Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru lakini niendelee kukupongeza kwa nafasi hiyo ya pekee na unaonesha ujasiri mkubwa sana kwamba hatukukosea kukuchagua, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kibali cha pekee kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya mchango mkubwa sana wa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazowafanyia wananchi wa Ushetu. Nina mwaka mmoja nikiwa Mbunge Bungeni lakini fedha zilizokuja Ushetu kwa mwaka mmoja ni zaidi ya Bilioni 17 zimeletwa na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya tu peke yake tumepokea zaidi ya bilioni 4.9, kwenye Kilimo ndio usiseme bilioni 21 ikiwemo na suala la ruzuku ya pembejeo, lakini kwenye elimu ni zaidi ya bilioni 5.8, ukienda kwenye maji na juzi tumepewa fedha nyingine za BOOST zaidi ya bilioni mbili, lazima tumshukuru Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana. Pia lazima tumshukuru Mheshimiwa Rais hata wakati anaingia madarakani, mfano tu kwenye Benki ya Kilimo (TADB) ilikuwa na mtaji usiopungua bilioni 60 na ndio ilikuwa inawakopesha wakulima, lakini mwaka 2021 Mheshimiwa Rais alipeleka fedha zaidi ya bilioni 208 kwenye Benki ya Kilimo. Benki ya Kilimo hiyo hiyo mwaka 2022 iliweza kupeleka fedha kwa wakulima, kwenye viwanda zaidi ya shilingi bilioni 268, ina maana ni zaidi ya asilimia 102, ni kazi ya Mheshimiwa Rais, ni kazi ya Rais wetu kafanya kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuomba tu, tunaongelea sana wakulima na ni asilimia 60 ya Watanzania wako vijijini wanalima. Niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Wizara ya Kilimo, lakini tuendelee kuipelekea fedha TADB Benki yetu ya Kilimo kwa sababu inahitaji mtaji mkubwa. Wakulima wengi wako vijijini hawana mitaji hawana mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikukumbushe tu kwenye azimio letu la mwaka jana Novemba, 2022, tuliazimia benki hii iwe inapewa bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya kuongeza mtaji wake na kwenye Azimio namba saba, naomba kwa ridhaa yako niweze kusoma kipengele kidogo; “Kwa kuwa pamoja na jitihada za Serikali kuipa kiasi kikubwa cha bilioni
208 mwaka 2021, kuna ahadi ya Serikali ambayo kama ingewezeshwa benki hii ingekuwa na mtaji wa jumla ya bilioni 706.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukuomba benki hii ipelekewe fedha ili iendelee kuwakopesha wakulima wadogo wadogo, iendelee kukopesha vyama vya ushirika na ndio iliyotoa mfano mkubwa sana kupeleka fedha kwenye vyama vya ushirika. Vyama vingi vya Ushirika mwaka huu vimenunua pamba na vimeleta ushindani sana kwenye nchi yetu. Kwa nini sasa bilioni 100 hii isiendelee kupelekwa kila mwaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukuomba Mheshimiwa Mwenyekiti na Bunge lako Tukufu benki hii ipelekewe fedha. Nishukuru sana hata kwenye taarifa ya CAG tumeona na ndio benki iliyofanya vizuri zaidi hata kwenye taarifa za ukaguzi. Kwa hiyo niendelee kuipongeza Menejimenti ya TADB pamoja na Mkurugenzi wake wamefanya kazi kubwa sana, kikubwa tuendelee kuisimamia ili iendelee kuwasaidia sana wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme; Kahama ni mji mkubwa sana na unaokua kwa kasi sana, lakini una changamoto kubwa sana ya umeme pamoja na halmashauri zake, hakuna umeme wa uhakika, unakatikakatika kwa muda wote na ndio mji unaokusanya fedha nyingi pamoja na halmashauri zake Ushetu pamoja na Msalala, lakini ukiambiwa mpaka leo hali ya umeme ni mbaya mno. Hata upande wa REA nikiongelea kwenye Jimbo la Ushetu, kata zangu 10 hazina umeme kabisa wa uhakika, umeme ni wa kusuasua na kinachosikitisha sana ni Mkandarasi, haiwezekani Wilaya ya Kahama yenye halmashauri tatu inapelekewa Mkandarasi mmoja. Mkandarasi huyo huyo awepo Msalala, Mkandarasi huyo huyo aweke Ushetu, Mkandarasi huyo huyo awe Kahama Manispaa, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Kata yangu ya Mapamba, Ulewe, Ubagwe, Ulowa, Idahina, Chambo, Mpunze, Gulungwa, Nyamilangano pamoja na Bhutibu mpaka tunavyoongea havina hata ile kilometa moja moja, ni kidogo mno, ni maeneo makubwa yamesimamishiwa nguzo tu. Kwa hiyo ningeomba suala hili umeme uende lakini maeneo ambayo miji yake inakua kwa kasi Wakandarasi kwani kuna shida gani ya kupeleka Ushetu kuwa na Mkandarasi wake, Msalala kukawa na Mkandarasi pamoja na Manispaa kukawa na mkandarasi wake. Malalamiko mengine ya wananchi tunayasababisha sisi kwa sababu huwezi kupeleka Mkandarasi mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TARURA hiyo hiyo Kahama ina Meneja