Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya Ofisi ya Wairi Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai na uzima ambao umetuwezesha kusimama hapa na kufanya jambo hili muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri; vilevile niwapongeze Wenyeviti wa Kamati za Bunge zote ambazo zinasimamia ofisi hii kwa kuwasilisha hotuba nzuri za taarifa za Kamati zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kama ambavyo Wabunge wenzangu wamefanya, nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa fedha nyingi sana ambazo amezileta katika Jimbo la Bukene kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea fedha nyingi kwenye miradi ya maji, sasa hivi tunayatoa maji Nzega Mjini kuyafikisha Bukene, zaidi ya bilioni 24 na bilioni sita zimeshatoka; kuna fedha nyingi sana za miradi ya umeme, miradi ya barabara tunapasua barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee pia niipongeze Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mradi mkubwa sana wa mazingira ambao tumeupata pale kwenye Kata ya Sigili, Wilaya ya Nzega ambako jumla ya bilioni 2.5 zitatumika katika kujenga visima, maghala na mashine ambazo zitaongeza thamani ya mazao yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia; jambo la kwanza ambalo ninapenda kuongelea; niombe Ofisi ya Waziri Mkuu ifanye coordination kati ya Wizara ya Nishati na Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale jimboni kwangu kuna mradi mkubwa wa bomba la mafuta yanayotoka Uganda kwenda Chongoleani, Tanga. Na ndani ya mradi huo pale jimboni kwangu kuna mradi mkubwa sana wa kujenga coating yard. Yadi ambapo mabomba yote yatakayolazwa kutoka Uganda mpaka Tanga ndipo yatakapopakwa rangi maalum ili yatakapofukiwa chini yasioze. Ni mradi mkubwa mno wa zaidi ya bilioni 600; ni mradi mkubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu iwakutanishe Wizara ya Nishati na Ujenzi kwa sababu ilivyo sasa kila Wizara naona inafanya jambo lake kiutofauti. Wizara ya Nishati inaendelea kusimamia ujenzi wa yadi hii kubwa, ujenzi unaendelea vizuri. Lakini hata yadi hii ikikamilika hayo mabomba hayawezi kufika pale ili kupakwa hiyo rangi maalum kwa sababu hakuna barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayopita kwenye mradi huu ni barabara ya vumbi, ya changarawe, nyembamba, haina madaraja. Na mzigo unaopaswa kupitishwa kwenye barabara hiyo wa mabomba ni mzigo mzito, mkubwa sana. Mzigo wa mabomba zaidi ya tani 270,000, mabomba 86,000. Na kuna special trucks ambazo zimeshakodiwa, magari maalum zaidi ya 300 yatakuwa yanapishana kila siku. Kwa hiyo, barabara ilivyo sasa hivi huu mzigo hauwezi kupita na kufika pale coating yard.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijaona kama Wizara ya Ujenzi inaona umuhimu huo wa kuishughulikia barabara hii kwa sababu tangu miaka ya fedha miwili iliyopita ilishafanyiwa upembuzi yakinifu, ilishafanyiwa usanifu wa kina lakini miaka yote inapata fedha kidogo sana ambazo hazitoshi hata kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Meneja wa TANROADS Tabora ameshaandika barua kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kuomba kibali aruhusiwe kutangaza na Wizara impe fedha ili ujenzi uanze. Kwa hiyo, ninaona nishati wanafanya kazi kivyao na Wizara ya Ujenzi nao kwa upande wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu iwakutanishe kutokana na umuhimu wa mradi huu basi hicho kipande cha barabara kutoka Nzega ambako lami inaishia kupita Itobo mpaka Sojo ambako ndiko coating yard ilipo kiweze kujengwa kwa kiwango cha lami ili kupitisha mzigo mkubwa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu usalama wa chakula. Kabla ya msimu huu wa mavuno tulionao hapo nyuma tulipatwa na upungufu mkubwa wa chakula ambao ulisababisha bei ya mahindi kupanda sana, ilifika mpaka 22,000 mpaka 23,000 kwa debe, lakini niipongeze Serikali ilituletea mahindi kutoka NFRA ambayo yalikuja kupunguza makali ya bei kutoka 22,000 kwa debe mpaka 14,000 na ambayo ilisaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili kuondokana na tatizo hili, uwekezaji kwenye miradi ya umwagiliaji haukwepeki. Ushauri wangu; ni lazima tuongeze fedha ili tuweze kujenga miradi ya umwagiliaji, tuisimamie ili tuweze kujinasua na suala hili la kila mara upungufu wa chakula kwa sababu mvua zenyewe kutokana na mabadiliko ya tabianchi haziaminiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye jimbo langu kwenye Kata ya Kahama Nhalanga kuna mradi wa umwagiliaji ambao Serikali ilitumia zaidi ya bilioni moja kuujenga. Lakini mradi huu kimsingi haufanyi kazi. Miundombinu ya mashambani imeharibika, tuta limepasuka na bilioni moja zilishatumika lakini ile tija na tulichotegemea kupata hakipatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ungeweza kumwagilia hekta 1,000, karibu ekari 2,500, tungeweza kupata zaidi ya tani tano za mpunga, lakini haufanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza kwamba sasa hivi Serikali imepeleka ma-engineer wa umwagiliaji kila wilaya ili skimu za umwagiliaji ziweze kusimamiwa. Kwa hiyo, napongeza hatua hii ya kuwekeza, lakini lazima tuwekeze kwenye miradi ya umwagiliaji ili tuondokane na tatizo la upungufu wa chakula wa mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwamba tumepata mradi mkubwa wa umwagiliaji kwenye Kata ya Sigili, Kijiji cha Lyamalagwa, Bonde la Mto Manonga ambako zaidi ya hekta 3,000, kama ekari 4,500, ambazo mkandarasi wa kujenga bwawa ameshapatikana na zaidi ya bilioni 11 zitatumika ili kujenga skimu kubwa ambayo tutaweza kumwagilia zaidi ya ekari 7,500 ambayo itatupatia mazao ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ni maeneo mawili ambayo ninaomba kusisitiza na kushauri ili tuweze kuondokana na tatizo la upungufu wa chakula ambao unasababisha kupanda sana kwa bei ya chakula kama ambavyo tume-experience miezi miwili, mitatu iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia 100. Nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)