Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuipa fursa hii. Kwanza kabisa naomba niende kwenye suala la mifugo. Wakati ninakwenda kuchangia Bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naomba moja kwa moja nianze na Wizara ya Mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la ufugaji wa samaki kwa maana ya vizimba. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga fedha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya uwezeshaji kwenye eneo hilo la suala la ufugaji wa samaki kwenye vizimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tarehe 5 niliuliza swali linalohusisha ufugaji wa samaki hao na ikaonekana kwamba fedha hii imetengewa Shilingi bilioni hizo nilizozitaja na kwamba inakwenda kupelekwa kwenye Ziwa Victoria. Swali langu la pili la nyongeza nilikuwa nimeiomba Serikali kwamba ipeleke gawio sawa na maziwa mengine. Isiende shilingi bilioni 20 hii yote katika Ziwa Victoria bali iende na kwenye maziwa mengine ikiwemo Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Waziri wa Mifugo Mheshimiwa Abdallah Ulega baada ya swali langu aliniita ofisini kwake na akaniambia ameshazungumza na timu yake sasa tunapata gawio, Ziwa Nyasa tunapata gawio la shilingi bilioni tatu ambayo itapelekwa kwenye suala la ufugaji wa vizimba katika Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine naomba niende kwenye suala la viwanda na biashara. Kwenye suala la viwanda na biashara naomba niende moja kwa moja katika Kata ya Mwengemshindo katika Manispaa ya Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ walichukua maeneo ya Kata hiyo ya Mwengemshindo ni miaka 15 sasa tangu maeneo hayo yamechukuliwa na wananchi bado wanalia hawajalipwa fidia, hawaelewi hatma ya maisha yao. Wanashindwa kuendeleza aidha kuongeza kama ujenzi wa nyumba au kufanya shughuli nyingine zozote zile za maendeleo. Fedha hii Shilingi bilioni 3.9 leo hii nimesimama hapa katika Bunge lako tukufu ninataka Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja ku-windup hapa aniambie ni lini Serikali itapeleka fedha hii shilingi bilioni 3.9 kwa wananchi wa Kata ya Mwengemshindo katika Manispaa ya Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye miundombinu, naomba nizungumzie barabara ya kilometa 28 ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Barabara hii inatoka Mbinga mjini inapita katika Kata ya Ruwaita, inapita Kindimba, Mahenge, Litembo ambayo barabara hii ni barabara ya kimkakati. Mheshimiwa Rais alikuja pale na akatoa ahadi, Rais wa Awamu ya Sita akiwa Makamu wa Rais alitoa ahadi pale kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Sasa ni wakati muafaka, ninaomba fedha hii itengwe ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika naomba niende kwenye barabara ya kilometa 35 ambayo inatoka Kigonsera kwenda Matili yenye urefu kilometa 35 ambayo inapita Kitumbalomo, Lukalasi. Matili ni kata ambayo ndiyo inabeba uzalishaji mkubwa wa mazao ya nafaka katika Mkoa wetu wa Ruvuma. Kwa hiyo, ninaomba barabara hii sasa ni wakati muafaka fedha ipelekwe ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami na Mheshimiwa Benaya Kapinga amekuwa akizungumzia sana barabara hii. Naomba sasa kwa heshima hiyo ya Mheshimiwa Kapinga na mimi Jacqueline Ngonyani Msongozi, barabara hii sasa iweze kutengewa fedha na iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Barabara ya Likulufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 124. Hii ni barabara ambayo inaunganisha Nchi yetu ya Tanzania na Nchi ya Mozambique na barabara hii nimekuwa nikiimba kila nikiamka kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka husika lazima niisemee barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama ambaye ndiye inapita kwenye jimbo lake amekuwa akiizungumzia sana hii barabara na sasa mimi pamoja na yeye kwa heshima hiyo tunaomba barabara hii ianze kujengwa haraka sana kwa sababu barabara hii ni barabara ambayo itaunganisha hizi nchi mbili. Manufaa ya barabara hii ni kwamba itasaidia kuchochea uchumi katika Nchi yetu ya Tanzania, itasaidia kuimarisha soko ambalo limjengwa kwenye Mpaka wa Tanzania na Mozambique pale Mkenda. Tuna soko ambalo limejengwa mpaka sasa fedha ya Serikali imetumika lakini bado halitumiki kwa sababu miundombinu ya barabara pande zote mbili haijakaa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii itaongeza biashara kwenye eneo hilo la mpaka. Itaongeza mzunguko wa fedha katika Manispaa ya Songea na Jimbo la Songea Vijijini, Jimbo la Peramiho kama nilivyosema. Pia wananchi wa kutoka Mozambique watatumia uwanja ule wa ndege wa Songea ili kuweza kusafiri kwenda kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa barabara hii itatengewa fedha kwa maana ya heshima hiyo lakini pia mumpe heshima Chief Whip wetu ambaye amekuwa akifanya kazi hapo wakati mwingine anakosa fursa ya kusema kama ninavyosema basi mpeni hiyo fursa ya hiyo barabara ni barabara muhimu sana ili tuweze kufikia malengo tunayokusudia kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ukarabati wa shule kongwe. Iko Shule ya Sekondari ya Msindo iliyopo katika Wilaya ya Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma. Hii shule ni kongwe, shule hii imechakaa sana inahitaji ukarabati, halikadhalika katika shule hiyo hiyo kunahitajika hostel ya watoto wa kiume. Kimsingi wamekuwa wakilala kwenye jengo ambalo halifai na wala jengo hilo ni kama vile ghala. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ifanye jitihada za makusudi ili kuokoa ustawi wa watoto wale mwisho wa siku tunahisi kwamba wanaweza wakapata magonjwa mengine kwa sababu jengo hilo wanalokaa vidirisha ni vidogo sana kwa sababu ni ghala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika sekondari hiyo hiyo kuna hitaji la bwalo la chakula la shule hiyo. Sasa hivi wanapikia kwenye eneo la wazi, kwenye mti nje wanapikia chakula hapo. Kwa hiyo, ninaamini bwalo likishajengwa maana yake hata ustawi wa afya zao wale watoto wetu zitakuwa ni njema. Kwa hiyo, niiombe Serikali ifanye hivyo haraka sana ili kuokoa hali halisi na mazingira halisi yanayojitokeza kwenye shule hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya, Wananchi wa Kata ya Msindo wamejenga jengo la upasuaji katika eneo la jengo ambalo lilianza awali kabla ya kituo cha afya hakijajengwa. Jengo lile wananchi wamejitolea wamefikia kiwango cha kuezeka lakini hawawezi kuendeleza kwa sababu hawana fedha ndiyo wameishia hapo. Tunaomba msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipelekwe fedha pale ili waweze kwenda kumalizia jengo lile la upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka sasa niendelee kwenye suala hilo hilo la afya. Tarafa ya Mbuji katika Wilaya ya Mbinga, Jimbo la Mbinga Vijijini ni tarafa ambayo inabebwa na Kijiji cha Mpaka, Unyoni, Litembo, Mbuji, Kitulo. Tarafa hii yenye vijiji hivyo vikubwa bado haina kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wewe unafahamu vizuri Mkoa wa Ruvuma, tunaomba sasa upeleke kituo cha afya kikajengwe kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi ambao wanaizunguka tarafa ile, kwa maana ya kata tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu zahanati. Katika jimbo hilo hilo, wilaya hiyo hiyo ya Mbinga bado kuna tatizo la zahanati, zahanati hakuna. Nilipokuwa nazungumzia kituo cha afya maana yake hata zahanati huko chini hakuna. Kuna uhitaji wa zahanati 38 katika eneo hilo. Mheshimiwa Banaya amekuwa akipiga kelele hapa kila siku anaomba zahanati zijengwe katika maeneo haya. Sasa na mimi kama mama nimesimama hapa katika Bunge lako kulisemea hilo hilo. Nipaze sauti, labda kwa sababu ni mama, ili wananchi hawa waweze kupata fursa ya kujengewa zahanati na nitataja baadhi siwezi kutaja maeneo yote 38; basi nitataja baadhi itakuwa ni wakilishi kwa maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zahanati hizo zinazotakiwa zijengwe ni katika Kijiji cha Likoho, Lugavi, Njombe, Kizota, Ukata, Lisao, Mzuzu, Mhagawa, Mtaya, Liyombo, Liuhula na nyinginezo. Naomba maeneo haya yatengewe fedha ili zianze kujenga. Safari ni hatua, hata ukitutengea 10 tu itakuwa ni hatua nzuri kwa mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliongelee ni suala la mmomonyoko wa maadili…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline nakuongezea dakika moja tu malizia hilo kwa sababu ni la maadili.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwenye suala la mmomonyoko wa maadili naomba tu niseme kwamba tuna kila sababu sisi kama Wabunge kuhakikisha kwamba tunaleta sheria iwe ya mkazo hapa Bungeni, itengenezwe sheria na sisi tuipitishe kama Bunge ili kuweka utaratibu mzuri ambao utawafanya wale wanaoshughulika na mambo haya waweze kubanwa kwa namna moja au nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa kwa kuwa wewe ulikuwa Makamu Mwenyekiti naomba upendeleo wa dakika moja. Naomba nitumie nafasi hii kuwapongeza sana viongozi wa dini ambao wamejitokeza kuzungumzia suala la mmomonyoko wa maadili katika nchi yetu. Tumeona Shehe Mkuu wa Tanzania amesema, tumeona maandamano kule Arusha, na tumeona viongozi wa madhehebu mbalimbali wanazungumza sana kuhusiana na kukemea kuhusu jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona pia viongozi hawa wa dini wa madhehebu mbalimbali wote ambao wanakemea, lakini nampongeza sana Apostle Buludoza Boniphace Godwin Mwamposa. Yeye kabla ya kuanza ibada kila jumapili anaanza kukemea jambo hilo na wote wafanye hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Jacqueline.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenye dhamana…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Jacqueline…
MHE. HACQUELINE N. MSONGOZI:… wa maendeleo na ustawi wa jamii hatujamsikia sauti yake akikemea jambo hili hatumwelewi tunaomba atoke na aseme kuhusu jambo hili.