Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Japo niliomba kuchangia kesho, lakini kwa sababu ya tayari umeshanipa ridhaa hii nami niwe miongoni mwa wachangiaji ambao wamechangia Wizara hii ya Maji, Wizara nyeti kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nitachangia maeneo matatu, la kwanza nitaanza na shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa ujumla, lakini la pili nitakuwa na maombi, la tatu nitatoa shukrani kubwa kwa Wizara kwa mambo makubwa waliyoyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kusema kama wenzangu walivyotangulia kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kazi kubwa, nzuri waliyoifanya, lakini nimshukuru mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana ya kwamba, bila yeye naamini kabisa nguvu ya Mheshimiwa Waziri ingekuwa hapa na sisi tusingepata kutoa pongezi kubwa ambazo leo tunazitoa kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa mambo makuu matatu, la kwanza ni kwa namna ulivyo mnyenyekevu kuwasikiliza Waheshimiwa Wabunge wanapokuja kwako na changamoto, namna unavyojishusha, hata pale ambapo hauna fedha unajua sina namna ya kutekeleza hili Mheshimiwa Mbunge analoniambia, lakini wewe unalibeba kuonesha kwamba, tayari una uwezo na kumpa matumaini Mheshimiwa Mbunge aliyekuja kwako, hili ndilo linalokubeba kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni namna ambavyo unaonekana kwenye dhamira ya dhati ya kutatua changamoto kubwa yam aji nchi hii. Hili nakuona kabisa pale unapozungumza na hata mtu anapokutana na wewe namna unavyojipambanua kuonesha kweli dhamira yako kuanzia uso, maneno unayoyazungumza na vitendo vyako ambavyo umedhamiria. Hili linakupa sifa kubwa sana kwenye pongezi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu nikupongeze kwa namna ambavyo nilivyokuja kwako baada ya uchaguzi, 2020 baada ya miezi mitatu tu. Nilikuja na changamoto kadhaa kwenye wilaya yangu, pale Shirati leo hii wanakuita mkwe, wanakuita kwa sababu walikuwa wana zaidi ya miaka 10 wanaomba huduma yam aji pale, kumi-kumi na mitano, baada ya uchaguzi ule Mheshimiwa Waziri uliniahidi ndani ya siku 100 eneo lile lote la Kata ile ya Mkoma wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kweli ndani ya miezi mitatu Mheshimiwa Waziri nikupongeze kwa kiasi kikubwa kwa sababu, baada ya miezi mitatu wananchi wa pale Shiratu walipata maji safi na salama na leo hii umenitengenezea jina, lakini umetengenezea jina Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla wake hasa ukizingatia kata ile miaka yote ilikuwa ni kata ya upinzani. Leo tunazungumza kwa kazi kubwa uliyoifanya wale wananchi hawana namna wanakupongeza na wanakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio huo mradi peke yake, kuna miradi kongwe ambayo ilikuwa imesimama ndani ya wilaya ile, kuna mradi wa Nyarombo. Mheshimiwa Waziri mradi ule ni zaidi ya miaka mitano na kuendelea, umekuja kwenye utendaji wako unafanya kazi. Mradi wa Kiamuameko Muge hivi ninavyokwambia unatoa maji. Mradi wa Roche zaidi ya miaka mitano huko nyuma, ninavyozungumza sasa hivi unatoa maji. Mradi wa Marasibora, mradi ambao ulikuwa ni kichefuchefu katika miradi uliyoitaja, leo ninavyozungumza na wewe unatoa maji. Mradi wa Nyambori ambao ulikuwa kimsingi yote hii ni miradi ambayo Mheshimiwa Waziri kwa namna unavyofanya kazi ninavyozungumza na wewe ndio maana nikasema ni lazima nikushukuru kwa kazi kubwa nzuri unayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nikushukuru Mheshimiwa Waziri katika utendaji wako ukiacha hii miradi ya nyuma, umenipa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, mfano fedha ya Uvico. Leo ninavyozungumza tunatekeleza mradi wa maji kwa fedha ya Uvico kutoka Shirati unakwenda Kata ya Raranya mpaka Ingrijuu kule. Mheshimiwa Waziri sina namna ya kukupongeza na kukushukuru kwa kazi kubwa nzuri unayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukushukuru wewe na kukupongeza nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana meneja wa wilaya yangu ya Rorya, Engineer James, ni kijana ambaye umeniletea baada ya kumuondoa yule aliyekuwepo na uliniahidi kwamba nakuletea kijana ambaye atafanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Waziri nikuombe utafute namna hawa vijana ngazi za wilaya wanaofanya kazi vizuri muone namna ambavyo mnaweza kuwapa promotion, ili waendelee kuwa na moyo wa kutekeleza yale ambayo Serikali imekusudia kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana. Naendelea kukushukuru kwa fedha ulizonipa kwenye mradi wa Kata ya Rabol katika vijiji vyake vyote vitano. Nikushukuru kwa fedha ulizonipa kwenye mradi wa Gabimoori kule Nyamagaro na mengine mengi Mheshimiwa Waziri umekuwa ukiyafanya. Pamoja na uzuri wa haya Mheshimiwa Waziri, nilivyoingia kwa status iliyokuwepo