Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitumie nafasi hii kukupongeza wewe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hili; tuna imani kabisa ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumshukuru Rais wetu Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya. Hivi navyoongea kuna baadhi ya vijiji vyangu ambavyo vilikuwa vinaitwa vijiji vya giza; kwa mfano kama pale Changarawe Kata ya Masanze leo hii wamewasha umeme. Pamoja na hayo ndani ya wiki wanaenda kuwasha umeme katika Kijiji cha Ilakala katika Kata ya Muhenga, kule wedo katika Kata ya Kisanga na maeneo mengine ya Jimbo la Mikumi. Zaidi ya vijiji 20 vinaenda kuwasha umeme ndani ya mwezi huu, ni jambo kubwa sana kwetu na kwa niaba ya wananchi wa Mikumi tunaipongeza Serikali ya Rais wetu mama yetu Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya akiwa kama mratibu mkuu wa shughuli za Serikali ndani ya Bunge. Nimesikiliza hotuba yake ya bajeti; na niseme tu kwamba nafarijika kuona kwamba miradi ya kimkakati inaendelea, na kule Morogoro ukiondoa Bwawa la Mwalimu Nyerere tuna mradi mwingine mkubwa wa reli ya mwendokasi (Standard Gauge Railway - SGR) ambayo kipande cha kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kimeshakamilika kwa asilimia 97 na kipande cha Morogoro kuja Makutupora kimeshakamilika kwa asilimia 92.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu shughuli za Serikali na hasa kupambana na umaskini na pia kuhakikisha nchi yetu inafikia kwenye uchumi wa viwanda, ndilo jukumu lake kubwa. Katika hilo tunaona kuna activities mbalimbali ambazo zinaendelea lakini kubwa kuliko yote ni uratibu wa kuangalia ni jinsi gani sekta mbalimbali ndani ya Serikali zinawasiliana na zinafanya kazi pamoja ili rasilimali chache ambazo tunazo zitumike kwa tija na ufanisi kwa ajili ya maendeleo ya wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masikini hana anasa ya kutapanya rasilimali chache ambazo anazo; na ndiyo maana suala la uratibu (coordination) ni suala la muhimu kuliko yote kwa sababu tukifeli hapo tumefeli pakubwa. Kwa hiyo jukumu la uratibu Ofisi ya Waziri Mkuu ni jukumu kubwa ambalo wanapaswa kulibeba kwa uzito mkubwa. Kufanana na hayo ni TAMISEMI, ambao nao kwa sababu wanagusa sekta nyingi wanapaswa kufanya kazi kwa karibu sana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuratibu sekta mbalimbali, iwe uvuvi, kilimo, barabara, afya, elimu hata pia usalama katika ngazi ya vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikupatie taarifa ya kusikitisha; sekta ya uratibu ambayo ndiyo roho ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilivunjwa, sababu ya kuvunjwa kwa kitengo hiki ama idara kamili ambayo ilikuwa inasimamia uratibu wa viwanda, kielimu, uvuvi, ushirika, mazingira, kila kitu ambacho nakizungumza ambacho hakina idara kilikuwa kinaratibiwa kwenye idara ya uratibu wa sekta lakini hakipo. Sasa jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana ya kushirikiana kwa karibu na TAMISEMI katika kuhakikisha kwamba wanaenda kuboresha maisha kwa wananchi wetu, idara hii ya uratibu ni muhimu mno katika usimamizi wa shughuli mbalimbali za uzalishaji mali pamoja na pia kupambana na umaskini katika ngazi za chini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo rai yangu kwa Serikali iangalie sababu za kuvunja idara ya uratibu wa sekta ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Je, sababu hizo zina mashiko na athari yake ni nini kuondoa ile idara? kwa hiyo ni muhimu kuangalia upya uamuzi huo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la kupambana na umaskini, umaskini si pepo ambalo litaondoka kwa kulikemea ama kwa kunena kwa lugha. Umaskini ni hali ambayo unaweza ukapambana kwa maarifa. Unapopoteza maarifa maana yake umepoteza silaha muhimu sana katika kupambana na umaskini. Ndiyo maana tunasema kwamba suala la uratibu wa sekta mbalimbali kuona jinsi gani tunatumia rasilimali chache ni muhimu mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo tumewekeza kwenye reli ya mwendokasi ni nyingi sana. Vituo ambavyo vinaenda kusimama kwenye mwendokasi pale Kilosa ni vituo ambavyo uwekezaji wake ni mkubwa mno. Najaribu kufikiria, tumejipangaje kuona kwamba uwekezaji huu mkubwa unaenda kulipa? Kwa sababu nikiangalia basi la kutoka Kilombero kuja Kilosa la freedom linabeba abiria 20 mpaka 30 hawawezi kwenda kutumia kituo hiki ama stesheni hii ya mwendokasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia abiria wanaotoka Dar es Salaam kuja kilosa sioni nani ambaye anaenda kutumia kituo hiki cha SGR kwa maana ya treni ya mwendokasi. Lakini nikijaribu