Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nishukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nitoe shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wa Mkoa. Vilevile Injinia Joyce Bahati wa RUWASA lakini pia ndugu yangu Palanjo wa IRUWASA kwa kazi kubwa inayofanyika katika Jimbo la Kilolo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliposimama hapa mara ya kwanza kuchangia Wizara hii kuna mambo kadhaa niliomba mwaka jana, na niishukuru sana Wizara hii kwa usikivu. Niliomba usambazaji wa maji katika Mji wa Ilula. Ninashukuru sana Wizara hii imechukua hatua, milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya UVIKO zilipelekwa pale na usambazaji umefanyika. Ninawaomba wale wanahabari waliokuwa wanataja Vitongoji vya kuzunguka Ilula havina maji waende sasa wakapige picha kwa sababu maji yanatoka ili tujue walikuwa na nia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu, wiki iliyopita Mheshimiwa Waziri kwa usikivu wako umeongeza shilingi milioni 500 kwa ajili ya Mji wa Ilula. Ninakushukuru sana, tenda ile itangazwe mapema ili ule usambazaji uendelee katika vitongoji vyote vya Kata ya Ilula na Nyarumbu ili wananchi wale waendelee kunufaika na maji. Haikutosha kupitia IRUWASA shilingi milioni 350 kwa ajili ya Mji Mdogo wa Kilolo ambazo pia juzi kwenye mazungumzo umepitisha. Kwa maana hiyo ndani ya bajeti ya mwaka huu tayari tuna shilingi milioni 850 zinaenda ambazo zimeongezeka katika Bajeti iliyopita. Ninakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikakushukuru kwa ajili ya miradi mingine niliyoomba mwaka jana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri mmeifanyia kazi. Mradi wa Uhambingeto ambao umekuwa ni chechefu kwa muda mrefu. Mradi huu tayari umeshatafutiwa mkandarasi na amepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba kuweka sign ile mikataba mapema ili mradi ule wa Kata ya Uhambingeto uweze kufanyika mapema. Ninashukuru pia kwamba kuna miradi mingine miwili ambayo imechukua muda kidogo kupata wakandarasi lakini tayari imepatiwa fedha. Mradi wa Masege Masalali, Kihesa Mgagao na Mradi wa Ifua – Lisoli ambayo pia tuliiomba mwaka jana na imepata fedha. Mimi ninashukuru sana kwa sababu mmefanyia kazi mapema na ninaona kwamba kuna dalili njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri huwa anasema wali wa kushiba huonekana kwenye sahani na mimi nakubaliana naye. Lakini kuna vijiji na kata ambazo huo wali wa kushiba zinauona ila kama tunavyoenda kwenye hoteli umefunikwa na ile karatasi ya nailoni bado haujafunuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo kata ambazo bado hazijapata maji. Naomba nitaje baadhi ya maeneo. Kata nzima ya Ng’ang’ange haijapata maji tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini pamoja na hayo, tunavyo vijiji baadhi ambavyo kuna mradi wa Mto Mtitu ambao ni Mradi wa Mto Mtitu ni mradi wa mkoa siyo mradi wa wilaya. Mradi wa Mto Mtitu maji yake yanapita katika Majimbo ya Kilolo Kalenga, Iringa Mjini pamoja na Jimbo la Isimani. Na huu mradi tayari pendekezo limeshaletwa liko mezani kwako kwa ajili ya kuomba mkopo kwa Serikari ya Korea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mradi huu ufanyiwe kazi kwa sababu una vijiji vingi sana katika Jimbo la Kilolo pia kikiwepo Kijiji cha Kitoo. Kijiji cha Mtitu chenyewe ambao ndio Mto Mtitu unaitwa nacho bado hakijapata maji na ninaomba mradi huu ufanyiwe design nzuri ili uweze kukidhi pia baadhi ya maeneo ya Kilolo; kwa sababu chanzo ni Kilolo lakini ukiangalia Vijiji vya Kilolo ni vichache vitakavyopata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa Kilolo – Isimani ambao Mheshimiwa Waziri unaufahamu, ulishautembelea. Mimi pamoja na Mheshimiwa Lukuvi wa Isimani tunakuomba mradi ule ukamilike. Umefika asilimia 64 na imebaki kidogo, na una-cover vijiji vingi sana vya Kilolo pamoja na vya Isimani. Ninakusihi sana katika bajeti ya mwaka ujao ukamilishe mradi ule ili wananchi wa Kilolo na wananchi wa Isimani waweze kunufaika na mradi ule kwa sababu ni mradi mkubwa ambao una maslahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitoe ushauri mdogo kuhusu miradi iliyopo katika Jimbo la Kilolo. Jimbo la Kilolo lina vyanzo vingi vya maji kwa hiyo, miradi mingi ni miradi midogomidogo kwa sababu tukitengeneza miradi mikubwa itakuwa gharama kubwa isiyokuwa na umuhimu. Nimeona kuna tendency ya kuiangalia kwa ukubwa miradi mikubwa lakini hii miradi ya Shilingi Milioni 500 tayari umeshasambaza maji vijiji vitatu, Shilingi milioni 600 umeshasambaza maji kata tatu, kidogo inapewa umuhimu mdogo kutokana na udogo wake kwa sababu ni ya gharama ndogo. Mimi napenda hii miradi ipate kipaumbele imalizwe mapema kwa sababu miradi mikubwa inachukua muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili unahusu suala la mita za maji. Mheshimiwa Waziri unafahamu kwamba kwenye umeme tumeshatoka kabisa kwenye post paid watu kuzungukazunguka kwenye nyumba kusoma mita ni unnecessary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani pale Mkoa wa Iringa mmeshajaribu prepaid na inafanya kazi vizuri. Mimi ninaomba twende kwenye prepaid tuachane na watu kuzunguka, mwisho watu watapigwa mawe waambiwe ni panya road kumbe ni wasoma mita. Kwa hiyo, mimi ninaomba sana kwamba twende kwenye prepaid tuachane na haya mambo ya postpaid. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda kushauri ni Jumuiya hizi za Usimamizi wa Maji. Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba miradi hii imekuwa mingi na inakamilishwa kwa haraka, lakini ni kweli kwamba hakuna mfumo bora wa usimamizi wa hii miradi kwenye vijiji na hizi Jumuiya za Usimamizi wa watumiaji maji bado hazijawa imara vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba kuwe na utaratibu mzuri ili miradi hii iweze kuwa bora na endelevu. Na tukumbuke kwamba kwenye vijiji vyetu si kwamba sasa hivi watu wanataka kuchota maji kwenye vituo tuu. Kama sisi tulivyo mijini na wao pia wanataka maji yafike kwenye nyumba zao. Kwa hiyo, hizi Jumuiya zikiimarishwa zitasaidia kuweka taratibu nzuri za kuingiza maji kwenye nyumba zao. Mimi naomba sana hizi Jumuiya ziangaliwe ili tuweze kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana. (Makofi)