Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia nimpongeze Spika wetu pamoja na Naibu Spika na Wenyeviti wote ambao wamechaguliwa kwa namna ambavyo mnaendesha shughuli za Bunge hili kwa uwazi na kwa namna ambayo tunapata tija. Pia nichukue fursa hii kutoa shukrani za pekee na pongezi ambazo zinatoka kwa wananchi wangu wa Vunjo kwa Mheshimiwa Rais wetu na Amiri Jeshi wetu Mkuu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wake na Waziri Mkuu pia kwa namna ambavyo wanaendesha nchi yetu tukabaki tukiwa na nchi iliyotulia kisiasa na kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kasi ya ukuaji wa Pato letu la Taifa bado linaridhisha ukilinganisha na sehemu nyingine ambapo tunaanza kuona recession ikitokea, mporomoko ukitokea lakini hapa kwetu tunaona kwamba pato linakua kwa takribani asilimia tano. Vilevile mfumuko wa bei uko chini kuliko kwa majirani zetu, pia na riba zimeanza kushuka, ingawa si sana lakini zimeanza kushuka; jambo ambalo linatuonesha kwamba pengine hapa tunapokwenda ni pazuri zaidi kama hali ya dunia nayo itarudi kwenye hali ambayo ni tulivu kutoka hii ya sasa ambayo mambo yanakuwa magumu. Naamini kwamba kwa wanavyotabiri wenzetu ni kwamba ndani ya mwaka huu wataona mafanikio sana kwa sababu vita vinaendelea na kuna mkanganyiko kwenye soko la kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti,sasa niseme hivi, kusema kweli wana-Vunjo wamemshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa ujumla kwa miradi mingi kama wengine wanavyosema. Tumepata miradi mingi kama vile mradi wa maji kule Njia Panda ambao umeshakamilika, shilingi bilioni 2.3 zimekwenda huko. Vilevile kuna miradi ya maji kwenye Kata za Mwika Kaskazini, Mwika Kusini, Mamba Kaskazini, Mamba Kusini, Marangu Mashariki na Magharibi, Kilema Kati na Kilema Kusini na yote inaendelea. Miradi yote ina takribani shilingi bilioni tatu, haijakamilika. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri nilikutana naye na ameniahidi kwamba fedha zitakwenda kukamilisha miradi hii kabla ya mwisho wa bajeti inayoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata vituo viwili vya afya, kituo kimoja tumepata kule Kirua Vunjo ambacho kilikuwepo lakini kikainuliwa hadhi ya kuwa kituo cha afya na kimepata vifaa vyote ambavyo vinastahili. Pia tumepata Kituo cha Afya Malangu Mashariki. Vyote hivi tunazungumza zaidi ya bilioni moja ambazo zimetumika na Serikali.
Mheshimiwa Spika, vilevile tumepata madarasa; kila mtu anayafahamu madarasa ya UVICO pamoja na madarasa mengine. Tumepata madarasa shule nzima ambayo ni ya wasichana pale Njia Panda. Kwa hiyo nataka niseme kwamba Serikali imewekeza vizuri na Mungu awajalie wote ambao wamewezesha miradi hii kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme pia kwamba TARURA wamepata pesa, tumepata barabara, zimechimbwa vizuri. Hata hivyo ninachosema ni kwamba barabara nyingi sasa hivi zimeharibika tena. Hii ni kwa sababu barabara zinazopitishwa grader mvua zikinyesha, na kwa sababu kule kwetu ni mwinuko basi zitakuwa zimepoteza hadhi. Lazima sasa tuombe TARURA wapate fedha ya ziada kwenda kukarabati hizi barabara ambazo zimeharibika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza nikatumia muda mwingi sana kuzungumzia mambo ya jimbo, lakini nasema kwamba wote tunashukuru; tunajua kwamba fedha imetafutwa na Mheshimiwa Rais. Mimi sitazungumzia juu ya CAG kwa sababu nitatoa machozi hapa nikianza kuizungumzia CAG. Mngeacha nimalize haya kwanza na baadaye tutaanza kuzungumza, kama mwenzetu alivyosema, pengine tutakuja kwa wakati mwafaka.
