Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nami naomba kuchukua nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha siku ya leo kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu. Pili, naomba nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba, Taifa letu linakwenda mbele. Tatu, naomba nimshukuru sana Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri sana ambayo jana amelielezea Taifa letu, hotuba ambayo ime-cover mambo mengi.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa ufupi, naomba nizungumzie mambo mawili makuu ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyazungumza katika hotuba yake. Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia suala la maji. Sisi sote tunajua changamoto zilizopo sasa hivi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, lakini namshukuru sana Waziri Mkuu, naishukuru sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa jitihada ilizofanya kukabiliana na tatizo hili la maji, hasa katika Jimbo langu la Nanyumbu. Ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu wakati mama yetu Samia Suluhu Hassan anachukua nchi tulikuwa na changamoto kubwa sana ya maji. Ndoo ya maji ilifikia shilingi 2,500 ndani ya miaka hii miwili amefanya mapinduzi makubwa na sichelewi kuyaeleza ndani ya Bunge lako nini kimefanyika ndani ya jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, wakati mama anaingia madarakani kata zifuatazo zilikuwa hazina maji kabisa na wala walikuwa hawajui nini maana ya maji ya bomba, lakini leo ninavyozungumza tuna maji ya bomba na wananchi wananufaika na huduma hiyo. Kata ya Nandete walikuwa hawajui kabisa huduma ya maji, Kata ya Mikangaula walikuwa hawajuikabisa huduma ya maji, Kata ya Nangomba, Kata ya Mikangaula Nangomba walikuwa hawajui kabisa, Kata ya Kamundi walikuwa hawajui kabisa, lakini ndani ya miaka miwili yamefanyika mapinduzi makubwa, leo wananchi wanajua nini maana ya mabomba na nini maana ya maji safi na salama. Jambo hili namshukuru sana Waziri Mkuu kwa kuisimamia Serikali vizuri na hatimaye wananchi wananufaika na huduma hizi.

Mheshimiwa Spika, ndani ya hotuba yake Waziri Mkuu amezungumzia upatikanaji wa maji katika ile miji 28. Wilaya yangu ya Nanyumbu ni moja ya wanufaika wakuu wa ile miji 28.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka kwamba, mwaka jana tulitia saini ule mkataba. Ule mkataba tulitia saini pale Ikulu kwamba, wakandarasi wale waje katika majimbo yetu na watekeleze mradi huu, lakini mradi huu umechelewa sana, ndani ya mwaka mmoja mradi haujaanza.

