Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ameendelea kunilinda na kwamba nipo hai sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa weledi mkubwa sana, ninamshukuru pia kwamba kwenye Jimbo letu la Ngorongoro tumeendelea kupata fedha nyingi sana kwa ajili ya maendeleo zikiwepo fedha za afya, elimu, maji pamoja na umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba pia nichangie hoja ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia katika Bunge lako, kuhusiana na masuala ya ufisadi kwenye nchi yetu. Nimesikia kwamba Wabunge wengi wanasema hao watu watupishe. Watupishe waende wapi? Wanatakiwa warudishe fedha za Watanzania ndiyo waweze kitupisha, hili linatakiwa kufanyika na wale wote waliopewa mamlaka na Mheshimiwa Rais, kwa sababu inaonekana Mheshimiwa Rais yeye amechukia ufisadi sana, lakini inaonekana kwamba baadhi ya watu ambao ni wateule wa Mhehsimiwa Rais, hawauchukii ufisadi ndiyo maana tunamuona Rais anachukia lakini watu wengine wamenyamaza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu la Ngorongoro tumepata fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo lakini kunakuwepo na vikwazo vingi sana. Kwa mfano, leo Wizara ya TAMISEMI inaleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa lakini unampa mtu wa Ngorongoro shilingi milioni 20 ajenge darasa sawa na mtu aliyeko Dar es Salaam! Kule ukitoa cement kutoka Arusha mpaka Ngorongoro cement inafika kwa shilingi 25,000. Mwananchi aliyeko Arusha Mjini ananunua cement kwa shilingi 16,000. Inatakiwa tunapotoa fedha kwa jaili ya miradi ya maendeleo tuangalie umbali na mazingira katika Majimbo yetu. Siyo unampa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro milioni 20 ajenge darasa na hivyo hivyo unampa mtu wa Dar es Salaam Milioni 20, Mkurugenzi wa Dar es Salaam ananunua cement kwa shilingi 14,000 mpaka 15,000 lakini Ngorongoro cement inafika kwa shilingi 25,000, yule Mkurugenzi utakuwa unamuonea! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba watu wa TAMISEMI wanapanga miradi ni lazima waangalie maeneo wanayopeleka hizo fedha. Unampa Mkurugenzi shilingi milioni 400 ajenge Sekondari akiwa Dar es Salaam, akiwa Morogoro unampa pia na wa Ngorongoro ajenge kwa shilingi milioni 400. Wakati kule hata lori ya mchanga ni zaidi ya shilingi 300,000 lakini kusafirisha kutoka Arusha mpaka Ngorongoro unatumia gari za shilingi 1,500,000 mpaka Ngorongoro wakati mtu wa Arusha anakodisha gari kwa shilingi labda 200,000 tu. Kwa hiyo, ukijaribu kuangalia ni lazima tutekeleze miradi, tutenge fedha za miradi kwa kuangalia maeneo. Majimbo yetu yaliyoko mbali ni lazima tu – consider cost tunazowapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo letu la Ngorongoro huduma zetu za afya bado ni duni sana. Ukijaribu kuangalia kwenye Kata zetu. Kati ya kata 28 unakuta kwamba ni zaidi ya Kata Sita tu ndiyo zenye vituo vya afya lakini Kata nyingine 22 hakuna vituo vya afya. Kwenye Vijiji pamoja na Kata hakuna zahanati, lakini mwaka jana Serikali ilisitisha huduma kwa ajili ya ndege ya Fly Medical Service iliyokuwa inatoa huduma ya chanjo kwenye vituo 18 ndani ya eneo la Ngorongoro. Kupitia Hospitali ya Wasso kulikuwa kuna vituo 10, kupitia Hospitali ya Kanisa ya Endulen walikuwa wana vituo Nane lakini Serikali imesitisha huduma hiyo. Kwa hiyo, wale wananchi waliokuwa wanahudumiwa kwenye vituo 18 kwenye Kata ambazo hazina zahanati na Serikali haijafikisha barabara katika yale maeneo wananchi wale hawapati huduma ya chanjo, watoto wadogo pamoja na wakina mama wajawazito.

Mhehsimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali tuiangalie kwa sababu ndege ile imesajiliwa Marekani mwaka 1979 na imetoa huduma Tanzania kwa miaka yote 44 bila shida, lakini hatujui ni nini kimetokea mwaka 2022 ndege ile ikanyimwa kufanya kazi. Wale wananchi wakina mama wajawazito ambao hawana namna ya kufikia hospitali na watoto kupata chanjo ni wakati muafaka sasa Serikali kuwaruhusu wale wamisionari waweze kutoa huduma tena katika eneo la Ngorongoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Uchukuzi, Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu anajua nilishamwandikia, Waziri wa Uchukuzi anajua, pamoja na Waziri Mkuu anajua nilishamwambia suala hili kwa muda mrefu, toka mwaka jana mwezi wa Sita mpaka sasa hivi kuna watoto wadogo wanazaliwa na ambao wana miezi Tisa sasa hawapati huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa inaratibu suala lingine la kuhama kwa hiyari eneo la Ngorongoro. Suala lile hakuna mtu anayepingana na mtu anayehama kwa hiari, wananchi wamendelea kwenda wenyewe. Tumeona kwenye ripoti ya CAG kwamba wananchi waliohama ni 2.5 percent ambayo ni kaya 500 zenye watu zaidi ya 2,580, lakini wananchi wengine waliobaki kwa sensa ya juzi ni zaidi ya kaya 25 ambazo zina watu zaidi ya 100,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakaa, siku ile Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema hapa kwamba ni suala la hiyari, lakini wananchi waliobaki zaidi ya 100,000 ukienda kwenye eneo la Tarafa ya Ngorongoro kuna shule zaidi ya 26 za msingi zenye watoto zaidi ya 18,167. Watoto wa Sekondari zaidi ya 3,250 hakuna vyoo, watoto wanaenda chooni porini kwa sababu Serikali imekatalia kujenga vyoo, vyoo vimejaa, hawatoi ruhusa ya wananchi kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wao, kwa nini hili linatokea kama suala lenyewe ni hiari kwa nini watu walazimishwe kuishi katika maisha ambayo hayafai kwa binadamu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba ni lazima Serikali iweke wazi lengo lao kwenye eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, kama ni kuhama kwa hiari watu wanaondoka lakini mpaka leo watu waliojiandikisha ni kaya 1,500, lakini mpaka leo wamechukua kaya 500. Wale waliobaki kaya zaidi ya 1,000 hawana mbele wala nyuma hawajui wanafanya nini, wako stranded katika maisha yao hawawezi kuendelea tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba katika eneo letu la Tarafa ya Ngorongoro Wizara ya TAMISEMI inapanga fedha inapelekwa wananyimwa vibali kwa ajili ya kujenga na watoto wanakaa madarasani mpaka nje. Ni lazima Serikali iweke wazi wale wananchi wasiendelee kuishi kama watu ambao hawatambuliki kama watu ambao hawatambuliki katika nchi yao. Ni vizuri tujue kwamba wale wananchi wako pale lakini suala hili ni la hiari. Suala lenyewe limekuwa ni upigaji mtupu, angalia leo usafiri kutoka Ngorongoro mapaka Handeni gari ni sawa na kontena kutoka China kuja Tanzania ni ufisadi mtupu. Watu wanajitochotea fedha, watu wanawalipa watu ambao hawahusiki, unakuta nyumba zingine ni hewa. Nyumba unaandikiwa namba 59 hiyo nyumba haipo, mkatafute, au nyumba namba 57 na 58, 55 na 56, nyumba hazipo, watu wanajiandikia wanajichukulia fedha za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichoonekana kwenye ripoti ya CAG ninaishauri Serikali mkafuatilie ule mradi muone kwamba ni mradi wa watu ambao ulibuniwa kulikuwa kuna fedha ambazo zipo walitaka wale wakakosa njia. Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro sasa hivi watu wanasema limejaa lakini eneo lenye watu ni five percent only, maeneo mengine yako wazi, bado inaweza kumudu model ya multiple land use model.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende tena kwenye suala la barabara yetu ya lami kutoka Wasso mpaka Sare. Tunaishukuru Serikali kwamba tumepata kilomita 49, lakini niiombe Serikali muendelee kutuangalia, Ngorongoro barabara iliyopo ni hiyo moja na ndiyo inashikilia uchumi wa Wilaya yetu ya Ngorongoro. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, kwamba aliahidi kilomita 50 tunaiomba kwenye bajeti hii iweze kututengea kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Ngorongoro nao kunufaika na matunda ya rasilimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la umeme. Tunazo Kata za Malambo, Samunge, Pinyinyi pamoja na Kata ya Kirangi eneo la Mageri pamoja na Bwero Kata ya Samunge na maeneo mengine ambayo hayana umeme kwenye Jimbo letu la Ngorongoro. Wameweka nguzo zaidi ya miaka 5 mpaka sasa hivi nguzo zingine zinaanguka, ninaishauri Serikali sasa iweze kumalizia miradi ya umeme kenye Wilaya yetu. Wananchi wanahitaji maenedeleo na umeme ni maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningetaka kulizungumzia ni suala la elimu. Wataalam wanasema ukitaka kuliua Taifa uharibu vitu viwili. Suala la kwanza ni afya pamoja na elimu. Kwenye shule zetu za msingi tunakuwa na mrundikano mkubwa wa wananfunzi ambao inapelekea wengi kuhitimu Darasa la Saba hawajui kusoma na kuandika, nimesikia pia Wizara ya Elimu wako katika utaratibu wa kuweza kubadilisha mitaala yetu. Nafikiri tusifanye elimu kama eneo la majaribio.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)