Mheshimiwa Spika, lakini nitumie fursa hii kuzungumzia mambo mengine ya kitaifa ambayo si lazima yawe ya kijimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza unajua kwamba Sensa imetoka, takwimu zimeanza kutoka na takwimu muhimu zimeshaanza kutoka lakini nashangaa sana hatujaona hii mipango inayokuja ikigusia na kuonesha kwamba kuna namna gani tunaenda kujipanga upya ili tutoe miradi na huduma zetu hasa za jamii kwa kuzingatia idadi ya watu kwenye majimbo.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye Serikali kuna baadhi ya halmashauri yenye majimbo zaidi ya moja, zinayo majimbo matatu. Sasa inapofika kwamba wakati Serikali inapoanza kugawa keki hii wanasema tunapeleka kwenye halmashauri, halmashauri inakuwa na majimbo mawili tunaanza kugombana na majimbo yote ni makubwa. Kwa mfano Jimbo la Vunjo lina idadi zaidi ya watu 255,000, Jimbo la Mheshimiwa Ndakidemi, Moshi Vijijini lina watu 284,000 halafu unatoa ambulance moja. Tunaanza kugombana na mwenzangu hapa, kwamba sasa zitaenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naamini ni vyema kwamba mzingatie kuwa kuna halmashauri zina majimbo zaidi ya mawili, na aidha muangalie ukubwa wa hayo majimbo. Kuna halmashauri ambazo idadi ya watu ni nusu ya hao tulio nao sisi lakini wao wanakuwa treated kama halmashauri wanapata kama sisi tunavyopata mpaka tunabakia kupigana huko bila sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nataka nizungumzie suala zima la kutengeneza bajeti hii ya mwaka huu. Bajeti tunayotengeneza sasa hivi haikuzingatia uhalisia wa hali ya uchumi wa dunia, na ndiyo maana tunaona kwamba fedha zilizopokelewa katika Wizara nyingi kwenye upande wa miradi ya maendeleo zimekuwa zinaenda kwa kusuasua sana. Sehemu nyingi zimepata chini ya asilimia 50 ya bajeti ya maendeleo; na sababu ni nini; tulitegemea kwamba tutapata fedha nyingi kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nawaambia kwamba kwa hali ilivyo sasa hivi kwenye uchumi wa wenzetu ambaoo unapata matatizo ya recession inakuwa vigumu sana wahisani kuja kwa kasi hiyo waliyokuwa wanatumia mwaka uliopita. Kwa hiyo ni lazima tujaribu kwa kuona tutafanyaje na ili mwaka huu tuweze kuzingatia. Kusema kweli riba zimepanda juu kwenye soko la kimataifa; na kwa vile zinapanda juu inakuwa vigumu sana kupata mikopo. Wale wawekezaji wetu wanapeleka fedha Marekani kwa sababu riba za Marekani zimepanda hadi kufikia asilimia tano. Kwa hiyo wanapeleka fedha badala ya kutukopesha sisi; na wakitukopesha riba itakuwa juu sana kwahiyo itakuwa si himilivu na hivyo Deni la Taifa linaweza likaanza kuwa si himilivu. Kwa hiyo nataka niseme kwamba hilo ni jambo ambalo tunahitaji kuliangalia sana tuvyoelekea mbele, na ninaamini tutaona kwamba hali itakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti,naomba niishie hapo, lakini naendelea kutoa shukrani kwa nafasi niliyopewa. Ninaamini kwamba Serikali itazingatia ushauri tunaoutoa kwa sababu ninamini una uhalisia na itatuwezesha kuwa na mpango ambao unatekelezeka bila kulaumiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.