Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuwa mchangiaji katika Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza kabisa nilikuwa naomba nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Rais wetu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya Tanzania hii katika sekta zote zile ikiwemo sekta hii ya maji vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waislam tunaamini pale kwenye Quran kuna aya inasema kwamba wallahu yarzuku myashau bighairi hisab; kwamba Mwenyezi Mungu anamruzuku mwanadamu mambo bila hesabu ya aina yoyote ile. Sifa hizi zipo kwa mdogo wangu Aweso. Aweso ni mnyenyekevu, mtulivu, mwadilifu, mchapakazi, anaheshima, na mabega yake yapo chini kila siku. Ndugu yangu endelea kuwa hivyo hivyo chapa kazi na sisi kaka zako tuko nyuma yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri anamsemo wake huwa anasema, kwamba ukiona Kobe kapanda katika mti basi kapandishwa huyo si bure. Mimi niseme tu Naibu Waziri anafanya kazi kweli kweli. Nikushukuru sana dada yangu kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuweza kumsaidia Mheshimiwa Waziri na kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa kwa ujumla wake. (Makofi)

Mhehimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila; katika Wizara hii ya Maji kuna Katibu Mkuu ndugu yangu Sanga. Huyu bwana ni muadilifu kweli kweli huyu bwana ni muungwana kweli kweli anatoa ushirikiano kwa Wabunge ukimpigia simu anapokea pale ambapo akishindwa kupata simu yako anakutumia message na atakwambia samahani kiongozi nilikuwa kwenye mkutano. Katibu wetu Mkuu fanyakazi na mimi niseme tu katika kipindi hiki cha sasa hivi katika Awamu ya Sita Mheshimiwa Rais Wizara ya Maji inakwenda kufanya mabadiliko makubwa sana kwa kuwa na Katibu Mkuu kama ndugu yangu Sanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee mbele. Mkurugenzi wetu wa RUWASA anafanya kazi nzuri kwelikweli, Mheshimiwa Rais akufanya kosa kuliona jicho lake pale lakini pale kwangu tuna meneja wa RUWASA, kijana yule anafanya kazi safi sana shida yake ni moja tu yule kijana ni Samaki Nchungu anatokea kule Mtwara na wale ni watoto wetu sasa tunashindwa kumpa zawadi pale Kibiti ya kuweza kumpa mke lakini anachapa kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilisimama hapa, wakati nimesimama nilikuwa nimeomba fedha katika miradi mbalimbali ambayo iliyokuwa imesimama katika Jimbo la Kibiti. Mheshimiwa Waziri aliniambia kwamba kaka yangu usiwe na wasiwasi tutajitahidi kadri ya uwezo wetu tutapeleka maendeleo kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Mimi ninafaraja kusema tumepeleka fedha katika Mradi wa Mtunda Shilingi milioni 790 mkandarasi yupo site nani kama Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hivyo haitoshi tumeweza vile vile kupewa fedha pale katika Kata ya Mjawa Shilingi milioni 502 mkandarasi yuko site, mabomba yametambazwa katika Kata ya Mjawa utafikiri vile uyoga nani kama Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niendelee mbele pale Kilula Tambwe kuna mradi mzuri sana wa maji umepelekwa pale shilingi milioni 452 mkandarasi yupo site kazi zinaendelea na Diwani wa Kata ile ndugu yangu Tabwe anaendelea kusimamia mradi ule safi sana Mheshimiwa Rais tunamshukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo kuna mradi wa Shilingi bilioni 1.3 mradi wa pale Nyanjati kwenda kule Kivinja A. Mradi ule kila kitu kimeshakamilika tunasubiri tu kusaini makaratasi yale ya mkandarasi. Mimi nikuombe chondechonde Mheshimiwa Waziri hakikisha kwamba hili linaenda kufanikiwa na mwaka jana nilisema hapa mambo yakiwa mazuri tutakupa zawadi na kwa uadilifu uliokuwa nao jana niliwaona shemeji zangu sijui kama ile ruhusa