Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kunipa uhai mpaka kufika leo. Pia napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuwafanyia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwenye Sekta ya Afya, sisi Kasulu tumeendelea kulamba asali kama alivyosema Mzee Makamba juzi. Tumepokea chini ya Mheshimiwa Rais Samia zaidi ya Shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kasulu DC. Pia tumepokea Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya Kitanga, tumepokea Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya cha Kurugongo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumepata pia Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba ambazo ziko MSD. Hapo nataka nigusie kidogo; Mheshimiwa Ummy yuko hapa; kwanza napongeza maamuzi ya Mheshimiwa Rais kufanya overhaul kwenye MSD na kupata Mkurugenzi mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mkurugenzi mpya na ninaamini kwamba ataenda kufanya marekebisho pale ambapo kulikuwa na changamoto ili kuhakikisha kwamba vifaatiba hivi na dawa vinafika kwa wakati. Nimtie moyo tu kwamba yeye sasa hivi ndio Mkurugenzi wa MSD, kwa hiyo, asiogopeogope. Pale ambapo kuna changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa mabadiliko kisheria, amwambie Waziri atuletee sisi hapa ndio Wabunge tunaotunga sheria, turekebishe kuhakikisha kwamba hatuna changamoto za kisheria ambazo tunaweza kuzipitia.
Mheshimiwa Spika, Kasulu vijijini tunayo changamoto ya watumishi. Mheshimiwa Waziri sisi tuna watumishi 192 peke yake. Tunazo Zahanati 32 Vituo vya Afya sita na Hospitali ya Wilaya moja, lakini wote hao wanahudumiwa na watumishi 192, ambayo ni sawasawa na asilimia 22 tu ya mahitaji yote. Chonde chonde, naomba sana Kasulu Vijijini katika jambo hili tupewe jicho la kipekee sana, kwa sababu watumishi wanafanya kazi sana, wanachoka. Tuna sekta kama upande wa mionzi, tuna mtumishi mmoja tu ambaye anahudumia halmashauri nzima. Kwa hiyo, naomba sana jambo hilo litazamwe.
Mheshimiwa Spika, suala la wizi wa dawa, kwanza linafanya bima yetu ya afya kubeba mzigo mkubwa sana, kulipa dawa ambazo watu hawajatumia. Pili, inachafua mno Serikali yetu. Majengo mazuri, lakini hayana dawa. Mwananchi haendi pale kwa ajili ya kutazama majengo, anaenda kwa ajili ya kutafuta huduma. Sasa nina ushauri kidogo, huwezi kuzuia wizi wa dawa kwa kufanya tu ziara za kushtukiza hospitali. Utafanya ngapi?
Mheshimiwa Spika, huwezi kuzuia wizi wa madawa kwa kusema kwamba ile sheria ambayo tuliipigia kelele kidogo kwamba maduka ya dawa yajengwe mbali na zahanati au na Kituo cha Afya, Hapana. Kwa sababu yakijengwa hapo hapo au mbali, wizi kama upo, upo tu. Hoja yangu ni kwamba, katika dunia ya leo ambayo teknolojia imekuwa kubwa sana, Mheshimiwa Waziri unayo fursa ya kuja hapa kutuomba hela tukupe fedha za kutosha uweke mifumo thabiti ya IT ili kuweza kuondoa wizi wa dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda huko kwa wenzetu, suala la wizi wa dawa limeshaondoka, siyo kwa sababu ya vitisho wala kauli mbalimbali, Hapana. Ni kwa sababu wameweka njia ambazo ni za kisasa za mifumo ya kiteknolojia kwa ajili ya kulinda dawa. Wewe Mheshimiwa Waziri kipindi ukiwa ofisi kwako huwezi kujua kuwa Kasulu Vijijini kuna kiasi dawa kiasi gani? Siyo mpaka upige simu, uki-click tu unaona track. Njoo uombe hela hapa Bungeni, tukupitishie uende ukafanye. Najua ni investment kubwa, lakini ukafanye kwa ajili ya maslahi mapana ya Watanzania, otherwise naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)