Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie hii Wizara yetu ya Maji. Kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna alivyotuletea fedha kwenye majimbo yetu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee nimshukuru sana kaka yangu Waziri Aweso kwa kazi kubwa anayofanya ana sifa nyingi sana. Na hapa majuzi nimegundua sifa yake nyingine ambayo sikuwa naijua na ambayo inanifanya niendelee kumfagilia zaidi, nimekuja kugundua kumbe pia ni mshabiki wa simba. Kwa hiyo, ninazidi kukupongeza sana kwa kazi kubwa unayofanya na ni kweli tumeendelea kuona unavyoishi na misemo yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee pia, nimshukuru sana msaidizi wako, Dada yangu Mheshimiwa Injinia Maryprisca, Naibu Waziri wa Maji, anaupiga mwingi sana. Dada huyu sijui kama analala, lakini kwa kweli kazi kubwa anafanya. Nimemuona kwenye jimbo langu amefika tumetembea naye vijiji zaidi ya vinne, hakuchoka, hakula, ameenda kula jioni kule Bariadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimpongeze sana na nikuhakikishie kwamba, ulipofika pale Mkula ulisema ule mradi utafunguliwa hivi karibuni na kulikuwa na tatizo la pump, nikuhakikishie kwamba, pump imeshapatikana na wiki hii tulikuwa tunafanya water test na nina imani kwamba, mpaka mwisho wa mwezi mradi huu sasa wananchi wataanza kutumia maji pale kwa hiyo, nikushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee pia, nimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, kaka yangu Injinia Sanga. Anafanya kazi kubwa, anatusikiliza Wabunge, anatupa ahadi nzuri na ana ahadi pia amenipa nyingine, ninaomba aweze kufanya utekelezaji wake ndani ya mwaka husika wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru sana DG wa RUWASA kaka yangu Clement. DG anafanya kazi kubwa sana, upatikanaji wa maji vijijini; 2020 Jimbo la Busega upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 39, tunavyosema leo upatikanaji wa maji ni asilimia 64. Hizi ni jitihada kubwa sana za Mheshimiwa Waziri, jitihada kubwa sana za mkurugenzi wa RUWASA kwa kazi kubwa anayofanya kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimshukuru dada yangu Mariam, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu. Dada huyu anafanya kazi kubwa, anatuheshimisha sisi Wabunge na sisi tunasema tutampa ushirikiano kwa sababu yeye anatupa ushirikiano sana. Na niombe tu kama si namna ya kupanda basi msimuhamishe maana anafanya kazi kubwa, ila kama ni kupanda basi ruksa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze kijana mwenzangu, Engineer Ngangari ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Busega. Ni kijana msikivu, anasikiliza, ananishauri na mimi ninamshauri mwisho wa siku tunatengeneza kitu ambacho ni kimoja kwa ajili yaw ana- Busega.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri, ni Mjumbe wa PAC. Tumeenda kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na mamlaka, wapo mameneja na wakurugenzi wa mamlaka husika wanafanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba, wanasimamia miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano; tulienda Dar-es- Salaam tukakutana na DG wa DAWASA, aisee, brother big up sana, DG wa DAWASA anafanya kazi kubwa na zaidi ya yote amesimamia hata mapato ya ndani kuhakikisha kwamba, anayapeleka kwenye miradi. Hiyo ni sehemu mojawapo ya kuiga kwa wakurugenzi wengine wa mamlaka, ili wanapopata fedha za ndani wapeleke kwenye miradi, lakini pia tumeenda kule AUWASA kule Arusha na kwenyewe wanafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda hapa Babati kwa kijana mdogo sana, Msuya, anafanya kazi kubwa sana kule Babati kwa ajili ya upatikanaji wa maji. Lakini Mkurugenzi wa MWAUWASA kule Mwanza anafanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania wanaoishi pale Mwanza. Na sisi pia kwa mapato ya Wizara alitupatia mradi kule Busega kwa ajili ya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe mambo machache. Busega ndio kuna chanzo cha Ziwa Viktoria, lakini kuna vijiji ambavyo viko ndani ya kilometa 42 havina maji. Leo nikuombe, majuzi hapa ulijibu mradi wa maji wa Ziwa Viktoria kwenda Bariadi kutokea Busega, Maswa, Itilima na Meatu utaanza hivi karibuni. Niombe sana mradi huu ndio muarobaini wa matatizo ya maji katika Mkoa wa Simiyu, ndio muarobaini wa matatizo ya maji katika Jimbo la Busega. Nikuombe sana kama tayari umeshatangaza atakapopatikana mkandarasi basi aende kwa speed ili wananchi sasa walio wengi katika Mkoa wa Simiyu, hasa Wilaya ya Busega, waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mheshimiwa Waziri hivi karibuni mlitangaza mradi mkubwa wa maji pale Jimbo la Busega. Mradi wa thamani ya bilioni sita kwenye kata yetu ya Kabita, lakini mkandarasi hakupatikana, alikosa vigezo. Ninajua mnatangaza tena, niombe sasa speed iongezeke ili mkandarasi apatikane aweze kufanya kazi kwa ajili ya kuanza ule mradi. Nimeona kwenye bajeti tayari umetutengea, bajeti iliyopita milioni 950 na bajeti hii milioni 700. Ni imani yangu kwamba, ataanza kazi mapema ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pale Busega tuna kata kama tatu bado zina shida ya maji. Tuna Kata ya Nyaruhande, tuna Kata ya Igalukilo na Kata ya Ngasamo bado zina shida ya maji. Niombe sasa kata hizi tuziangalie kwa macho mawili ili tuweze kuzipatia maji na wananchi wa pale nao waweze kunufaika na Ziwa Viktoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja. (Makofi)