Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niaze kwa kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa zawadi kubwa ambayo ameitoa kwa wanasanaa wote kwa kitendo chake cha kutambua sekta hii na pia Wizara hakika tunampogenza kwa hili. Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuitambua sekta ya sanaa na kuipa Wizara Mheshimiwa Rais ameweza kupatia katika uteuzi wake kwa kumteua Mheshimiwa Nape Moses Nnauye kuwa Waziri katika Wizara hii, kwani tuna imani kubwa na Mheshimiwa Nape pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Anastazia Wambura. Tunaamini ataifikisha mbali sekta hii, suala la msingi ni kwamba Wizara hii ipewe support hasa kwenye suala la bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo tayari wameshaanza kuifanya. Pia naomba nimpongeze Waziri kwa kuzindua Tamasha la Filamu la Kimataifa la Tanzanite tarehe 23 Aprili, pale Mount Meru Hotel, Arusha. Tamasha hili lina tija sana kwa Serikali na wadau wa sanaa, kutangaza kazi zao, kimataifa. Pia litatoa ajira kubwa kwa Watanzania, litaongeza idadi kubwa ya watalii kuja Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba Mashirikisho ya Sanaa yaimarishwe ili yaweze kusaidia Wizara namna ya kuisaidia sekta hii. Mashirikisho hayo ni:-
(a) Filamu; waigizaji, waandishi wa miswada, uigizaji, wazalishaji na wasambazaji.
(b) Muziki; Muziki wa Dansi – CHAMUDATA, Muziki wa Injili - CHAMVITA, bongo flava, taarabu na rumba.
(c) Sanaa za Ufundi; tingatiga, uchoraji, ususi na ufinyanzi.
(d) Maonesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Wizara yako inayo orodha ya vyama vyote ambavyo ni wanachama katika mashirikisho yote kupitia BASATA. Hakika Mheshimiwa Waziri utakapotumia mashirikisho haya kuyawekea mkazo na utaratibu mzuri ni wazi utakuwa umeleta mafanikio makubwa sana. Kuna vyama ambavyo vimeshapiga hatua kubwa sana mfano, Chama cha Muziki wa Injili, kina matawi hadi mikoani japo si yote lakini chama kwa kupitia viongozi wake wamehamasisha na watu wengi (wasanii wa nyimbo/muziki wa injili) wamejiunga rasmi na kuna vitambulisho maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni wameweza kujiunga na bima ya afya na wanachama wengi wameweza kupatiwa kadi za bima ya afya na hivyo kunaondoa adha kubwa ya wasanii wanapougua kuanza kuomba misaada wa kuchangiwa kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu. Ninaamini utaratibu huu utaendelezwa kwa vyama vingine vilivyo wanachama wa mashirikisho husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usambazaji wa kazi za sanaa bado ni tatizo kubwa, Waziri tunaomba uingilie kati jambo hili na hasa kwenye mikataba, kwani ndipo penye uonevu na wizi mkubwa wa haki ya msanii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya adhabu ya mtu anayekamatwa na uharamia wa kazi za sanaa bado inamlinda mhalifu kwa kupewa adhabu ndogo, nayo iangaliwe upya ili kukomesha wizi wa kazi za wasanii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, COSOTA itoe maelezo ya malipo ya mirahaba kwani ni muda mrefu sasa hawalipwi. Je, ni chombo gani sasa kitapewa kazi ya kusimamia takwimu na ukusanyaji wa fedha hizi na kujiridhisa kuwa ni kiasi gani zimekusanywa na zimeenda kwa nani na je, ndicho anachostahili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, CD na DVD (mazagazaga) zinazouzwa mitaani kwa bei ya shilingi 1000, kwanza Serikali inapoteza mapato kwa sababu hazina stamp za TRA hazijalipiwa kodi. Pia zinawaumiza wasanii wetu wa ndani ambao wamepitia mlolongo mrefu sana hadi kupata stamp za TRA. Pia naomba stamp hizi ziwekwe utaratibu wa kupatikana mikoa yote. Naomba niishie hapa na naunga mkono hoja.