Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kukushukuru kwa kunifanya kuwa mchangiaji wa kwanza. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa uhai, namshukuru Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi Awamu ya Sita, nampongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, anakwenda vizuri sana na wananchi wa Jimbo la Same Mashariki wameleta salamu kwamba azipokee, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe na Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia, na leo ninaomba kuchangia kwa unyenyekevu mkubwa sana. Mheshimiwa Charles Kimei aliniuliza kwanini unachangia tangawizi kila siku, ninachangia tangawizi kila siku kwasababu kubwa moja, wananchi wangu wa Jimbo la Same Mashariki takribani asilimia 80 mpaka 85 wanalima zao la Tangawizi. Watanishangaa nikija nikaanza kuchangia kahawa, cocoa na miwa kwasababu wao wanalima zao la tangawizi, hivyo ni lazima nilizungumzie na kuisihi Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulianza kulima Tangawizi mwaka 1988. Zao hili lililetwa na mzee mmoja anaitwa Mzee Kilango Chikila. Hatujui alilitoa wapi, lakini alilileta mwaka 1988. Tukaanza kulilima zao la tangawizi kwenye miinuko mikubwa ya mita 800 hadi 1500. Tangawizi iliyo bora ni ile inayolimwa kwenye miinuko mikubwa, na Jimbo la Same Mashariki ni jimbo la milima na milima hii ya tarafa mbili yote inalima tangawizi kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelima tangawizi kwa miaka 34 sasa. Ninaongea kwa masikitiko kidogo lakini kwa unyenyekevu. Tumelima kwa miaka 34 sisi wenyewe bila kupata msaada kutoka Serikali Kuu; na kwa wakulima kama mnalima wenyewe bila ya kuboreshewa miundombinu ya kilimo ni lazima mtapata mazao hafifu. Tangu mwaka 2000 mimi nipo hapa Bungeni ninaongelea hili zao, lakini kwa uzito niliongea kuanzia mwaka 2005 nilipochaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninaiomba Serikali; na niongee kwa lugha ya unyenyekevu, lakini baadaye kama itapanda mnisamehe sana. Wananchi hawa wanalima hili zao wenyewe; nikiwa nina maana kwamba zao la tangawizi linatumia maji mengi sana, kwa hiyo tuna mirefeji lakini ile mifereji tumeitumia kwa miaka 34. Narudia tena, Serikali hatujapata msaada kutoka kwenu. Ni lazima Serikali mjue kwamba ninyi mnapaswa kuangalia miundombinu ya kilimo kwaajili ya wakulima. Hili ni hitaji la kikatiba la wananchi. Serikali ni lazima muwasaidie wakulima kwenye miundombinu ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka 34 hadi sasa ninapoongea tunategemea kulima tani 25,000 tu, lakini ujue tunavuna tani 25,000 tukiwa hatuna msaada wa Serikali. Iwapo Serikali mtafanya kazi yetu ya kikatiba ya kuboresha miundombinu ya kilimo ya Jimbo la Same Mashariki tunategemea tutavuna takribani tani 50,000. Juzi nilikwenda jimboni kufanya ziara nikaona nimletee Mheshimiwa Waziri picha hizi. Nikimaliza kuzungumza nitaomba hawa vijana waje wachukue wampelekee. Nimepiga picha miundombinu ya kilimo ya jimbo langu ambayo wananchi wanafanya wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa hii sio haki. Wananchi wanatengeneza miundombinu ya kilimo wenyewe ni kitu kigumu sana kwenye miinuko mikubwa ile ambayo Mheshimiwa Waziri wewe ulikuja, ulikuja kwenye ile miinuko. Na ninakuomba radhi, nitasema, pole sana kwa kuwa ulitapika sana kwenye ile miinuko. Ni kweli, yupo mwenyewe ameketi pale. Ile miinuko ni migumu lakini wananchi wale wanalima tangawizi kule, hawapati msaada wa Serikali, miundombinu ya kilimo yote hii wanatengeneza wenyewe. Mheshimiwa nitaomba upewe baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeanza kuchakata tangawizi sisi. Tumepata kiwanda ambacho sisi wananchi wa kule tulikijenga wenyewe. Hata hivyo ninaomba niipongeze sana PSSSF kwasababu ilikuja kuwa mbia, na sasa tumejenga kiwanda cha tangawizi ambacho ni cha kwanza katika Afrika Mashariki. Tangawizi tunayovuna ni hii hapa, tangawizi tunayochakata ni hii hapa, tangawizi ya unga tunayotengeneza ni hii hapa.
(Hapa Mhe. Anne K. Malecela alionesha aina ya tangawizi zinazolimwa, zilivyochakatwa na zao la tangawizi katika mfumo wa unga)
MHE. ANNE K. MALECELA: Kwa sababu kile ni kiwanda hatuwezi kuchakata tangawizi bila TBS kuja. TBS wameangalia ubora wa tangawizi ya Same Mashariki. Mtaniwia radhi, mkiangalia vizuri mtaona ni tofauti na tangawizi nyingine zozote hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumze kitu kimoja, kwa siku moja ya masaa 24 kiwanda kile kinachakata tani 10, sijui mmenielewa! Tani 10. Sasa sisi wenyewe kwa mwaka tunalima tani 25,000, siyo tangawizi ya kutosha kwenye kile kiwanda. Sijui Serikali mmenielewa hapa? Kwa siku moja tunachakata tani 10, kwa mwaka mmoja tunavuna tani 25,000 ina maana kile kiwanda hakitapata tangawizi ya kutosha. Serikali ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa nendeni mkaangalie miundombinu ya killimo na muiboreshe ili wananchi wale wavuna tangawizi kwa wingi, wawe na mazao ambayo yatakifanya kile kiwanda kipate malighafi ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwie radhi utakuwa. Angalieni Nigeria, Nigeria ina zao la tangawizi na ni zao la pili kuchangia kwenye GDP ya nchi asilimia 23. Kwa hiyo hili zao kama Serikali mtafanya kile mnachohitajika kufanya kwamba mkaboreshe miundombinu ya kilimo wananchi hawa watalima tangawizi kwa wingi. Mimi ninaomba hilo mliangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema naongea kwa unyenyekevu lakini Mheshimiwa Bashe hapana niongee kwa ukali sasa hivi. Kwanini mnawafanyia wale wananchi hivi? Mnategemea wananchi walime wenyewe, wavune kidogo waishi vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Bashe sitaunga mkono hoja yako hata kidogo; na ninatangaza kuondoa shilingi mpaka utoe jibu ambalo litanifurahisha, ama sivyo leo hotuba yako ya kilimo itakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme ukweli; kwanini Nigeria wao wanavuna tangaziwi nyingi kiasi kile? Ni kwasababu Serikali ya Nigeria imesimama imara kwenda kushika wananchi wake wanaolima tangawizi, na ndiyo maana Tangawizi inakuwa mchangiaji wa pili wa GDP ya nchi ile kwa asilimia 23. Mimi naomba, nafikiri sina mengi ya kuzungumza, hoja yangu kubwa wewe kama Serikali uje Same Mashariki ukaisimamie miundombinu ya kilimo cha tangawizi. Bila ya hivyo mimi na wewe hatutaelewena, sitaunga mkono hoja nitangoja mwisho. Ahsante sana. (Makofi)