Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii fursa. Sambamba na hilo naomba nikupongeze kwa kukalia hicho Kiti ili kuweza kuliongoza Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzanaia, Mwenyezi Mungu akubariki sana, Allahu zidna I’lmi wa Ruzukna fahma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa hotuba yake nzuri ambayo ameitoa kwenye Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni hotuba nzuri ni hotuba ambayo imeeleza mambo mengi ambayo yanawagusa Watanzania wote. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ni kazi iliyotukuka, kazi hii anaifanya ndani ya nchi yetu ya Taifa letu la Tanzania na nje ya mipaka yetu Afrika na Duniani kote kwa ujumla. Hongera sana Mama tunakuamini, tunakupenda sana tuko bega kwa bega na wewe kuhakikisha kwamba kila dhamira uliyokuwa nayo tunakuunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Bunge hili au katika nchi yetu ya Tanzania hasa Wabunge ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi, hakuna Mbunge yeyote humu ndani atakayesimama bila kueleza mazuri aliyoyafanya Mheshimiwa Rais katika Jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye elimu amefanya makubwa, ukienda kwenye maji amefanya makubwa, ukienda kwenye maji amefanya makubwa, ukienda kwenye barabara amefanya makubwa, ukienda kwenye michezo ndiyo funga kazi amefanya makubwa sana. Kwa hiyo, tunakupongeza sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo nataka kuchangia kwa kuanzia na eneo lifuatalo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, unyanyasaji wa watoto, ndoa za jinsia moja, malezi na makuzi ya watoto wetu. Kwa nini nimeanzia katika eneo hili? Nina sababu kubwa ya msingi. Bila watoto hakuna Taifa, watoto ndiyo Taifa letu na ndio tegemeo letu. Watoto ndiyo baraka ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia wanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutasema Mama amefanya kila kitu katika Taifa letu, shule nani anatakiwa aende? Anatakiwa aende Mtoto! Hospitali watoto wanatakiwa waende, barabara watoto wanatakiwa wazitumie, kila kitu kinatutegemea sisi na kinawategemea watoto hawa. Leo sisi ni Wabunge ambao tuko humu ndani, tufikirie kwamba una mtoto wako umemuacha huko nyumbani unaambiwa mtoto huyu sasa hivi ameingia kwenye kulawitiwa, kama mzazi kama mlezi unajisikiaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa dhamana ya kuwalinda, kuwatetea na kuwasemea. Kwenye hili ni jambo ambalo hatukubaliani nalo kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye jambo hili tusiletewe vitu kutoka huko, sisi kama Watanzania tunao utamaduni, mila na desturi zetu ambazo ndizo zinatuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huu Wabunge hili ni jambo la kulaaniwa. Ni lazima kama Wabunge tuwe na azimio la kulikataa hili jambo sisi ndiyo waamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaniuma sana na Watanzania inawauma sana. Nikiwa Mke wa Rais siyo sasa hivi nimeondoka kwenye kuwa Mke wa Rais isipokuwa sasa hivi ni Mstaafu, nilikuwa na Taasisi yangu na inaendelea Taasisi ya Wanawake na Maendeleo kauli mbiu ilikuwa ‘Mtoto wa Mwenzio ni Mwanao’. Maana yake ni kwamba Mtoto wa Mwenzio akiwa mwanao utamtendea vitendo viovu? Huwezi kumtendea, utamlinda na katika kumlinda kule utamtengenezea maisha ya baadae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo dunia kuna baadhi ya watu wanatengeneza utaratibu wa kuzaa watoto wawili. Sisi tulikuwa tunazaa watoto wengi, dunia hiyo hiyo leo wanatuletea ndoa za jinsia moja, hivi tutakuwa na kizazi sisi? Mwanaume akishafanyiwa kitendo cha namna ile basi hawezi kufanya kazi, atapata wapi watoto? Hawezi kupata watoto. Kwa muktadha huo ni lazima jambo hili tulikemee vikali kadri inavyowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo kwa sababu wenzangu wengi wamesema na mimi niishie hapo. Hili jambo hatulitaki sehemu yoyote nitakayosimamishwa duniani nitasema hili jambo silitaki na