umepata mke wa tatu yupo pale anakusubiri. Tunaomba sana tuhakikishe kwamba ule mradi unakwenda kusainiwa na unakwenda kufanya kazi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa kuliko yote namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Nilimwambia kwamba katika Jimbo letu la Kibiti kuna maeneo ya Delta kule pamoja na kata za Kihongoloni, Maparoni, Mbuchi, na Msala. Tangu jimbo lile lilivyokuwa limeanzishwa hawajawahi kuona bomba, Mheshimiwa Waziri akaniambia kwamba bwana sikiliza tunakwenda kufanya mpango kutafuta fedha na tunaenda kufanya upembuzi yakinifu katika Bonde la Mto Rufiji. Nataka niseme tu, Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana mzigo umetoka shughuli zinaendelea piga kazi nani kama Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa haya yanayotokea mimi niseme tu sisi watu wa Wilaya ya Kibiti tukiwa tunapigaga kura zile za kuchagua Rais ndiyo huwa tunaongoza Mkoa wa Pwani 2025 panapo uhai sijui Mama huyu atazibeba beba vipi zile kura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba niendelee mbele. Pamoja na kuyasema yote haya mazuri mimi nilikuwa naomba niishauri Serikali katika mambo mawili tu; jambo la kwanza nilikuwa naomba nishauri Serikali; jana nimewasikia Wabunge wenzangu na sisi ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sizungumzii tu Kibiti peke yake tumesikia malalamiko ya watu kutoka Mtwara na watu kutoka Lindi, bajeti tunajua kwamba haitoshi, Mheshimiwa Waziri angalieni huko Serikalini kama itapendeza twende tukawatafute wadau ambao wanaweza waka-finance hii miradi na kuijenga vile vile wadau wapo mnaweza mkayatoa maji katika mradi ule wa Mtwara Ruvuma Walter Project wapo wadau wanaweza wakaifanya shughuli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama vile haitoshi, kwa ndugu yangu Mabula jana aliongea kwa ukubwa sana vile vile wadau wapo, tuwatafute ambao wanaweza wakaifanya miradi hii mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la msingi naomba niungane na Mheshimiwa Ngasa; jana alishauri jambo moja la msingi kwelikweli. Alisema kuwa kwenye hii miradi wakati tunatoa hizi tender tuangalie ukubwa wa zile tender. Najua kuna sheria zetu za manunuzi zinatubana, lakini tuwe flexible. Kama inapendeza kuna vimiradimiradi hivi milioni 500, milioni 700 labda mpaka bilioni moja itolewe katika ngazi ya wilaya kule tunaisimamia karibu sisi na madiwani na. Ile miradi mingine mikubwa mikubwa inaweza kwenda katika ngazi ya mkoa ili mambo mengine yakawa yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na yote haya, naomba tu niseme, Mkoa wetu wa Pwani mmetufanyia mambo makubwa sana ukizingatia kwamba pale sisi tumefungiwa mradi mzuri sana pale Chalinze kwa ndugu yangu Mheshimiwa Ridhiwani. Sisi Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa Viwanda, maji ni uti wa uhai, lakini kama hivyo haitoshi katika shughuli zetu za mambo ya viwanda maji ni kitu cha msingi. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais, tunakushukuru sana Mheshimiwa Aweso piga kazi na sisi tupo atakayekuzingua na mimi nakwambia tu kaka zako tupo, tutakusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la mwisho naomba nizungumze tena ni lamsingi kwelikweli. Mheshimiwa Waziri huyu ana mambo mengi. Sasa, ikikupendeza, tutakapopitisha hii bajeti mimi nilikuwa naomba tu unipe Mheshimiwa Naibu Waziri niende naye Kibiti, twende kule twende tukakague miradi ile, tukazungumze na wananchi kule. Nataka nimuhakikishie tu Mheshimiwa Naibu Waziri akifika kule pweza wataliwa kambare watapatikana changu wapo na mambo mengine yataendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninasema kwamba naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)