Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Afya, Wizara hii tunaitegemea sana lakini inalinda uhai wa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nitaanza kuwapongeza sana Wizara kwa kazi kubwa na kasi nzuri inayoendelea hivi sasa kwa upatikanaji wa madawa. Jambo hili linakwenda vizuri lakini yote haya baada ya mabadiliko yaliyojitokeza hivi karibuni naamini Mheshimiwa Waziri kwa uzoefu wake atatusaidia sana Waheshimiwa Wabunge na kuhakikisha huduma za kinamama zinaendelea kupatikana katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningeomba jambo moja, Wizara hii ambayo anaisimamia Mheshimiwa Ummy. Sisi kwenye Wilaya yetu ya Itima tumejenga hospitali ya wilaya lakini tumejenga kituo cha afya. Lakini vilevile kuna bajeti iliyopitishwa mwaka jana kwa ajili ya kuleta vifaa tiba, mpaka hivi sasa ninavyoongea na mkandarasi ni MSD, mpaka hivi sasa kati ya vifaa 51 vimekuja item saba tu. Sasa utaona ni namna gani Serikali inavyozidi kuwekeza katika maeneo haya muhimu lakini bado tunakuwa na changamoto hiyo kubwa ambayo na Serikali tayari inaendelea kuleta fedha nyingi katika maeneo hayo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kupongeza tu, Serikali imeendelea kuongeza majengo katika hospitali yetu ya wilaya lakini na katika vituo vyetu vya afya. Changamoto kubwa ni pale ambapo watumishi hawapo wa kutosha. Wilaya yangu ya Itilima ina takribani wakazi 500,000. Watumishi Idara ya Afya ni 171 tu, sasa tuna vituo vya afya vinne na tuna zahanati 31 na tuna hospitali ya wilaya. Utaona ni adha ipi kubwa ambayo watumishi hawa wachache ambao tunawapata na tunawapa kazi ngumu ya kushindwa kuwahudumia wananchi hawa na matokeo yake mtumishi huyu wa afya anafanya kazi mpaka inazidi uwezo wake na wakati mwingine inafika mahala anajibu tofauti kwa sababu tayari akili yake imeshazidiwa jinsi ya huduma aliyotoa kwa siku hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara husika kuna vijana ambao wamechukuliwa kwenye baadhi ya halmashauri kuendelea kujitolea. Katika nafasi hizi ambazo zimetolewa basi iwe kipaumbele kuhakikisha kwa sababu wapate hiyo ajira angalau itatutia moyo na vijana wengine ambao wapo mitaani wataendelea kushawishika kuendelea kutoa huduma na kusaidia kwenye maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine tuna Kituo chetu cha Afya Zagayu ni cha muda mrefu sana hakina wodi ya wazazi, wodi ya watoto na maabara na kimechakaa sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri basi katika mipango yake akiangalie kile na kubwa zaidi ombi langu kubwa ni kuhakikisha tunaletewa watumishi wa kutosha katika Wilaya yetu ya Itilima na Kituo cha Afya cha Mwanunda ambacho ni kipya kimeshakamilika tunatarajia Juni Mungu akipenda kinaweza kukamilika kikaanza kutoa huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa watumishi tulionao hao wachache haitawezekana. Pongezi nyingi tunaendelea kukupa Mheshimiwa Ummy tunachoamini kwamba na pongezi hizi tunakuamini ni mchapakazi na nimsikilizaji mzuri kwa Wabunge na kwa wananchi na kwa wataalam wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tungeendelea kukuomba pale ambapo kuna umuhimu basi tia nguvu ili shughuli zinazofanywa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan ziendelee kutimilika kwa vitendo. Tukifanya hivi wananchi wetu na malalamiko haya ambayo tunayazungumza tutakuwa tumeyapunguza kwa asilimia kubwa sana. Changamoto ya afya ni kubwa, kubwa sana lakini tunahitaji sasa kuendelea angalau ku-balance uwiano wa watumishi wetu katika maeneo husika ili kazi hii ifanyike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na la mwisho, ombi langu kubwa kwa Mheshimiwa Waziri ninaomba sana watumishi utupatie wa kutosha nakumbuka kwenye program ya Mkapa Foundation ulikuja kutupatia watumishi pale Itilima na ukaahidi kituo cha afya pale Makao Makuu. Naomba Mheshimiwa Waziri kiwe kipaumbele chako kwa sababu ni maneno uliyazungumza wewe na bahati nzuri Mwenyezi Mungu amekurudisha kwenye Wizara hiyohiyo, sasa naomba sana utekelezaji huo ufanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)