Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 61(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023, naomba kuwasilisha hoja kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kuruhusu na kunipa fursa hii adhimu ya kuwasilisha hoja hii ya azimio hili. Naomba pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi bora na thabiti aliyouonesha kwa taifa letu tangu alipoingia madarakani. Nawaomba Watanzania wenzangu tuzidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema ili aweze kutekeleza majukumu haya ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sote tulishuhudia katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hali ya demokrasia na utawala bora imeendelea kuimarika nchini.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyochangia kuimarika kwa demokrasia ni pamoja na haya yafuatayo: -
(1) Uamuzi wa kuruhusu shughuli za siasa hasa mikutano ya hadhara kufanyika nchini kote; uamuzi huu umefufua na kuimarisha shughuli za siasa nchini, kwani vyama vya siasa vimepata fursa ya kunadi sera zao na kutoa mawazo mbadala ambayo yatasaidia Serikali kutekeleza huduma za kijamiii na kiuchumi hususan masuala yanayogusa maendeleo ya wananchi;
(2) Kuanzisha vikao vya maridhiano ya kisiasa miongoni mwa vyama vya siasa nchini ili kuhakikisha kunakuwepo mahusiano mema miongoni mwa makundi ya kisiasa yaliyokuwa yanahasimiana;
(3) Kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya kimfumo na kisheria yanayoongoza shughuli za kisiasa na kudumisha misingi ya amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania; na
(4) Kuridhia kuundwa kwa kikosi kazi cha kufanyia kazi masuala yananyohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini ambapo lengo kubwa la kikosi kazi hicho ilikuwa ni kupendekeza namna bora ya kutekeleza haki ya vyama vya siasa ikiwemo kuwepo na uwanja sawa wa kufanya shughuli za kisiasa bila kukiuka sheria na maadili ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa diplomasia ya uchumi ambapo Mheshimiwa Rais mwenyewe amekuwa chachu ya mafanikio hayo kwa kuwa mwanadiplomasia mahiri. Katika kipindi hicho, tumeshuhudia nchi yetu ikipitia mafanikio haya yafuatayo: -
(1) Kuongezeka kwa masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika masoko ya nje;
(2) Kuimarika kwa mahusiano ya kimkakati na makampuni ya kimataifa yanayolenga kuwekeza katika sekta za uzalishaji ili kuchochea uchumi wa nchi yetu;
(3) Kuwezesha upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka kwenye taasisi za fedha duniani ambapo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, miundombinu, afya na maji.
(4) Kukua kwa shughuli za uwekezaji na kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji wapya nchini kutoka nje ya nchi, baada ya kufanyika maboresho ya mazingira ya kufanya biashara nchini;
(5) Kupitia filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour amefanikiwa kutangaza vivutio vilivyoko nchini na hivyo kukuza sekta ya utalii ambapo tumeshuhudia watalii maelfu kwa maelfu wakiingia nchini na hivyo kuongeza pato la Taifa; na
(6) Kuimarika kwa mahusiano na mataifa mengine na taasisi za kimataifa kutokana na ziara mbalimbali ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya nje ya nchi ambazo zimezaa matunda makubwa. Mathalan, hivi karibuni nchi yetu imepokea ugeni mkubwa wa Mheshimiwa Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani. Kupitia ziara hiyo, Serikali ya Marekani imeahidi kuimarisha ushirikiano na Tanzania kwenye sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, viwanda, usalama wa mitandao, TEHAMA, afya usafirishaji na usalama wa chakula.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niwasilishe Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuimamrisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi kama ifuatavyo: -
Kwa kuwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha wazi nia yake ya kuifanya Tanzania kuwa moja, salama na bila kundi lolote kuwa nyuma katika kufurahia demokrasia ya kweli;
Na kwa kuwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kuimarisha diplomasia ya uchumi ambayo imelenga kuiletea Taifa letu maendeleo;
Kwa hiyo basi, Bunge hili katika Mkutano wake wa Kumi na Moja, Kikao cha Kwanza, tarehe 4 Aprili, 2023, linaazimia kwa dhati na kauli moja haya yafuatayo:-
(a) Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini; (Makofi)
(b) Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukuza demokrasia ya uchumi; na (Makofi)
(c) Kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika majukumu yake ya kazi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kumwombea afya njema, baraka na ulinzi wa Mwenyezi Mungu katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naafiki.