Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia azimio hili la kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mtakubaliana nami katika kipindi hiki cha miaka miwili Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha wazi dhamira yake ya kusimamia misingi ya haki za binadamu, utawala bora, demokrasia, pamoja na diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la haki za binadamu, nampongeza sana Mhehimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mikutano ya hadhara, kufungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungwa, kukubali kufanya maboresho ya sheria za huduma za vyombo vya habari na tayari rasimu iko wazi, kusema hadharani kuhusu kutoridhishwa na upatikanaji wa Haki Jinai na kuunda Tume ya Haki Jinai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika katika eneo la utawala bora, nampongeza sana Mhehimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake aliyowasilisha wiki iliyopita kwenye Mkutano wa Summit for Democracy, ameiambia dunia kwamba Tanzania itarudi kujiunga katika OGP (Open Government Partnership). Hii ni hatua muhimu sana kwa sababu msingi wa OGP ni kuimarisha Serikali ambazo zinafanya kazi kwa uwazi, uwajibikaji na kuwainua wananchi kuweza kuwajibisha Serikali. Kwa kitendo hiki itaongeza imani kwa wawekezaji wakubwa ambao wanapenda kuwekeza kwenye nchi ambazo zina mifumo thabiti ya utawala bora na sera ambazo zinatabirika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la demokrasia, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuimarisha demokrasia hapa nchini kwetu. Alianza hivyo kwa kuunda kikosi kazi ambacho kimemshauri katika maeneo ya demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa na mengi ambayo amependekeza, tayari ameshaanza kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikirejea tena katika hotuba yake ya wiki iliyopita katika Mkutano wa Summit for Democracy, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kwamba Sheria ya Vyama vya Siasa inakwenda kuboreshwa, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inakwenda kuboreshwa na mchakato wa Katiba Mpya unakwenda kuanzishwa. Nami naamini kupitia yote haya, moja ya azma yake kubwa ya kuimarisha ushiriki na ushirikishwaji wa wanawake katika siasa na wenyewe utakwenda kuimarishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha katika eneo la dipolmasia ya kiuchumi, wote mtakubaliana nami kwamba katika miaka hii miwili Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi yetu. Katika kipindi cha miaka miwili, kupitia ziara alizofanya nje ya nchi, tumeweza kupata miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 793 ambayo imesajiliwa TIC. Hilo ni jambo kubwa sana la kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo, hivi karibuni tumepata ugeni wa Makamu wa Rais wa Marekani Mheshimiwa Kamala Harris, na kupitia ugeni wake Tanzania imeweza kupata msaada wa kifedha wa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 560 ambayo ni sawasawa na takribani shilingi trilioni 1.3.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, inaonesha ni namna gani ambavyo kuna umuhimu mkubwa wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aendele kufanya ziara nje ya nchi kwa sababu ziara hizi zinapata tija na sisi ambao tunapata nafasi mbalimbali za kushiriki mikutano ya nje ya nchi, tunajisikia fahari sana pale ambapo tunajitambulisha tunatoka Tanzania. Nasi tunafuata nyayo zake za kuhakikisha kwamba fursa yoyote ambayo tunaipata tunaisemea vizuri nchi yetu na tunatafuta fursa mbalimbali za nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja na naomba niungane na Wabunge wenzangu wote na Watanzania wote kumuunga mkono na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mageuzi makubwa anayoyafanya katika eneo la haki za binadamu, eneo la utawala bora, eneo la demokrasia na eneo la diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)