niliwahi kukwambia, wilaya yangu ndio wilaya inayozungukwa na maji kwa asilimia kubwa Mkoa wa Mara, zaidi ya asilimia 77 inazungukwa, asalimia 23 peke yake ndio nchi kavu ambayo utafanya shughuli za kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nakwambia leo inawezekana ukizunguka kwenye Mkoa wa Mara pamoja na haya mazuri uliyoyafanya inawezekana ndio wilaya yenye changamoto kubwa sana ya maji kuliko wilaya nyingine zote. Na nikakwambia kipindi tunaingia ni vijiji 12 peke yake kwenye wilaya katika vijiji 87 ndani ya wilaya vilivyokuwa vina maji, vijiji 25 vilikuwa vina miradi ambayo inaendelea, vijiji zaidi ya 50 havikuwa na mradi wowote wa maji katika utekelezaji wake, lakini nakushukuru angalao katika miradi hiyo ulivyoingia na hii niliyoisema hapa angalau leo tunazungumza zaidi ya vijiji 35 vina maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu ni nini Mheshimiwa Waziri; tunayo miradi miwili mikubwa ambayo ninaamini kabisa ukiweka fedha pale ninaamini kabisa utatusaidia kwa kiasi kikubwa. Mradi wa kwanza ni huu mradi wa miji 28. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kama ulivyotuahidi bajeti yam waka jana na saa hizi umesema tena hapa, pamoja na iliyokuwa inazungumzwa kwamba, miradi ile haitatekelezwa, nikuombe kwenye miradi ya miji 28 utuondolee hii aibu ambayo ipo ndani ya wilaya kwamba, tunazungukwa zaidi ya asilimia 77, maji sisi wengine wamezungumza hapa ni kilometa mia mbili na kwenda juu, sisi Mheshimiwa Waziri ndani ya mita mia mbili, ndani ya mita mia moja, kuna wengine ndani ya mita hamsini tunayaona yale maji, lakini hatuna maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu iliyoje kwa Mheshimiwa Mbunge kwa miaka nenda-rudi unakwenda kwenye maeneo yale unazungumzia maji ambayo wananchi wanayaoga, lakini hawana maji safi na salama. Nikuombe kupitia mradi wa miji 28 nafikiri wewe unafahamu na kwa sababu, umefika kule zaidi ya mara mbili tuondolee hii aibu kututekelezea kwenye ule mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna mradi wa vijiji ambavyo vilikuwa vinatekelezwa, vile ambavyo vinazungukwa na Ziwa Viktoria. Kwangu nina vijiji zaidi ya 20 ukiangalia kwenye ile takwimu, ukitekeleza haya mawili, vijiji ambavyo vinazungukwa na Ziwa Viktoria vijiji 20, ukatekeleza ile miji 28 ndani ya wilaya yangu utakuwa umeondoa asilimia kubwa sana ya upungufu wa maji. Na nikuombe Mheshimiwa Waziri katika hili tuachane na ule utaratibu wa kuzungumzia asilimia katika utekelezaji wa maji twende tuangalie namna ya kutaja vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mimi leo nikikwambia nina vijiji 87, vijiji vyenye maji ni 35, vijiji vilivyosalia zaidi ya 42 havina maji, hiyo ndio takwimu unayotakiwa Kwenda nayo. Ukienda na takwimu ya asilimia wakati mwingine yanachukuliwa maji yale ambayo yanaenda na msimu wa mvua. Tukisema hiyo asilimia ya utekelezaji wa maji kutokana na msimu wa mvua ile inatuchanganya kwenye rekodi zetu. Twende kwenye utekelezaji wa vijiji na kwa sababu umekwishafanya kazi kubwa sana uone vijiji vyote ambavyo tayari umefikisha maji vingapi havina maji na uende mpaka ngazi ya vitongoji usiishie kwenye vijiji peke yake kwa sababu, Kijiji kimoja kinaweza kikawa na vitongoji vinne, lakini maji yapo kwenye kitongoji kimoja. Ukienda kwa hiyo, status itakuwa ni rahisi sasa kujua na mipango yako ya mbele namna gani kwa kiasi kilichobakia uweze kukitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie niende kwenye maombi yangu mengine sambamba na hili. Kuna miradi ambayo Mheshimiwa Waziri ulivyokuja kufanya ziara ilikuwa inatakiwa itoe maji, kwa mfano Mradi wa Komuge. Nikushukuru kwa kiwango ambacho imekeishafanyika, lakini nikuombe kwa sababu, kuna fedha ambayo iliombwa kwenye bajeti huu unakwenda mwezi wa sita, wape fedha wale vijana ili waweze kutekeleza yale maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine wa Nyehara, Kijiji kile ambacho nilikwambia, Kata ya Chang’ombe. Wape fedha ili waweze kutekeleza ule mradi angalao tuweze kufika mahali na sisi tukasema tunajivunia yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikushukuru sana, la mwisho, nitoe shukrani sana kwa namna ambavyo nimeona vijiji umeviweka vinakwenda kutekelezwa kwenye bajeti ya mwaka huu. Kijiji… kinakwenda kutekelezwa kwenye bajeti ya mwaka huu, Bubumbi, Sota, Sakawa, Kabache, Roche, Osiri, Kwatia, Kirong’we, Mang’ore, Kyogo, kwa maana ya upanuzi wake. Chereche, Deti, Ochuna, Omuga, Orio pamoja na Makongoro. Mheshimiwa Waziri nikuombe hivi vijiji ambavyo nimetaja vimetengewa fedha, fedha ikienda naamini itafika itasaidia asilimia kubwa wilaya yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, pamoja na kwamba, umenishtukiza, lakini nimetoa mchango wangu. Nakushukuru sana, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)