Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi niungane na Bunge lako Tukufu kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kusimamia na kutekeleza majukumu yake kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimepata nguvu ya kusimama kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa mambo kadhaa. Jambo la kwanza ni namna ambavyo alipokea Taifa hili kwenye mazingira magumu mpaka hapa alipotufikisha, halikuwa jambo rahisi. Lakini pia kuiaminisha jamii kwamba kiongozi sio mwanaume peke yake na mwanamke anaweza kufanya na akafanya vizuri. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mazingira hayo ameonesha kama kiongozi lakini ameonesha njia. Kwa sisi ambao tuko hapa kwenye chombo hiki kwa niaba ya Watanzania, kwamba matamanio yake ili ayafikie lazima Bunge tutimize wajibu wetu wa kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Spika, natambua mengi yamezungumzwa na Wabunge wenzangu kuhusu kukuza demokrasia; lakini napata mazingira magumu sana, kwamba ni kweli amekuza demokrasia lakini amekuza demokrasia iliyodondoshwa na nani? Wa chama gani? Hayo maswali lazima tujue kwamba na jamii inayotusikiliza inapata maswali hayo hayo. Tunapozungumzia mikutano ya hadhara; yalizungumzwa hapa tena na kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu kwamba lazima tutenge muda wa kufanya kazi na muda wa mikutano na tulipiga makofi Wabunge ndani ya Bunge hili. Leo tunapongeza kurudisha mikutano ya hadhara ni kweli. Tunampongeza amerudisha lakini nani aliiondoa? wa chama gani? Sisi Bunge tunasimama wapi?

Mheshimiwa Spika, nipongeze…

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa kuna taarifa, iko wapi? Mheshimiwa Cosato Chumi.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimpe taarifa msemaji anayezungumza hivi sasa. Wakati Mheshimiwa Boutros Boutros Ghali alipogombea nafasi ya UN aliomba kwamba yeye atagombea kwa kipindi kimoja, ilipokuja mara ya pili akasema anabadilisha atagombea tena mara ya pili. Akaulizwa kwa nini? Akasema ni mjinga tu asiyebadilisha mawazo yake na kuendana na hali na nyakati. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani taarifa hiyo unaipokea?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nimwambie Mheshimiwa Chumi kaka yangu nimepokea taarifa sasa sijajua nani ni wajinga ambao wameamua kubadilisha utaratibu waliokuwanao na kuja na utaratibu mwingine.

Mheshimiwa Spika, maridhiano yanayoendelea ni maridhiano ambayo yana afya kwa Taifa. Ili ufikie uchumi tunaoufikiria ni lazima uruhusu mawazo mbadala. Mawazo mbadala utayapima kama yana maslahi kwa Taifa utayatumia kwa sababu Taifa ni la kwetu sisi sote.

Mheshimiwa Spika, naunga sana mkono azimio hili kama sisi tutaendelea kumsaidia. Ukimtazama mazungumzo yake anatamani kulitoa Taifa lilipo na kulipeleka mahala fulani; lakini tukikaa kwenye unafiki hatutamsaidia Mheshimiwa Rais. Tukisimama imara kumpongeza, leo tukitazama uchumi wa watu pamoja na vitu, Bunge tukisimama imara tutamsaidia Mheshimiwa Rais na tutampongeza kwa sifa anazostahili kusifia. Tutampongeza Mheshimiwa kwa kuimarisha uchumi kwa kusimamia vyema kama Bunge kuondoa mianya yote ya Rushwa na matumizi mabovu ya fedha.

Mheshimiwa Spika, yote haya ambayo ameyaanzisha Rais wetu jambo jema la kupongezwa lazima liwekwe kwenye msingi bora wa Sheria Mama ambayo ni Katiba mpya. Katiba iliyopo si kwamba yote ni mbovu lazima maboresha yafanyike. Maboresho ya kwanza ni kuanzia kwenye Sheria yenyewe ya Uchaguzi, namna tunavyopatikana na namna ambavyo tunaweza kupata viongozi wengine kutokana na wananchi wenyewe walivyoamua.

Mheshimiwa Spika, ili tufikie malengo ya hayo maridhiano ambayo leo Mheshimiwa Rais ameongoza majadiliano hayo ni lazima, tunapozungumzia Sheria hii ambayo ni Katiba mpya, ameonyesha kwamba Chama Cha Mapinduzi mko tayari; ni lazima mchakato huo uanze mara moja ili kusimamia yale anayoyazungumza. Atapokuja Rais mwingine afuate misingi ya Sheria yetu ambayo ni Katiba mpya ya nchi yetu. Tusipofanya hivyo, leo Rais tunampongeza hapa akija Rais mwingine atakuja na nini?

Atakubali hiyo mikutano ya hadhara? Au ataiondoa tena wakati iko kwa mjibu wa Sheria kwenye Katiba yetu ya nchi? Ni lazima misingi inayowekwa leo kwenye utawala bora ije isimamiwe na yeyote atakayepata nafasi hiyo.

Mheshimiwa Spika, si kwamba tunapozungumza kama vyama vya Serikali mbadala tunazungumza mabaya tu. Tumeanza kuonesha njia kabla ya leo, tarehe 8 Machi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Baraza la Wanawake (BAWACHA) walimkabidhi tuzo ya kuimarisha demokrasia. Kwa hiyo, sio jambo baya, ni jambo jema, mnapoona jambo linafanyika lazima tupongeze, lakini tupongeze tukiamini haya mambo yamejengwa kwenye msingi imara. Katiba mpya ni sasa Katiba mpya ni lazima. Ahsante.