Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja hii muhimu iliyoko mezani na nianze kwa kuunga mkono hoja ya Waziri Mkuu kwenye Bajeti ya Waziri Mkuu.
Kwanza nimshukuru pia kwa uwasilishaji mpana ambao umegusa sekta mbalimbali lakini pia namshukuru sana Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kutuletea miradi mingi sana siwezi kueleza mmoja mmoja. Nilikuwa namwambia mtu mmoja wakati fulani nilikuwa nampongeza rais, akasema unampongeza Rais kwa nini mbona anafanya kazi yake? Nikasema wewe hujui kinachoendelea acha sisi tumpongeze kwa sababu tunajua aliyotufanyia kwenye majimbo. Kwa hiyo aendelee kupokea hizi pongezi, sisi tunampongeza kwa sababu tunamtia shime ili aendelee kupata moyo wa kuendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kikubwa ni hiyo fairness yake ya kuhakikisha kwamba kila jimbo linapata mgao sawia. Zamani haikuwa hivyo unakuta mtu mwenye nguvu ndiyo anapata share kubwa zaidi, kwa hiyo ndiyo maana tunampongeza.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwanza nianze pia kuishukuru Wizara ya Kilimo kwa kutuletea mahindi hata Jimbo langu lilikuwa limeathirika lakini baadhi ya maeneo tumeshapokea hayo mahindi, rai yangu ni kwamba Watendaji wetu wa Serikali waendelee kuwa waaminifu kwa sababu inaonekana sehemu nyingine watu wanaandikisha majina ya watu ambao hawana uhitaji, wakati wao ndiyo wanaochukua hayo mazao kwenda kujinufaisha, kwa hiyo niombe vyombo vinavyohusika Wakuu wa Wilaya na Maafisa Tarafa kwenye maeneo yote siyo tu Jimbo langu na sehemu zingine zote hili jambo walifatilie kwa karibu.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba watanzania wenye njaa wanapata chakula siyo watu kwenda kujitajirisha, hii tuwaonye pia hao wanaofanya hivyo kwa sababu watafungwa, Serikali haipo hapa kwa ajili ya kuchezacheza.
Mheshimiwa Spika, kwenye kilimo ningependa kuchangia zaidi, sasa hivi hali ya hewa inaendelea kubadilika sana kwa sababu ya haya mabadiliko ya tabianchi, hapa Tanzania tumezoea sana kulima haya mazao hasa mahindi kama ndiyo zao letu kuu, sasa tuone wenzetu wa kilimo waanze kufanya utafiti hasa kwenye zao la muhogo kama ndiyo kiwe chakula ambacho kinatoa zaidi, tunapozungumzia nafaka.
Mheshimiwa Spika, miaka ya nyuma huko hata kule kwetu Iringa tulikuwa tunalima sana mtama, lakini miaka ya hivi karibuni huu mtama umepotea. Kwa hiyo, wenzetu wa kilimo sasa watusaidie kwanza kutoa elimu pia kufanya utafiti zaidi kama tunaweza tukapata mtama ambao ni mwepesi zaidi wa miezi miwili pia utawanyike katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa sababu tunakokwenda hali itakuwa mbaya zaidi.
Mheshimiwa Spika, hapo hapo kwenye kilimo kwenye vyuo vyetu vya VETA kuwe kuna mitaala mahsusi ambayo inaelezea namna gani tunawafundisha vijana kulima kwa sababu ukiangalia kadri tunavyoendelea ardhi inazidi kupungua, kwa hiyo, uhitaji wa kulima kwa tija unakuwa mkubwa zaidi, mtu atumie eneo dogo lakini azalishe kwa tija zaidi. Sasa hii itawezekana tu kama tutajikita katika kutoa masomo yanayohusu kilimo lakini na zile shule zetu za kilimo za zamani ziweze kurudi ili tuanze kuwaandaa vijana kutoka huko, hiyo itasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la mbolea ya ruzuku pia tunaishukuru sana Serikali kwa kutoa mbolea za ruzuku lakini tuwaombe wenzetu wa Wizara ya Kilimo waanze maandalizi mapema. Mwaka huu sehemu nyingi za Tanzania hata katika Jimbo langu la Kalenga wananchi wamechelewa sana kupata mbolea, pamoja na kuwa mvua zimekuwa pungufu lakini pia mbolea zenyewe zilichelewa sana. Kwa hiyo tunawaomba wenzetu wa kilimo maandalizi yaanze mapema ili mbolea zipatikane mapema, pale ambapo mvua zipo basi Watanzania waweze kunufaika na hii ruzuku ambayo Mheshimiwa Rais amewapa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kuzungumzia eneo lingine la kukuza uchumi hasa upande wa bandari, kwamba bandari tunajua ni lango kuu la uchumi, naipongeza Serikali katika mipango yake ya kutaka kuanza kujenga Bandari ya Bagamoyo. Tanzania inaweza ikawa hub ya uchumi unaotokana na bandari katika eneo la Maziwa Makuu pamoja na Afrika Mashariki kwa ujumla wake pengine hata na SADC, kwa hiyo jambo hili liende haraka.