Mheshimiwa Spika, nimefurahi, jana mara baada ya Waziri Mkuu kuzungumza nikakutana na Waziri wa Maji na amenihakikishia kwamba, sasa kila kitu kimekamilika na huu mradi unakwenda kuanza. Naomba niwahakikishie wananchi wangu wa Jimbo la Nanyumbu, mradi huu unakuja kuanza na vijiji takribani 20 vitanufaika na mradi huu, hili ni jambo la kupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa maji pamoja na kwamba, unapita katika vijiji mbalimbali hadi kufika katika Mji wa Mangaka hapa ndipo kwenye walengwa wakubwa katika mji huu. Wananchi wa Mangaka wanashindwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi kwa sababu ya ukosefu wa maji. Leo utashangaa guest house zetu zote za Mangaka tunachukua maji ya kopo, hatuna maji ya bomba. Kwa hiyo, tuna imani kabisa kwamba, mradi huu utawezesha wananchi ambao wanaenda kuwekeza mbali na Wilaya yetu watarudi na kujenga nyumba nzuri, hoteli na hatimaye wale watu watalii wanaotoka Msumbiji kuja katika Mkoa wetu wa Mtwara watakuwa na mahali pazuri pa kufanya shughuli zao za starehe.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niipongeze Serikali katika miradi, kuna miradi mikubwa ya mabwawa ndani ya jimbo langu. Kuna ukarabati mkubwa wa bwawa ndani ya Kata ya Sengenya ambao Serikali imetoa bilioni tatu na milioni mia nne, mradi huu unaanza hivi karibuni na takribani vijiji 10 vitanufaika na mradi huu; Mradi wa Upanuzi wa Bwawa la Sengenya.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Maratani Serikali imejenga bwawa kubwa lenye thamani ya shilingi bilioni moja na milioni mia tano, lakini imeleta bilioni tatu na milioni mia sita kwa ajili ya kuweka mtandao wa mabomba, vijiji vinne vitanufaika na mradi huu, Kijiji cha Lipupu, Maratani, Mchanganee na Malema. Mambo yote haya ya maendeleo yamefanywa ndani ya kipindi kifupi chini ya utawala wa mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, mradi wa uchimbaji wa visima. Ndani ya miaka miwili visima visivyopungua 25 vimechimbwa ndani ya jimbo langu na mikakati inaendelea katika kuhakikisha kwamba, sasa visima hivi vinawekwa mitandao ya maji, ili wananchi wanufaike.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoka hapo naomba niende kwenye mtandao wa barabara. Naipongeza sana Serikali, wakati mama yetu anaingia madarakani Jimbo langu la Nanyumbu lilikuwa linapata shilingi milioni 550 kwenye TARURA, leo ninavyozungumza tunapata bilioni mbili na milioni mia nne, ni jambo la kupongeza sana, lakini sio kupata fedha tu, fedha zile tunazisimamia. Mimi kama Mbunge wa Jimbo lile nahakikisha matumizi sahihi ya fedha, value for money, ionekane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya miaka miwili tumeweza kujenga barabara kilometa 4.5 za lami, jambo ambalo ndani ya Wilaya ya Nanyumbu kitu lami kilikuwa hakipo ndani ya mji wetu. Leo ndani ya jimbo langu tumeweza kuweka taa za barabarani, jambo ambalo wananchi walikuwa hawajui kama kuna taa za barabarani. Hii yote imefanyika chini ya miaka miwili ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni jambo la kupongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, tumeweza kujenga madaraja yasiyopungua 15, makalavati na vivuko mbalimbali, hii yote ni kwa sababu fedha zimekuja lakini tunazisimamia. Nami naomba niwape rai ndugu zangu Wabunge, fedha hizi zinapokuja tuwe wasimamizi wakuu wa hizi fedha. Tunatambua kwamba kuna TARURA, kuna Engineer TARURA lakini bado Mbunge una sababu ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha hizi.

Mheshimiwa Spika, jambo la Tatu naomba niipongeze tena Serikali kwenye kilimo. Wilaya yangu ilikumbwa sana na baa la njaa. Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan tuliomba msaada wa chakula cha bei nafuu na Serikali imetupatia takribani tani 1000. Wananchi wamepata mahindi ambayo yameuzwa kwa bei nafuu. Kuna baadhi ya watendaji ambao hawakuwa waaminifu walitumia fursa hii kujinufaisha.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mkuu wetu wa Wilaya Mama Chaurembo na Kamati yake yote ya Ulinzi na Usalama kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kupambana na hawa watumishi ambao siyo waaminifu na hivi ninapozungumza wengi wamepelekwa Mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Kwa hiyo, mimi naipongeza sana Serikali ila rai yangu kwa Serikali, tunatambua tuna njaa, tunahitaji wananchi wawezeshwe pembejeo kwa wakati, mbolea kwa wakati ili waweze kuepukana na baa hili la njaa.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kinachofanyika, mbolea iko mbali na wananchi, haiwezekani Wilaya ya Nanyumbu mtu afuate mbolea kilometa 54 toka alipo, hili jambo litakwamisha sana maendeleo ya wakulima wetu. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iliangalie hili chini ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba tena kuchukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa yale yote ambayo inaendelea kuyafanya ya kuhakikisha kwamba wananchi wa nchi hii wanaishi katika maisha bora na salama.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Ahsante sana. (Makofi)