Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayoifanya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amefanya mambo mengi. Kila mkoa, kila Mbunge aliyepo humu ndani, kila mwananchi anaona mambo yote aliyoyafanya kwenye mkoa wake, kwenye kata yake kwa maendeleo yetu Watanzania. Kweli tunampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, pili, naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yako nzuri ambayo umeitoa, ni nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nawe pia nakupongeza kwa jinsi unavyoendesha Bunge letu hili. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wangu wa Morogoro umefaidi mambo mengi sana kwenye maendeleo anayoyaleta Mheshimiwa Dkt. Samia, Rais wetu. Nianze na ujenzi wa Reli ya Mwendokasi. Kama ulivyosema kwenye Speech yako, kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ambayo ina kilomita 300 na inagharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania bilioni 792.99 ambazo zinajenga reli hii na kuendelea mpaka Dodoma, yaani inakwenda vizuri, imebakia asilimia kidogo kumalizika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba sana na Watanzania wengi wanaisubiri sana hii reli ambayo Mheshimiwa Rais anaisimamia iweze kukamilika na kuleta manufaa ya kiuchumi, mawasiliano, na mengine mengi ya kuinua pato kwa wananchi na nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa upande wa wananchi, hii reli tuisimamie na kuitunza na siyo kuiharibu kama tunavyoharibu miradi mingine wakati mwingine.

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao tunajivunia sana ni wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere. Bahati iliyoje tuliyonayo kwa Mkoa wa Morogoro? Hili bwawa liko kwenye Mkoa wa Mororogoro Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini pamoja na Mkoa wa Pwani. Hii itafua umeme kwa megawati 2015 na inagharimu hela za Kitanzania shilingi bilioni 869.93. Kweli tulijivunia, tulikwena, nami nilikuwepo wakati inawekwa maji na Mheshimiwa Rais alishuhudia maji yanawekwa. Kwa kweli Mheshimiwa Rais tunajivunia sana kwa Bwawa letu la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, hili Bwawa la Mwalimu Nyerere licha ya kuwa na lengo la kufua umeme ambao utatosheleza nchi yetu, ambapo tutaweza kuuza nchi za nje, pia ni kivutio tosha cha utalii kwa watu wa Tanzania, hasa na watu wengine.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naweza kusema kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere, limeleta ajira kwa vijana wetu na hasa vijana wa Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani ambao wanajivunia kuwa na bwawa na Watanzania wote kwa ujumla. Bwawa hili la Mwalimu Nyerere limeweza kukuza Kata na Miji ambayo imeizunguka. Mfano, mzuri ni Kata ya Mvuha pamoja na Kisaki ambayo ukienda unaona kweli maendeleo yanakuja.

Mheshimiwa Spika, sasa tufanye nini? Ushauri wangu; ili kuendeleza na kulifikia hili Bwawa la Mwalimu Nyerere, ili paweze kufikika kwa urahisi, miundombinu mpaka sasa hivi siyo mizuri. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri, barabara ya kuanzia Ubena - Mvuha mpaka Kisaki na barabara ya kuanzia Bigwa - Mvuha - Kisaki mpaka kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere ziweze kujengwa kwa kiwango cha Lami ili kusudi liweze kufikika kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naomba kuongelea ni kuhusu Mradi wa Sukari pale Mkulazi. Bahati nzuri hii Mkulazi na yenyewe iko kwenye Mkoa wa Morogoro. Kuna Mkulazi Na.1 na Mkulazi Na. 2 ambako kuna kiwanda kinachojengwa pale Dakawa Mkulazi kwa shilingi bilioni 39.84.

Mheshimiwa Spika, ninachoomba ni kuwa, miwa inalimwa ambapo mpaka sasa hivi imeshalimwa na kiwanda kimejengwa na kimefikia asilimia 75. Mara kitakapokamilika, kitazalisha tani 50,000 za sukari; ambapo zitakapozalishwa hizo tani 50,000 zitasaidia kupunguza uhaba wa sukari katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni hekta 2,974 mpaka sasa hivi zimelimwa. Ushauri wangu, wakulima wamejitokeza wengi kutoka Kijiji cha Mbigili, Kata ya Mbigili Wilaya ya Kilosa ambao na wenyewe wamewekeza kwa wingi, kwa hiyo wamepata ajira. Tatizo lililopo, hawapati maji ya kutosha. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri Serikali waweze kuwapa maji, kwa maana ya kilimo cha umwagiliaji kusudi tuweze kuzalisha sukari kwa wingi na wakulima waweze kufaidi katika kazi hii ya kilimo kwenye Mkulazi Na. 1 na Mkulazi Na. 2. Zikifanya vizuri itaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ni ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege. Naipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais kwa kukarabarti viwanja vya ndege vilivyopo kama Geita na Dodoma kama nilivyovitaja na viwanja vingine.

Mheshimiwa Spika, swali langu moja kwa Serikali, ilikuwa ni kiwanja cha Ndege cha Morogoro; kwa niaba ya wananchi wa Morogoro, habari ya hiki kiwanja tulishaiongelea humu Bungeni. Kwa hiyo, naomba kujua hatima yake na bajeti ya fedha ya kiwanja hiki kitajengwa lini, ili kusudi wananchi wa Morogoro pia waendelee kufaidi matunda ya Serikali. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni Benki ya Kilimo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais anaitolea fedha ambazo mpaka sasa hivi imeshapata takribani Shilingi bilioni
78.54 ambayo imenufaisha wakulima takribani 119,797.

Mheshimiwa Spika, tunavyofahamu ni kuwa, takribani wananchi wa Tannzania asilimia 65.5 wanategemea kilimo. Kwa hiyo, wakulima hawa wamehamasika sana kwenye kilimo, uvuvi pamoja na mifugo. Kwa hiyo, ushauri wangu, kwenye Benki hii ya Kilimo ambayo ni mkombozi kwa mkulima iweze kuongezewa fedha kusudi wanufaika waweze kuwa wengi kwenye benki hii ya kilimo ambayo inapata fedha hizo lakini hazitoshelezi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningeomba kuongelea ni kuhusu masuala ya Lishe. Bila kuwa na lishe nzuri hatuwezi kuwa na Taifa lenye afya na lenye kuendeleza mambo kiutaalamu. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri kuwa masuala haya ya lishe tuyachukulie kiundani na twende nayo vizuri. Kwa sababu sasa hivi tunaona kuwa kuna ukondefu ambao umepungua ndiyo kwa jitihada zilizotolewa, lakini tufuate ushauri wa lishe, tuweze kutumia chakula cha lishe.

Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine, nilikuwa naomba elimu iweze kutolewa kwenye kliniki...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, namalizia kwa kusema kuwa ukatili wa watoto naomba kwa kweli kama ilivyoongelewa humu ndani utiliwe maanani.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nakushukuru sana, na ubaraikiwe na Mwenyezi Mungu. (Makofi)