Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia kwenye Wizara ya Maji.
Awali ya yote naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Wizara ya Maji kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na Wizara kwa ujumla kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya. Sambamba na hilo nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwatua wanawake ndoo kichwani. Ama kweli hakuna mwanamke anayeweza kutupa mtoto wake, na mama ametambua tatizo la maji ni tatizo la wanawake. Tuna mpongeza sana.
Mheshimiwa Spika, nilisimama kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwaajili ya kuomba maji na Mheshimiwa Waziri akanihakikishia na akaniambia; ukiona mama mtu mzima analia ujue kuna jambo; nitahakikisha hili jambo linamalizika au kupungua kwa kiasi kikubwa; na ndiyo maana leo nimesimama kwa ajili ya shukran. Mheshimiwa Waziri amenipatia pesa takriban bilioni 12.5 kwa ajili ya mradi mkubwa kutoka chanzo cha Ng’apa kuja Mitwero hatimaye kusambaza mabomba katika Jimbo letu la Mchinga, ahsante sana Mheshimiwa Waziri kwa fedha hizo ambazo umenipatia. Sasa ninaamini lile tatizo la maji limeanza kupungua na baada ya muda si mrefu tatizo la maji litatoweka katika Jimbo letu la Mchinga ambalo liko katika Manispaa ya Lindi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kuna Tarafa ya Mipingo tayari maji sasa hivi yanatiririka. Mheshimiwa Waziri wanakusubiri tu uje uzindue kama ambavyo ulivyoahidi wakati ule tulipokuwa pale Mnyangara ahsante sana Mheshimiwa Waziri. Haukuishia hapo tatizo la maji la Mchinga lilikuwa ni tatizo tete na ni tatizo kubwa; maji kulikuwa hakuna walikuwa hawajui maji ya bomba sasa hivi maji yanatiririka bombani.
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo ukanipatia visima vinne na tayari hivyo visima vinne vimeshakuwa katika harakati za kumalizika kuna kisima cha Kilolambwani tayari kimemalizika, Uleka kule kisima kimemalizika na maji yanabubujika hayana hata utaratibu jinsi yanavyobubujika ahsante sana. Sasa tuko kwenye kisima kile cha tatu Namkongo ambako Namkongo kulikuwa na shida kubwa ya maji; wakitoka Namkongo wanamalizia Nanjime. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kunipatia maji katika Jimbo langu la Mchinga.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna bilioni 1.5, na hii umetupelekea Mnyangara na tayari kazi inafanyika; umetupelekea Mputwa tayari kazi inafanyika; vile vile umetupelekea Kiwawa kazi zinafanyika, na ndiyo maana nimesema nasimama hapa kwa ajili ya kutoa shukrani zangu za dhati kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika. Mwaka 2022/2023 bado kuna miradi mipya ambayo mmetupatia.
Mheshimiwa Spika, kuna mradi mpya wa upanuzi kutoka Kilangala kwenda Mihambwe Sinde hatimaye kufika kule Mtumbikile. Mradi huu una jumla ya shilingi milioni 340. Sambamba na hiyo kuna mradi ambao utakuwa ni Phase II kutoka Moka kwenda Matimba; na maeneo haya yote yalikuwa na matatizo makubwa ya maji huku umetupatia milioni 250 jumla ya milioni 590. Hukutuacha hapo hivyo hivyo bado ukatupatia visima vitano ambavyo vitachimbwa katika Jimbo letu la Mchinga. Nasema ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kila kwenye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Sambamba na mafanikio hayo makubwa ambayo tumeyapata kwa muda mfupi katika Jimbo letu la Mchinga bado tuna changamoto katika tarafa ya Milola kuhusiana na suala la ukarabati na mabomba ambayo ni chakavu katika ile kata ya Milola. Maji yapo lakini yanayomwagika ni mengi sana. Tunachoomba Mheshimiwa Waziri utusaidie kiasi cha fedha ili tuweze kufanya ukarabati wa mabomba yale ambayo yanavujisha maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye bomba kuu pale Nyirola.
Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine ambao nashauri huu mradi ambao ni wa bilioni 12.5 pesa ambazo tayari zimetoka ni bilioni 1.8 na ni mradi wa mwaka mmoja. Ombi langu kwa Serikali ombi langu kwako Mheshimiwa Waziri mtufanyie kadri inavyowezekana kadri bajeti inavyoruhusu ili kutupatia zile pesa kwa wakati ili ifikapo tarehe 3 Mei, 2023 kama tulivyokubaliana mradi huu uwe umekamilika. Tulikubaliana kwenda kusaini ule mkataba na ulikuwa tayari. Mheshimiwa Waziri vile vile nitakuomba twende tukazindue ule mradi wakati huo huo kazi iendelee.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. ninaipongeza sana kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia na kwa kuwatua ndoo wanawake wa Jimbo la Mchinga. Mwenyezi Mungu akubariki Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete kabla hujakaa tusaidie Jimbo la Mchinga liko Mkoa gani hapa nchini? Washa kisemeo chako.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mchinga lipo Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Lindi ndiyo mkoa ambao Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatokea huko katika Jimbo la Ruangwa. (Makofi)