Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda na mimi kuchangia; na ninaanza kwa kuunga mkono hoja kwa sababu mimi nimesimama hapa sina nongwa kubwa na Waziri wetu wa Maji, Naibu wake na Katibu Mkuu. Naibu Waziri alikuja jimboni kwangu akapanda kwenye milima juu kabisa kwenye vyanzo vya maji, ametusaidia sana, Mungu awabariki sana mnafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa mara ya kwanza tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutusaidia Mradi wa Miji 28, mradi wa Kiburubutu ambao tangu Mbunge akiwa marehemu Abbas Gulamali ulikuwa haujafanyiwa kazi na haujapatiwa pesa, safari hii umepatiwa pesa kwa hiyo, tunawashukuru sana na tunawapongeza. Naomba tu mtusaidie katika vile visima ambavyo tumechimba sasahivi mpango wa pili ni ma-tank tupate fedha kwa ajili ya ma- tank.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muda wangu huu ambao nimepewa wa kuchangia sauti yangu inaongea kwa unyonge sana kutokana na masikitiko ya wananchi wangu ambao tunawaboreshea maji; wengi ni wakulima wa mpunga na miwa.
Juzi tarehe 5 mwezi wa tano walikaa katika vyama vyao wakaamua kuhusu maslahi yao ya miwa katika mikutano yao mikuu, lakini jana nimepokea simu zaidi ya hamsini wakiwa wanasikitika kuhusu maamuzi yaliyofanywa na Serikali kuingilia maamuzi yao; kwa kweli imenisikitisha sana. Natumia nafasi hii kusema ili Serikali iliyopo hapa isikie isaidie kufuatilia. Kama tunaboresha maji huku tunaendelea kuharibu na kuingilia shughuli za wananchi za uzalishaji itakuwa hatufanyi kitu chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia muda wangu huu ili Mawaziri na viongozi waliokuwepo hapa wasikie. Kwenye biashara, kwenye kilimo cha muwa kuna shida kubwa sana. Naligusia hapa kwa sababu hakuna maana nyingine yoyote kama tunaboresha mambo ya maji kwa wananchi halafu wakulima kule wananyanyaswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna kiongozi wa Serikali ameenda kuzungumza na wananchi, hawajafurahia maamuzi yao Kata ya Sanji. Na kwa bahati nzuri nimeongea na Mheshimiwa RC, Mkuu wa Mkoa Shigela, analifanyia kazi hili. Nimeongea na Waziri Bashe analifuatilia. Jambo hili halijakaa vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu uko hapa naomba kutumia nafasi hii wananchi wangu wasikie kwamba, nimelisema hapa na tunalifuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tume zimeshaundwa kufuatilia jambo hili, lakini halifanyiwi kazi na tume zinafichwa taarifa, yanazushwa maneno ya uwongo kujenga faida ya watu kunufaika na kilimo cha muwa na sukari. Mambo haya ni kama yale yaliyotokea Kasalali, mambo haya ni kama yanayotokea hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimetumia muda huu wa kuchangia Wizara ya Maji kushukuru kwa miradi waliyotuletea, lakini kwa kweli ni masikitiko makubwa sana na kilichotokea jana; kwa mara ya kwanza kupokea mimi simu karibu hamsini za wananchi wakilalamika wanataka kupanda mabasi kuja Dodoma kwa sababu maamuzi yao yamekiukwa. Ni imani yangu ni kwamba, kuwa Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa watachukua hatua madhubuti za kuwasikiliza wananchi wale upya; kwa sababu Sheria za Ushirika wamefuata na taratibu wamefuata, lakini zemeenda zimetenguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishia hapa. Nashukuru sana. (Makofi)