Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nianze kwa kwa kukushukuru wewe kwa kunipa fursa hii. Pia ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na kutuletea bajeti hii ya kilimo ambayo ni ya kimapinduzi, nashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri ametupitisha kwenye awamu tulizopitia za dira mbalimbali za kuendeleza kilimo, naamini mpango huu unaleta mapinduzi kwa sababu unazingatia mambo muhimu sana ya kimkakati na dira na naamini kwamba Awamu hii ya Sita itakwenda kubadilisha sasa kilimo hiki ambacho kitakuwa kimewaondolea asilimia zaidi ya 65 wananchi wetu wengi umaskini. Namshukuru pia Waziri na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake pamoja na uongozi wa Wizara yote kwa kazi nzuri na kwa wasilisho zuri la bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na machache ambayo ni ya haraka haraka kwa sababu muda mfupi. Kwanza niseme kwamba ni vizuri katika kutekeleza tujue kwamba tunataka kupata tija ya haraka, kupata tija ya haraka ni lazima tuangalie Serikali ifanye tathmini ya mazao ya kimkakati kwa kila Mkoa. Siyo kila mkoa una comparative advantage zinazofanana. Unaweza ukazalisha mahindi kule Rukwa kwa bei nafuu sana ukayauza kwa tija sana kwa hiyo ikawa ni nzuri, lakini ukaanza kuweka tu kila zao liende kila mahali ukapeleke korosho kule Kilimanjaro itakuwa haifai. Kwa hiyo, lazima tuainishe kwamba Mikoa hii wale wenzetu walifanya hivyo, Mikoa hii kwa ardhi yake itafaa kwa mazao one, two, three au moja la kimkakati na lingine linaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kilimanjaro sisi zao letu la kimkakati kiasilia lilikuwa ni kahawa, lakini kwa sababu ya uzembe tuliofanya hapo katikati huduma za kiugani zikapotea ile kahawa kule sasa imekuwa haioti tena, hasa kule Vunjo. Kwa hiyo, sasa tumeanza kuingia kwenye mazao mengine hasa horticulture mazao ya mbogamboga, matunda na maua na kadhalika. Kwa hiyo, sasa naomba hivi katika mpango mkakati huu uliokuja wa kujenga maghala madogo madogo ningeishauri Serikali iende iangalie yale maghala yaliyokuwa yanamilikiwa na Vyama vya Ushirika madogo madogo kwa kila Kijiji halafu ijaribu kuyaboresha yale maghala na kuyaboresha hasa siyo kuyaweka tena kuhifadhi kahawa ni kuhifadhi mbogamboga, ndizi ndiyo zinauzika ndiyo zenye tija, ina maana muweke majokofu kwenye yale maghala ambayo siyo makubwa lakini yanaweza kutosheleza kuhifadhi mazao haya ambayo sasa hivi ndiyo yamechukua nafasi ya kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba kwa vile sasa tulizembea kahawa ikafa kule kwetu, basi wale ambao wanaotaka kuendelea kuzalisha kahawa basi tuwape mbegu za kahawa, miche ya kahawa bure. Waziri alituahidi naamini itatokea hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme kwamba tatizo kubwa katika kilimo ni kwamba tunazalisha kabla hatujajua bei. Kwa hiyo mbolea ikipanda bei wewe unatumia gharama kubwa kununua mbolea ile lakini hujui kwamba utaenda kuuza namna gani, bei utakayopata ukiuza ile kahawa yako au mahindi ni shilingi ngapi. Mimi nafikiri kama mwenzetu alivyosema pale kwamba ni vizuri Serikali itafuta masomo halafu iwe inatoa zile bei, inatangaza zile bei ambazo imepata kule nje. Inatangaza bei elekezi kwa kusema kwamba ukilima mahindi au ukilima mbogamboga hizi au ukilima kahawa au pamba kwa msimu huu tuna kuhakikishia kwamba tumeshapata wanunuzi contract buyers ambao watakubali kukulipa shilingi fulani, kwa hiyo margin utakayoipata kwa cost management ambayo tumefanya utapata margin hii, na ukimwambia mkulima atanunua mbolea bila hata ruzuku kwa sababu anajua kwamba tayari ukifuata ile bei ya mbolea na input nyingine kwenye ile bei ambayo utapata ni faida. Sasa sisi tunazalisha halafu tunakwenda kupata hasara hata ukiweka ruzuku halafu ukienda kuuza kwa hasara it doesn’t help na tumeshapoteza ruzuku yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwa mfano sasa hivi suala zima la mahindi. NFRA ina mahindi mengi lakini bei za mahindi zimepanda zimefika mpaka shilingi 800 kule Arusha. Mimi nafikiri kwamba huu ndiyo wakati ambapo sasa NFRA isiuze kwa middlemen yale mahidi, mahindi yauzwe ili yamfikie mlaji moja kwa moja. Kwa sababu ukiuza kwa middlemen ina maana ile faida ya yale mahindi ambayo tumewezesha NFRA ikanunua itakwenda kwa wale wafanyabiashara wa kati. Kwa hiyo, naomba hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya kuangalia ununuzi, uuzaji wa mazao yetu kama pamba. Tunajikuta kwamba kwa sababu riba zilikuwa kubwa, zinaanza kushuka hapa lakini ni kwamba riba kwetu bado zipo juu sana na watu wanaouziwa mazao yetu ni wale ambao wana-process hapa kama pamba kutengeneza nguo. Kwa hiyo, tunaomba hivi ile Benki ya TADB iwe inawawezesha wale wanunuzi wenye viwanda vya ku-process mazao yetu hapa kupata mikopo kwenye riba kati ya Mbili mpaka Nne hivi ili waweze kununua kwa wingi na wakienda kuuza nje wao zile bidhaa walizo- process hapa waweze kuziuza kwa faida in a way ambayo ina ushindani, ndiyo tunasema sasa dira yetu sasa ni uchumi shindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba hiyo haitawezekana kama watu watakopa wahifadhi hii pamba ya kuchakata mwaka mzima halafu riba inaongeza zile bei kwa hiyo baadaye itakuwa hawawezi kushindana wanapoenda kwenye soko la dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa naamni kwamba kweli bajeti hii ni bajeti ambayo ni tofauti, ni bajeti kabambe, ni bajeti itakayotekeleza dira ambayo inayosadikika. Isipokuwa naomba Mungu aniweke hai mpaka mwaka 2030 ili nione mafanikio haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.