mmoja wa TARURA na Halmashauri zake tatu. Meneja huyo Ofisi yake iko Kahama Manispaa lakini huko huko aende kuzungukia kata 20 za Ushetu na vijiji 112 na vitongoji 560, barabara haziwezi kufunguka. Huyo huyo aende Msalala kwenye kata 18, huyo huyo abaki Mjini kwenye Manispaa ya Kahama kwenye kata 20, Meneja mmoja wa TARURA. Tulikuwa na Meneja wetu kwenye halmashauri zetu, lakini wakaondolewa wakarudishwa makao makuu wakapewa kazi ya ku-survey tu, meneja akabaki mmoja tu, haiwezekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mameneja wetu warudishwe, kama tunahitaji twende vizuri kwenye bajeti zetu za upande wa TAMISEMI, Mameneja hawa warudishwe haraka kwenye halmashauri zetu. Hali ni mbaya na tunavyoongea leo hali ya Ushetu ni mbaya mno. Barabara inayotoka Kata ya Ulewe kufanya mawasiliano na Halmashauri ya Ushetu ili wananchi waende kutibiwa kwenye hospitali yao ya wilaya, hakuna barabara, imekatika, wananchi hawapiti kabisa. Pia Kata ya Ubagwe kwenye Daraja la Ubagwe kuja Ulowa kwenda kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu, hakuna mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Naibu Waziri wa Ujenzi tuambatane naye kesho kwenda kushuhudia adha hii, kwa sababu mwaka jana hili nililisema kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwamba barabara hizi zimeshatoka TARURA zimepelekwa TANROADS, zinahudumiwa na Mkoa, lakini hakuna fedha zilizotengwa za matengenezo. Sisi kama Wabunge tunatakiwa tulie kwa nani, tulalamike kwa nani, tumwambie nani ili tuweze kufikishiwa huduma zetu kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasubiri mpaka tatizo litokee, wananchi waende na maji, akinamama wanaoenda kujifungua hospitalini waende na maji, ndio tukimbie sasa na magari yetu kwenda kuona tukio! Naomba niende na Naibu Waziri au Waziri wa Ujenzi akashuhudie kesho adha ambayo leo wanaipata wananchi wangu katika Jimbo la Ushetu. Barabara hazipitiki, naomba mwaka huu zitengewe fedha ili ziweze kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie suala la maliasili; jimbo langu ni kati ya majimbo yanayopakana na mapori mengi. Halmashauri yangu kupitia Baraza la Madiwani tulishakaa tukaomba wafugaji wetu watengewe eneo la malisho. Tumepeleka barua kwenye Ofisi ya Maliasili, tukapeleka barua TAMISEMI watutengee eneo kwa sababu ni maamuzi ya Baraza la Madiwani, lakini tunavyoongea ni mwaka wa pili hajaja hata Waziri kuja kushuhudia kwamba ni eneo gani, ni pori gani angalau walete wataalam litengwe kwa ajili ya malisho kwa sababu ni pori la halmashauri. Wafugaji wetu sasa hakuna mahali pa kuchungia, lakini wafugaji wetu hawa hawa wakiingia kwenye hayo mapori wanakamatwa na wanafilisiwa ng’ombe wao, hatuwezi kulikubali hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri twende tukashuhudie wananchi wangu eneo walilolitenga, angalau watoe ushauri kwamba pamoja na kwamba Baraza la Madiwani limetenga eneo hili, lakini ushauri wetu ulikuwa moja mbili, tatu, lakini hawataki hata kwenda. Naomba kupitia Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili twende akashuhudie wananchi ambapo wametenga eneo la malisho tuwasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba niliseme, tuna wananchi wenzetu ambao wanahangaika na mikaa, sijajua kwa nini Wizara ya Maliasili inabaki kupitia TFS kukamata tu wananchi, kukamata sio suluhu. Tumeanza kukamata wananchi hao na kuwaweka na kuwachomea baiskeli, kuchoma mkaa toka uhuru. Hivi hatuna akili ya kubuni kwamba twende na utaratibu gani sasa? Hivi kwa nini Wizara ya Kilimo imekuja na hoja ya kutenga mashamba ya block farm kwa ajili ya wakulima ambao hawana mitaji. Sasa maliasili inashindwaje kutenga maeneo ambayo yatakuwa special kwa wananchi wadogo wadogo ambao wanajishughulisha na biashara ya mkaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa watengewe maeneo wakapande miti ili waweze kuvuna miti yao badala ya kuwakamata. Wamewakamata miaka mingapi toka uhuru, leo miaka 61 tunakamata wamepata nini? Wameacha kuchoma mikaa? Si wako barabarani na baiskeli kila siku. Kwa nini gharama ambayo wanatumia kukimbizana nao kwenye magari wasiitumie sasa kuwa…

MWENYEKITI: Naomba umalizie mchango wako, sekunde tatu.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe tu, kwanza naunga mkono hoja, lakini niwapongeze sana Wizara ya Fedha kwa kutupelekea fedha nyingi kwenye sehemu ya Kilimo, lakini suala la maliasili na suala la Waziri wa Ujenzi, naomba tuondoke naye akashuhudie hali iliyopo katika Jimbo la Ushetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)