kuangalia ajali za mabasi na malori ambazo zinatokea, ukitoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ukitoka Morogoro mpaka Mikumi ajali ni nyingi mno. Mara nyingine tunasingizia tu mwendokasi wa madereva, lakini mwendokasi wa madereva si mwarobaini wa sababu za ajali za barabarani. Wembamba wa barabara, wingi wa magari, ubovu wa barabara ni maeneo muhimu ya kuyaangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa reli hii ya mwendokasi unaweza sana kutusaidia kupunguza ajali pia kupunguza safari za abiria wetu kutoka Dar es Saalam kwenda mikoa ya Kusini, kama tunaweza tukaitumia station hii pale Kilosa kwa umuhimu. Kwa mfano TRC inaweza ikawa na makubaliano na wenye mabasi ambayo yanaenda Ruvuma, Songwe, Iringa, Mbeya, Njombe na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini wakakata tiketi moja kutoka Dar es Salaam mpaka Mbeya lakini akifika pale Kilosa akaingia kwenye mabasi kwenda Mbeya, Songwe, Njombe. Kipande cha mwendo wa masaa sita tunaweza tukampunguzia huyu abiria saa moja na nusu. Kwa kufanya hivyo tunakuwa tume- save muda, kwa kufanya hivyo tunakuwa tumepunguza stress ya barabara na foleni barabarani, tukapunguza ajali tukapunguza mwendo lakini tukaongeza ufanisi, kwa maana ya uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linawezekana na tunaweza tukajifunza kwenye nchi za wenzetu jinsi mifumo ya usafiri, kwa maana ya treni za umma na mabasi binafsi yanaweza kuratibiwa katika kurahisisha safari za wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo malori yetu ni mengi sana ukiangalia na barabara zetu. Kuna umuhimu wa kujenga bandari kavu Kilosa. Ujenzi wa bandari hii kavu itakuwa na mantiki kwa sababu itaenda kuongeza ufanisi wa kituo ambacho kiko pale Kilosa kwa maana ya station ya pale Kilosa. Hili likifanyika nafkiri uwekezaji huu mkubwa unaweza kwenda kuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, linalofanana na hilo, kuna bilioni 571 zinawekezwa pale kwenye Kiwanda cha Sukari Ilovo. Tunajiuliza tunaenda kusafirisha vipi zile malighafi, kwa sababu reli ya kutoka Kilosa kwenda kwenye kiwanda kile cha sukari ilishakufa, na sioni jitihada zozote za kwenda kufufua reli ile? Ufufuaji wa reli ile unaenda kuimarisha uzalishaji katika kiwanda kile kinaenda kupunguza gharama ya uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa ile ambayo itakuwa affordable kwa mwananchi mmoja mmoja na; kwa maana hiyo inaenda kuleta tija ya uwekezaji mkubwa, ambao Serikali inafanya kwenye kiwanda kile cha Ilovo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji huu mkubwa wa reli sio tu kwamba unaenda kurahisisha maisha ya wananchi tu lakini pia hata utalii kwenye mbuga ya Mikumi. Mtalii anapofika Kilosa anapaswa kusafiri kilomita 100 kwenye barabara ya vumbi kufika Mikumi kuingia getini. Tumeshauri hapa si mara moja si mara mbili, kwamba inagharimu nini Serikali kufungua geti lingine upande wa Kiangali, kwa maana ya Kilosa, Mtalii atakaposhuka na treni ya mwendo kasi pale atembee kilomita 20 aingie getini afanye utalii wake? Hilo tukilifanya maana yake tutaupambanua uchumi wa mji wa Kilosa na vilevile tunaenda kuongeza tija ya reli hii ambayo uwekezaji wake ni mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha barabara barabara ya vumbi kutoka Kilosa mpaka Mikumi ndiyo ambayo tunategemea kuchukua watalii wetu ambao wanashuka kwenye mwendokasi ilia pate nafasi ya kuingia ndani ya mbuga yetu. Kwa kweli kwa hili ndiyo maana nasema kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu inapaswa kusimamia jukumu lake la kuratibu; TARURA kusimamia jukumu lake, kusimamia Wizara ya Maliasili na Utalii pia hata viwanda na biashara, kwa kufanya hivyo huu uwekezaji ambao tunaendelea kuwekeza kwenye mabwawa kwa ajili ya umeme, kwenye usafiri kwa (SGR) unaweza kwenda kuwa na tija kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sitendei haki kuchangia bila kuzungumzia changamoto za wananchi wetu hasa mipaka kati ya hifadhi, kwa maana ya TFS na vijiji vya kule Mdalasela kwa maana ya Kata ya Mikumi lakini kule Ulaya na baadhi ya maeneo ya Zombo, Nzitokwiva unasimamiwa na TFS ambao kila siku wanahamisha mipaka. Wakati umefika sasa tunategemea Serikali kuja kutuonesha mipaka ili wananchi watendewe haki ili waendeshe shughuli zao za kiuchumi kwa uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kilosa. Bado tumeona jitihada za Waziri Mkuu, alikuja kusimamia changamoto ambazo tunazo, lakini hilo halitoshi; tunaomba Serikali itekeleze yale yote ambayo Waziri Mkuu alielekeza akiwa kwenye ziara yake kule Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.