Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na mimi. La kwanza niweze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameweza kunisimamisha mahali hapa ili nami niweze kuongea kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Temeke. Nimshukuru sana Rais wangu Mama Samia Suluhu kwa kazi nzuri anayoifanyia nchi yetu ya Tanzania na hata sasa sisi wanawake tunajiona fahari kwa sababu tunaye kiongozi mwanamke ambaye hakika anaupiga mwingi.

Mheshimiwa Spika, nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Ummy pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa nzuri mnayoifanya, na tunaamini sana kwamba kwa sasa kazi hii itakwenda kufanyika vizuri na Watanzania tunawaamini sana. Lakini si ninyi tu, ni pamoja na timu yenu nzima ya Wizara ya Afya kwa kazi kubwa ambayo mnakwenda kuwafanyia Watanzania. Mimi pamoja na yote najua na ninaamini kabisa kwamba madaktari wapo, wauguzi wapo katika hospitali zetu; lakini nasema ni wachache. Kwa kuwa mmepata nafasi ambayo Rais amewaongezea muweze kuajiri basi tuombe muajiri kwa haraka sana ili hawa watumishi waweze kuwepo katika hospitali zetu nyingi na zahanati ambazo zimeongezwa na Rais wetu mama Samia Suluhu.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nijikite sana katika Jimbo langu la Temeke. Kwanza hospitali yetu ile ya Temeke imechukuliwa na imefanywa ni ya Rufaa ya Kimkoa. Lakini Serikali hamkutuacha hivyo Jimbo la Temeke mkatujengea hospitali nzuri sana ambayo iko Yombo Vituka, na ni hospitali ya kisasa na ni ya ghorofa. Kwa kweli tunawashukuru sana wana Temeke. Lakini pamoja na uzuri wa hospitali ile viko vifaa baadhi vimeshaingia, kwenye wodi zile viko vitanda na kadhalika ambavyo vimeingia.

Mheshimiwa Spika, lakini tuna tatizo moja kubwa sana. Ni kwamba, ile hospitali ya mwanzo chumba cha operesheni kiko chini, na ni kidogo, kina kitanda kimoja tu. Ikitikea kama wagonjwa wako wamezidiwa operesheni inafanyika kwa mtu mmoja tu. Kwa hiyo niombe sana juu kule tulikojengewa lile jengo la ghorofa kuna chumba kikubwa sana cha operesheni lakini vifaa havijafika na fedha mnazo MSD. Tumetoa karibu mwaka mmoja na nusu sasa lakini hatuwezi kufanyiwa operesheni kule kwenye chumba cha juu. Na kikubwa zaidi kinachoharibu ni kwamba, hospitali ile mmeiwekea lift lakini yule mkandarasi ambaye aliweka ile lift ameifungia; takriban mwaka mmoja na nusu sasa hatuwezi kuitumia kwa sababu anasema anatudai Serikali.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, niwaombe sana, mdogo wangu Ummy mwende, sasa mkaangalie jinsi gani Serikali inaweza kulipa lile deni la mkandarasi ili sasa hata MSD waweze kuweka vile vifaa kwenye chumba kile cha operesheni kule juu ili watu wetu waweze kufanyiwa operesheni wakiwa juu; kama bado mtakuwa mnahitilafiana kwenye kulipana deni la ile lift.

Mheshimiwa Spika, sisi Watanzania, hasa wana Temeke, naamini tunaipenda Serikali yetu, hivyo hatutaki kusema maneno mabaya kwa ajili ya Serikali. Tunajua ni kati ya ninyi pamoja na mkandarasi. Serikali tayari ninaamini wanatamani kuona sisi tunakwenda kwa lift ile.

Mheshimiwa Spika, na wahudumu ni wachache; pale wanapokuwa kwamba amefanyiwa operesheni chini inabidi wamsukume kwa stretcher kupandisha juu. Hali ni ngumu sana, na wauguzi wale ni wachache sana, kama nilivyosema. Kwa hiyo niombe sana ndugu zangu, lift ile ikafanye kazi. Lakin, pamoja na lift ile, vifaa vile kule juu viwekwe ili kile chumba kisikae bure.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wana Temeke tunajivunia pale kwa sababu tukizidiwa sana inabidi waende Temeke, na Temeke ni ya Rufaa sasa hivi, kupokelewa ni shida. Kwa hiyo naomba sana ndugu zangu, ninakuomba sana hawa wawe wasikivu, na ninaamini Serikali yetu ni Sikivu, kwamba watafanyia kazi hili jambo kwa sababu tayari mlete fedha zingine. Kilakala mnatujengea hospitali nyingine; lakini hii kama haijaisha kule Kilakala kweli itakwisha na kuletewa vifaa?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana, najua Mama Samia ni msikivu sana; tunapokwenda kuomba, kama kuna hitilafu ya fedha kidogo tukiomba naamini tunapewa fedha hizi. Ninamshukuru sana kwa sababu hata ile hospitali juzi tumeweza kuiangalia na mwenge ni hospitali nzuri ambayo tunakwenda kuikamilisha kipindi si kirefu, ile ya Kilakala.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu, lift hii ya pale Yombo Vituka wananchi wanafanyiwa operesheni, yaani ni kama foleni ambayo hata mimi wakati mwingine madaktari wanaponiita naona huruma. kwa kweli najisikia vibaya sana. Niombe sana lift hii ifanyiwe kazi, MSD msikie kilio chetu, kwamba vile vifaa vya chumba kile, hizo taa, sijui za kufanyia operesheni, vitanda hakuna ilhali fedha mnazo. Niombe sana Serikali sikivu iweze kutusikia sisi wana Temeke na kituo kile kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)