Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lushoto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya na kuhakikisha anawatua kina mama ndoo kichwani.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji pamoja na timu yake yote kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwa hakika Mwenyezi Mungu atawalipa.
Mheshimiwa Spika, kama inavyofahamika ya kuwa maji hayana mbadala, naishukuru Serikali imenipa miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili, lakini kama unavyojua changamoto ya maji bado ni kubwa sana katika jimbo la Lushoto na naomba niorodheshe maeneo yenye changamoto; Kata ya Gare, Kata ya Kwai, Kata ya Migambo, Kata ya Malibwi, Kata ya Ubiri, Kata ya Ngulwi, Kata ya Kwekanga na Kata ya Makanya.
Mheshimiwa Spika, kata hizi zote nilizoorodhesha hapo juu hazina mradi hata mmoja na zina hali mbaya sana kwa wananchi kukosa maji safi na salama. Kwa hiyo niiombe Serikali katika bajeti hii iangalie kwa jicho la huruma ili tuweze kuokoa maisha ya wananchi wanaoishi katika kata hizo hasa kina mama, wao ndiyo waathirika wakubwa wa huduma hii maji.
Mheshimiwa Spika, pamoja na baadhi ya kata ambazo zina miradi ya maji lakini bado kuna uhitaji mkubwa wa maji, kwani wananchi ni wengi kuliko upatikanaji wa maji yenyewe, kata hizo ni hizi zifuatazo; Kata ya Lushoto, Kata ya Mlola, Kata ya Kilole, Kata ya Kwemashai, Kata ya Mbwei na.Kata ya Magamba.
Mheshimiwa Spika, Kata hizi zina miradi kama nilivyosema, lakini bado mahitaji ni makubwa sana, kwa hiyo niiombe Serikali iongeze miradi katika kata hizi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, pia naomba niishauri Serikali yangu tukufu, Jimbo la Lushoto lina vyanzo vingi vya maji, lakini katika vyanzo hivyo kuna chanzo ambacho kina sifa zote yaani hakikauki hata wakati wa kiangazi, lakini pia ni chanzo chenye maji mengi, safi na salama na chanzo hicho kipo kileleni, hivyo basi kinaweza kupeleka maji kwenye kata 13 kati ya kata 15 za Jimbo la Lushoto, na chanzo hicho kikifanyiwa kazi na kwa kuwa kipo juu, maji yake hayatahitaji pump, ila maji yake yatakuwa ya mserereko mpaka yafike kwa watumiaji.
Mheshimiwa Spika, chanzo hicho kipo katika Kata ya Magamba eneo la chanzo linaitwa, Mstari Namba Tisa na mradi huu ukitekelezeka utakuwa ndiyo suluhisho la kudumu katika Jimbo la Lushoto. Kwa hiyo niiombe Serikali itumie chanzo hiki ili kuondoa kero ya maji katika Jimbo la Lushoto na ile dhana nzima ya Rais wetu pamoja na Waziri ya kumtua mama ndoo kichwani itakuwa imetekelezeka kwa vitendo pamoja na kumaliza tatizo la maji safi na salama na yenye kutosheleza kwa wananchi wa Lushoto.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Wizara hii ya Maji kwa asilimia mia moja.