silitaki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anatoa taarifa yake alizungumzia suala la shule 26. Miongoni mwa shule 26 shule 10 ziko tayari na ziko ndani ya Mikoa 10. Mikoa hiyo ni pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani na Mikoa mingine ambayo inafanya idadi kuwa shule 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachopenda kusema shule hizi ziko kumi na kila shule ni bilioni nne. shule hizi ni pesa za walipakodi wa nchi nchi hii ninachokiomba au ninachoshauri au kabla ya hapo mwezi wa saba mwaka huu zinaanza kuingiza wanafunzi wa kidato cha tano lakini katika uwasilishaji sikuona hata shule moja ambayo tungeona tu kwa mfano wakati wanatoa taarifa wanaonesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, nilikuwa kwenye Kamati ya Kudumu na Maendelaeo ya Jamii, sasa hivi niko katika kamati nyingine. Tulikuwa na lengo la kwenda kuzitembelea shule hizi hatujaweza kuzitembelea. Siamini kama kuna kamati imekwenda kuzitembelea. Ushauri wangu kamati hatawakiwa watu wachache waende wakazitembelee shule hizi kabla ya mwezi wa saba kuona je zina ubora? Ubora upo, je inawezekana mwezi wa saba au laa! Ushauri wangu waende wakazitembelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hizi shule tunaambiwa zimeisha ni kweli, mimi kwenye jimbo langu shule hii ipo ndani ya Jimbo langu la Mchinga. Ninachoshauri waweke ukuta yaani uzio kwa ajili ya kuwalinda mabinti hawa kwa sababu tunataka wasome vizuri na mabinti hawa ni mabinti wenye vipaji maalum lakini kwenye eneo la sayansi tunawahitaji wanasayansi wengi zaidi katika Taifa letu la Tanzania kwe sababu hii ni Tanzania ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nataka nizungumze kidogo kwenye suala la uvuvi, na uvuvi huu unawahusu sana vijana, wanaovua ni vijana, Ukanda wa Pwani una vijana wengi zaidi hata kwenye Jimbo langu la Mchinga kuna upande mzuri haujawahi kuokea nafikiri ni eneo la kwanza hata katika nchi yetu ya Tanzania, kuna beach nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba au ninachoshauri hao vijana uchumi wao mkubwa wanategemea Bahari, kule kuna Bahari hakuna mito, sasa vijana hawa wakopeshwe aidha maboti kwa ajili ya kujenga uchumi wao kwa ajili ya kipato chao, na si maboti tu na vitendea kazi vingine wakopeshwe watakuwa na uwezo wa kulipa kwa sababu watakwenda eneo la mbali kutafuta riziki lakini ukiwa na kile kimtumbwi hauendi mbali na unachokipata siyo kikubwa huo ndio ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka nizungumzie maliasili na utalii nilisimama hapa nikazungumzia suala la kuongezeka kwa tembo, na nilichangia hiyo hoja kuhusu tembo nikasema tembo ni wazuri sana tembo ni Wanyama ambao wanatuongeza fedha za kigeni tembo hao. Lakini watu wengi wanaopitiwa na tembo tembo siyo rafiki, tembo hii njaa ambayo sasa hivi inazungumzwa tumeletewa mahindi, ni kwa sababu maeneo mengine ni kwa sababu ya tembo wanakula vyakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaishukuru Serikali kwa kutuletea mahindi kupunguza ile njaa. nitakuwa ni mchoyo wa fadhila nisipoweza kuipongeza Serikali, Serikali imenitendea mambo mengi makubwa na mazuri miongoni ni kwenye hilohilo la hao Wanyama tembo hao, niliwaomba gari, wameniletea gari jipya Jimbo la Mchinga, niliwaomba kile kituo ambacho maaskari watakaa kwa ajili ya kuwadhibiti tembo na kuwafukuza wamenijengea kituo kizuri ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo wakati huo kulikuwa na maaskari wawili nikasema maaskari wawili watawezaje kudhibiti tembo 30 sasa hivi wameniletea maaskari zaidi ya 20. Kwa hiyo, ninawashukuru sana. Lakini sambamba na hilo kwa wale ambao watanzania wale ambao wanapitiwa na yale maeneo ambayo tembo wapo wasaidieni watanzania wanashida tena shida yao siyo ndogo shida kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo niwashukuruni sana nimshukuru sana Mheshimiwa Rais nina mambo mengi nitakuja kuyasema nitakapo changia Wizara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)