Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii tena katika Wizara ya Afya kuchangia mambo mbalimbali. Kwanza naomba nikupongeze sana dada Ummy, Mheshimiwa Ummy anafanya kazi kubwa sana ndio maana leo hii Mheshimiwa Rais amemrudisha hapo, ameona kazi ambayo ameifanya. Leo hii anawasikia Wabunge wengi wakiomba vifaa tiba kwa sababu tayari kuna majengo, kwa hiyo Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri wamefanya kazi kubwa sana kuleta fedha za UVIKO kujenga vituo vya afya vingi na ndio maana leo hii tunaomba vifaa tiba kwa sababu tunayo tayari majengo ambayo yanaenda kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo sana wa fadhila leo hii kama sitomshukuru Mheshimiwa Rais, kwa sababu Mheshimiwa Rais ni msikivu mno, mwaka jana nilisimama hapa ndani nilizungumza sana kuhusu masuala ya mafuta kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Leo hii nasimama hapa kwa kujidai kwamba Mheshimiwa Rais amesikia kile kilio chetu. Aliwaita watu wenye ulemavu Ikulu na akaelekeza Wizara ya Mheshimiwa Ndalichako kwa ajili ya kutenga bajeti ya watu wenye ulemavu, ya kununua mafuta Sh.60,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini hii bajeti ya Sh.60,000,000 kwa mwaka 2022/2023, itaongezeka kutokana na idadi tutakayopata kutokana na sensa. Tukishafanya sensa tutajua idadi kamili ya watu wenye ulemavu wa ngozi ili tuweze kupata mafuta yanayotosheleza kabisa, lakini kwa kianzio tumeanza vizuri, Sh.60,000,000 imetengwa na utaratibu mzuri sana utafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kufanya mabadiliko ya MSD. MSD leo hii tumepata kiongozi mwingine mpya na leo hii kila mtu anasifia MSD, lakini naomba niwaambie MSD jambo moja, wasijisahau na hizi sifa. Hawa hawa watu leo hii wanaowasifia kesho watawasema humu ndani mtawashangaa. Kwa hiyo, kwa makosa ya huko nyuma waangalie kitu gani wenzao walikosea na wao wajitengeneze kwa namna gani ili waweze kuboresha. Tunawaamini sana MSD na sisi, wao ni kimbilio letu kwa sababu sisi tunawawakilisha wananchi, kwa hiyo wao ni kimbilio letu sisi. Kwa hiyo, tunawaomba sana sana katika jambo hili waangalie sana maslahi ya wananchi zaidi.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii pia nina maombi kadhaa kwa Wizara hii ya Afya; leo namwomba Mheshimiwa Ummy, kuna jambo hili la mashine kwa ajili ya kuzuia kansa. Wanasema kinga ni bora kuliko tiba. Nawaambia kweli humu ndani Wabunge hawajawahi kuona mgonjwa wa kansa mtu mwenye ulemavu wa ngozi au mtu mwenye ualbino na kama wakitoka hapa wakaenda ocean road wakaona wagonjwa wa kansa watanielewa kwa nini kila siku nikisimama hapa nazungumzia suala la kansa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, basi naomba hizi mashine zilizopo ziongezwe zipo kwenye mikoa saba, basi tuone namna gani ya kuongeza hizi mashine ili kila mkoa wapate hizi mashine, wasiweze kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kuzuia saratani ya ngozi. Pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Ummy amefanya kazi nzuri sana. Leo hii nimefurahi mno, nimefurahi sana sana kwa kuona kwamba kitengo cha mionzi kinahamia Dodoma. Kwa hiyo sasa Dar es Salaam pale ocean road kipo kitengo cha mionzi, lakini pia Mwanza pale kipo na sasa hivi Dodoma kipo, ina maana itawasaidia watu wanaotoka Singida, Manyara, Arusha hawatoenda mbali sasa hivi watakuja hapa Dodoma kwa ajili ya kupata mionzi kwa ajili ya saratani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe pia jambo lingine Mheshimiwa Ummy, namwomba sana kitengo cha afya, huduma za afya kwa watu wenye ulemavu namwomba sana, leo hii tunazungumza kuhusu suala la afya ya akili, sisi walemavu mimi mwenyewe nawezakana sina afya ya akili, kwa sababu tukiudhiwa tunakasirika haraka sana, tuna mambo mengi sana ambayo yametuzonga, hiki kitengo kitatusaidia sana kwa huduma zake kwa ajili ya kushauri. Kwa hiyo naomba huduma ya utengemao ili iweze kutusaidia sisi tuweze kufanya majukumu yetu vizuri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)