Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya Makadirio na Mapato ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Pili, naungana na wezangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kutayarisha na hatimae kuiwasilisha hotuba hii katika Bunge lako tukufu kwa ufasaha na umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, nianze na hali ya upatikanaji wa maji vijijini; napenda kuipongeza Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mikakati ya kumtua mama ndoo kichwani. Hili ni jambo zuri sana na la kupigiwa mfano katika nchi yetu.

Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeonesha kuwa upatikanaji wa maji vijijini unaongezeka kila mwaka. Mwaka 2021 hali ya maji vijijini ulikuwa asilimia 74.5, mwaka huu imepanda kwa asilimia mbili. Naipongeza Serikali yetu kwa rekodi hii ya manufaa kwa wananchi.

Ushauri wangu katika upatikanaji wa maji vijijini ni kuendelea kuwasogezea vyanzo vya maji karibu na maeneo yao ili kuwapunguzia masafa marefu ya kufuatilia maji kwa matumizi yao.

Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu udhibiti wa uchafuzi wa vyanzo vya maji; vyanzo vyetu vya maji vinahitaji kuhifadhiwa sana. Vyanzo vingi vya maji viko katika hali ya kuweza kuhatarisha maisha ya wananchi. Utakuta chanzo cha maji hakina uzio wa kukihifadhi, wanyama wanaweza kuingia kwenye chanzo cha maji na kuhatarisha maisha. Aidha, kutokana hali ya dunia sasa hivi watu ambao si wazuri wasiopenda maendeleo inakuwa ni rahisi kuweza kufanya uharibifu wa chanzo cha maji.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu katika jambo hili kwa Serikali ni kuendelea kuchukua hadhari ya kuviwekea uzio vyanzo vote vya maji nchini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu vibali vya kuchimba maji; naipongeza Wizara ya Maji kwa kuweka utaratibu huu wa kuruhusu wananchi kuchimba visima vyao kwa matumizi yao binafsi. Hili ni jambo zuri sana litaisaidia Wizara kwa sehemu kubwa.

Ushauri wangu katika jambo hili ni kuweka udhibiti kwa kuwapa maelekezo ya kitaalam namna ya kuchimba visima hivyo ili kuepuka hatari ya miripuko ya maradhi yanayotokana na maji yasiokuwa salama.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.