshimiwa Waziri, lakini nimeuchapia kidogo, mimi nilikuja na huu kwa maana ya kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pale kwetu Igunga tuna mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Viktoria ambao Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imewekeza bilioni 620. Maji yametoka Mwanza na kufika Igunga takribani kilometa 400, hii ni legacy kubwa sana ya Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi wa Jimbo la Igunga, lakini pia na kwa maeneo ya Mkoa wa Tabora ukienda Nzega pamoja na Tabora Mjini na sasa unaelekea maeneo ya Kaliwa, Urambo na Sikonge. Nawashukuru sana Wizara kwa kusimamia huu mradi mkubwa wa kihistoria ambao umetatua changamoto kubwa sana ya maji katika eneo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niwashukuru kwa kuendelea kutupa support, tuna miradi ya maji mmeendelea kutupatia. Niliingia Jimbo la Igunga takribani huu ni mwaka wa pili, lakini tuna miradi zaidi ya saba ambayo inafanya vizuri sana katika eneo letu. Tumepeleka maji mpaka kule Mwamashimba karibu na Shinyanga, eneo ambalo lilikuwa ni gumu sana kufikiwa na maji. Mheshimiwa Aweso tuliomba fedha ukatupatia kwa maombi maalum na sasa tunakunywa maji ya Ziwa Viktoria tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi pia ya maji mingine ambayo inaendelea na usambazaji, lakini nishukuru zaidi pia kwa mwaka huu wa fedha mmetutengea bilioni moja kwa ajili ya kuunda mfumo wa maji taka katika Wilaya yetu ya Igunga. Hii ni historia nyingine ambayo tutakwenda kuiandika tutakuwa na mfumo wa maji taka katika mji wetu, jambo ambalo katika hali ya kawaida ilikuwa haiwezekani, lakini kwa ushirikiano ambao umetupatia Mheshimiwa Aweso na umetutengea fedha, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia mambo mawili kama ushauri katika kuhakikisha tunaboresha kazi zetu za usambazaji wa maji. Eneo la kwanza ambalo ningependa kuwashauri jioni hii, sisi ambao tumebobea sana katika masuala ya kiutawala huwa tuna principle moja au kanuni inasema kwamba, unapoongoza eneo dogo mara nyingi tunategemea ufanisi ni mkubwa.

Sasa kuna eneo moja ambalo mnaweza mkaliangalia na wasaidizi wako mlifanyie kazi; kwenye wilaya ambazo zina mamlaka mbili za maji kwa mfano Igunga tuna mamlaka ya mjini ambayo ni IGUWASA na mamlaka ya vijijini RUWASA, jitahidini kuwagawia maeneo haya watu ili angalao waweze kusaidiana katika kutatua changamoto ya maji. Tusijikute hizi mamlaka za mjini kati ya maeneo ya Mamlaka ya Mji unakuta kwa mfano Igunga mamlaka yetu hii ya mjini inahudumia kata takribani tatu, lakini mamlaka hii ya vijijini ina kata zaidi ya 34 kwa hiyo, inajikuta mzigo mkubwa unamuendea yule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama unavyoelewa sisi hapa tuna life span, tuna miaka mitano, lakini bajeti yetu inakwenda annually na kila annual moja ina quarter nne. Sasa ukijikuta huyu ana miradi mingi kwa mfano RUWASA, kama mfano Tabora tuna majimbo 12 kama kila jimbo tu likiwa lina miradi minne maana yake ana miradi kama 48. Sasa miradi 48 kwa mwaka mmoja kwa mtu anayetegemewa mkoa mzima utekelezaji wake na ufanisi utakuwa mdogo ndio maana nimekuja na hii hoja ya kusema tuwapunguzie maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukachukulie mfano kwa Igunga ukimpa IGUWASA hata kata 10 yule mwingine akabaki na kata zile 20 ufanisi utakuwa ni mkubwa hata mwaka mmoja unapokuja kufanya tathmini performance unajikuta performance iko vizuri.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikasema nishauri hili mlichukue na ninadhani unaelewa tulifika Wizarani tukaliomba na umesema hivi karibuni utatupatia ile GN ili IGUWASA iweze kuongeza mtandao wao wa kutoa maji, tunashukuru sana kwa kupokea pia ombi letu hilo. Hili unaweza ukaliangalia pia maeneo mengine linaweza likasaidia kujenga ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili lilikuwa ni suala la manunuzi, hata mdogo wangu Mheshimiwa Arthur Makanika hapa aliliongelea. Ni suala la ku-centralize, ukifanya centralization katika mfumo wa manunuzi kwa mfano kwa Mkoa wa Tabora tunaposema majimbo 12, ukiwa na miradi minne-minne, anapofanya manunuzi mtu wa mkoani inapofikia hatua mfano inahitajika tu koki, mpaka itoke mkoani waanze zile process maana yake ndio hii unakuta mradi wa bilioni moja imekosekana koki ya milioni mbili hamna mradi unaendelea pale, tutaendelea kuwasumbua sana kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninadhani unakumbuka hata sisi Igunga lilitokea hili. Tulikuwa na mradi mmoja wa Mwalala ulikuwa chini ya RUWASA, ilikufa pump ilihitajika milioni 11 tu, ilitusumbua zaidi yam waka mmoja wananchi wakawa hawapati maji, lakini ulipotoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa IGUWASA alienda alipiga kambi pale siku moja, saa 07.00 usiku mzigo umenyanyuka, tumemaliza kwa sababu, mamlaka za mjini wana uwezo wa kununua wao wenyewe palepale wanafanya procurement katika ngazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa hiyo, angalieni Instrument Act ya RUWASA mbadilishe hii item. Mnaweza mka-categorize, kwenye ngazi ya wilaya kuna manunuzi labda ya kwenda mpaka milioni kadhaa, ngazi ya mkoa wanakwenda milioni kadhaa halafu na Taifa mnaenda na miradi mikubwa ya billions of money, sawa Mheshimiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hapo tutakwenda vizuri. Itawasaidia kupunguza sana jam ili matatizo madogomadogo haya sijui pump imeungua inahitajika waya milioni moja milioni mbili, ukaanza mchakato wa manunuzi wa kuchukua muda mrefu, tutajikuta tunakaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niwashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mnaoendelea kutupatia. Sisi tupo kazini kama ambavyo tunasema na mama yetu tunamshukuru sana anatenga fedha nyingi za miradi ya maji na sisi tunashukuru. Aliposema atamtua mama ndoo kichwani, kweli anamtua ndoo kwa vitendo na sisi tunasema sana tunaishukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Naunga mkono bajeti ya 2022/2023, ahsante sana. (Makofi)