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali kwamba tulishaanza na tulishasikia kwamba kulikuwa kuna mpango wa kutengeneza mfumo wa kusomana kati ya TRA pamoja na shughuli zinazofanywa bandarini. Miaka miwili iliyopita tuliambiwa kwamba wanaanza majaribio, miaka miwili imepita hakuna kinachoendelea. Hii inaonesha kwamba nia ya bandari na nia ya TRA sioni kama iko vizuri! Kama wote wangekuwa na nia moja hii ingekuwa imeshakwisha na tunaweza kama Serikali tukapata fedha nyingi sana mambo yetu yanapopita kwenye mfumo. Kwa hiyo ninawaomba wenzetu TRA, Bandari mharakishe hili jambo la mifumo kusomana ili nchi iweze kunufaika na kazi kubwa. Muoneshe nia vinginevyo mnatutia mashaka kwamba hizi fedha zinazovuja wenzetu mnanufaika nazo. Kwa hiyo, hilo naomba muweze kuliangalia kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kuzungumza ni kwamba tunavyoelekea bajeti yetu hii mpya, kweli shule zetu za zamani zimechakaa sana, ninaiomba Serikali kwamba katika bajeti zake sasa tuanze kuziangalia shule zetu kongwe, hasa za shule za msingi nilishazungumza tena nalirudia tena, shule hizi ambazo zimejengwa miaka ya 1970, 1980 zimeshaanza kuchoka. Tunavyoweka nguvu katika kujenga shule mpya basi tuhakikishe kwamba ukarabati wa shule za zamani pia tunaendelea kuziboresha. Hilo nalo ni jambo jema Serikali ione namna gani tunafanya.
Mheshimiwa Spika, pia umaliziaji wa yale maboma katika maeneo ya mashule, katika maeneo ya hospitali kwa maana ya zahanati na vituo vya afya, ambapo tayari wananchi walishaanza. Vipo vituo vya afya ambapo vilijengwa siku nyingi unakuta vina wodi moja ya akina mama lakini hata sasa hivi wakina baba wanaumwa sana. Kwa hiyo, tungependa pia Serikali ione umuhimu katika vile vituo vya afya vya zamani kwangu Kalenga na nchi nzima kuanza kujenga pia wodi za wanaume kwa sababu uhitaji upo na tunavyokwenda huko tunakuta wananchi wanatuuliza.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ninapenda kuzungumza ni suala la upimaji wa viwanja. Kwa mfano, Serikali inajitahidi sana kutoa huduma kwa wananchi lakini kwa sababu ya ujenzi holela, mimi niko katika kijiji fulani, nimekaa hapa leo ninaamua naona kuna shamba kilometa 10 nakwenda nafyeka najenga kesho namleta Binamu, kesho namleta na Mjomba baadaye unashangaa eneo lile lina watu watano, lina watu kumi, tayari tunaanza kuisumbua Serikali, hamtuletei maji, hamtuletei shule. Sasa inaonekana kwamba Serikali haifanyi kazi lakini kwa sababu tumeshindwa kudhibiti ni namna gani tunaweka matumizi bora ya ardhi hasa katika eneo la makazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo Serikali iwekee mkazo mkubwa ili tusiwe na hizi changamoto tunakwenda kukagua miradi ya maji unaambiwa bwana mahali fulani sisi hatujaletewa maji, kwa nini kuna kitongoji fulani tumeanzisha. Kwa hiyo Serikali kwenye hiyo mipango miji iende pengine kwa haraka zaidi itaweza kuisaidia nchi ili mipango ikae vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la umeme. Serikali imefanya vizuri tunaishukuru, katika Jimbo langu la Kalenga nilibakiwa na vijiji vitatu sasa hivi wanavimalizia tunashukuru Serikali. Vipo vitongoji vingi sana ambavyo ni vikubwa katika bajeti hii Serikali sasa ione namna gani tutakwenda kupeleka kwa kasi umeme katika vitongoji ambavyo tayari maombi hayo kwenye TANESCO na REA. REA sasa kwa kuwa wanakwenda kumaliza vijiji, nguvu zaidi waelekeze kwenye vitongoji ili nako tuweze kukamilisha mambo hayo.
Mheshimiwa Spika, naona muda wangu umeisha ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)