Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali ya yote kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutujalia leo kuja kukaa hapa kujadili bajeti ya kuendesha nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi. Kuna mambo hapa yalisemwa na wengi walizungumza toka tumeanza Bunge hili kuhusu Ripoti ya CAG. Sitozungumza, ila nina shairi dogo ambalo lilitungwa na Haji Gora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Haji Gora alisema kwamba;
Kuna la ajabu mno la kushanagaza moyoni,
Kuna wakongwe watano wanashindana kwa fani, Wakata mawe kwa meno na kujaza matumboni, Nasema kinaganaga mengine yasikieni,
Farasi kula mizoga na kufukua mavani?
Kuna kijungu cha kuaga bila moto jikoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye agenda hiyo nimemaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja katika agenda na mchango wangu wa Fungu 65 – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu. Hapa nazungumzia vijana na ajira. Tatizo la ajira ni kubwa kwa dunia nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa Mwalimu tatizo la ajira lilikuwepo, wakati wa mzee Mwinyi tatizo la ajira lilikuwepo, wakati wa Benjamin Mkapa tatizo la ajira lilikuwepo, wakati wa Jakaya Kikwete tatizo la ajira lilikuwepo, wakati wa Magufuli tatizo la ajira lilikuwepo na sasa wakati wa mama Samia tatizo la ajira bado lipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali yetu tukufu ilifanya utafiti na utafiti huo iliufanya kuangalia nguvukazi ya nchi ambapo tuna nguvukazi ya watu 23,536,000 na zaidi. Lakini ilivyofanya hapo iliangalia hali halisi ya soko la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti hiyo ilionesha kwamba asilimia takribani 80 ya nguvukazi ya Tanzania ujuzi wao uko chini; asilimia 16.6 ya nguvukazi ya Tanzania ujuzi wao ni wa kiwango cha kati; asilimia 3.6 ujuzi wao ni wa kiwango cha juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi kwa kuwa ni nchi ya kiwango cha kati tulitakiwa asilimia ya kiwango cha juu iwe asilimia 12; asilimia 34 iwe ya kiwango cha kati na asilimia ya kiwango cha chini iwe 54 kwa kuwa tupo katika uchumi wa kiwango cha kati. Hii ilifanya ndiyo chimbuko la kuwa na programu ya kukuza ujuzi kwa ajili ya kupata ajira. Kwa bahati tukaweka hiyo programu, programu hiyo na components zake za kukuza ujuzi zikatajwa na iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikubaliana sekta binafsi na Serikali kwamba programu hii ambao ni Mradi Namba 6581 itasimamiwa na SDL (Skills Development Levy), kwamba one- third itatoka itakwenda kushughulikia tatizo la kukuza ujuzi kwa vijana. Na kukuza ujuzi kwa vijana maana yake tutapata tija kwenye bidhaa zetu na ajira zitazalishwa kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skills Development Levy iliyokusanywa kwa mwaka 2021/2022 ilikuwa bilioni 291, ambayo one-third yake ilikuwa bilioni 97, lakini kwa bahati utekelezaji wa programu hii ulivyokwenda, ilianza kuchangiwa kwa bilioni 15, tukaja bilioni 18 na sasa hivi tumeshuka tuko katika bilioni tisa. Tunajiuliza, je, tatizo la ajira kwa vijana liliisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa nataka niseme neno; na ninataka nitoe rai; Mwenyezi Mungu anasema kwenye Quran Tukufu fama amali Musa illa dhuriyya. Musa hajaaminiwa isipokuwa walibakia vijana watupu ndio waliomuamini Musa na niyo waliomfuata Musa. Lakini wazee wote waliogopa kwa sababu ya kumuogopa firauni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa vijana ambao sisi tunaanza kuwashushia hata hiyo pesa kwa ajili ya wao kupata ajira na kukuza ujuzi, tutakimbilia wapi? Serikali lazima itazame katika hili. SDL inatakiwa ipelekwe bilioni 97, sasa kama bilioni 97 haikupelekwa, je, hawa vijana tunawapeleka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo langu; SDL kama haijatoka kwa kiwango cha kutosha kama tulivyosema huku katika makubaliano, kwamba one-third ya SDL iende kwa ajili ya ajira na mafunzo kwa vijana ili kukuza ujuzi, hapa nina lengo la kuzuia shilingi kwa sababu vijana ni tatizo kubwa. Leo tutazame matatizo yote lakini bomu kubwa ni vijana. Sasa kama hatujawaangalia vijana tutaangalia kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kukuza ujuzi kwa vijana, kama hawajakuziwa ujuzi wao ina maana kwamba bidhaa zetu na vijana tatizo hatutoweza kulipatia ufumbuzi. Hii naomba tuweke kwenye Hansard, nakuja kuzuia shilingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza Mheshimiwa Mwijage kwamba kuna wazee ambao wamestaafu pensheni zao ni ndogo, malalamiko yao ni kwamba ile sheria iliyotungwa haifuatwi. Na maombi yao wanasema Serikali iunde Task Force kwa ajili ya kufuatilia tatizo la pensheni zao. Na wanaomba hii sheria basi, kwa zile changamoto zao, ikifuatwa hii sheria watakuwa wako sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika Jimbo langu la Jong’ombe. Niliahidiwa kupata skuli pale katika Shehia ya Kwalilatu kupitia TASAF. Lakini mpaka sasa hivi tunakwenda kumaliza bajeti hatujaona. Wananchi wamepita wamehojiwa, taratibu zimefanyika. Nilizungumza na Mheshimiwa Jenista wakati ule alisema atakuja yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali katika kipindi hiki ambacho kimebaki kwa kuwa jambo lilikuwepo katika mchakato, tunaomba tumalizie hili jambo ili kuweza kuwa-accommodate na kufanya lile jambo. Na mimi jamani mwenzenu nahitaji kura za kutoka kwa wananchi ili niweze kuja hapa. Kwa hiyo, jambo moja katika jimbo langu ni jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuzungumzia agenda yangu muhimu ile ya kwanza ya vijana. Endapo Serikali haitofanya, haito-ringfence watuambie mbinu gani watatumia, wata-ringfence lakini fedha at least zipatikane bilioni 36, vinginevyo Waheshimiwa Wabunge hakuna mtu ambaye hana tatizo la ajira katika jimbo lake. Tunafuatwa na wananchi. Nitaomba mje mniunge mkono wakati huo kwa sababu ya kuwasemea hawa vijana. Kama siyo hivyo ina maana kwamba tutawatelekeza vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa vijana wakiamua kufuata njia nyingine tutawafanya nini? Na ukimuona kijana kapata kitu sehemu nyingine mtakuja kusema vijana wanaharibika, lakini itakuwa kuharibika kwenu, kwa wenzenu watakuwa wametengemaa maana watakuwa wanawatumia wao. Sasa ili tuwatumie vijana wetu tuwajali katika ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Lakini pamoja na yote nitakuja kuzuia shilingi katika suala hili la SDL. Naunga mkono hoja; nashukuru sana.