Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nianze kukupongeza wewe binafsi kwa busara na hekima kubwa uliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Nimefurahishwa sana na taarifa uliyoisoma hapa leo Bungeni asubuhi ya kutufafanulia kuhusu taarifa ya CAG. Naamini kabisa ni busara imekuongoza ukaona ni bora niende nikafafanue ili watu wanielewe. Tumekuelewa vizuri sana na tuko tayari kusubiri kujadili mwezi Novemba kama taratibu zetu zinavyosema.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya nchi yetu. Hakuna mtu ambaye hajui kuwa Mheshimwa Rais anafanya kazi kubwa. Mheshimiwa Rais anapambana ili kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee na kazi ya kutupambania sisi Watanzania. Mheshimiwa Rais amefanya mambo makubwa, amefanya mambo mengi ambayo mimi binafsi siwezi kuyataja mambo yote, ni mambo mengi sana ambayo ameyafanya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye halmashauri zetu fedha zinaingia kila siku na mambo yanakwenda vizuri. Asilimia mia moja ya bajeti tangu Mheshimiwa Rais ameingia madarakani ndiyo kwanza halmashauri zimepelekewa asilimia mia moja ya bajeti. Siku zote bajeti kwenda kwenye halmashauri ilikuwa haifiki asilimia mia moja. Mheshimiwa Rais anatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati lakini wakati huo halmashauri zinaenda fedha zote kwa ajili ya matumizi ya Watanzania. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa kuweka ruzuku ya mafuta na mbolea. Hili jambo watu hawalioni kwa sababu limepozwa na ruzuku ya Mheshimiwa Rais. Leo Mheshimiwa Rais kwa hali ilivyokuwa kipindi kile asingeweka ruzuku ya mafuta kila kitu kingekuwa juu, na pia asingeweka ruzuku ya mbolea sijui wakulima wetu wangelimaje; nampongeza sana Mheshimiwa, Rais tunaamini anawapenda Watanzania anawafikiria na kuwahudumia.
Mheshimiwa Spika, binafsi pia nimpongeze Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Amekuwa akizunguka nchi nzima kutatua matatizo ya Watanzania. Nampongeza na ninamtakia afya njema aendelee kufanya kazi yake. Niwapongeze pia waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, leo najikita tu kwenye suala la tumbaku. Mimi nimezaliwa Tabora na tumbaku ndiyo imenikuza na kunifikisha hapa. Tumbaku Tabora ilishuka kwa kiwango kikubwa. Mwaka 2010/2011 tumbaku ikakataliwa kununuliwa mpaka tukaita makinikia, tulikosa kabisa masoko. Kwa hiyo tumepambana sana akiwepo Waziri Mkuu. Kabla ya mwaka 2010/2011 tulikuwa tunauza kilo milioni 120, lakini hapo katikati tumbaku yetu ilishuka mpaka tukafikia kilo milioni 60. Lakini tangu ameingia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu madarakani miaka miwili na kidogo, tumbaku yetu imepanda sasa hivi tuna kilo milioni 130.
Mheshimiwa Spika, nikikuambia kilo 130 ina maana naongelea dola milioni tatu, nikiongelea dola milioni tatu; ina maana Tabora tunakwenda kupokea bilioni saba. Nikiuangalia Mkoa wetu wa Tabora na zile bilioni saba naangalia kabisa jinsi biashara zitakavyozunguka, mzunguko wa fedha utakavyokuwa mkubwa na maendeleo yatakavyopatikana.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini nampongeza pia Waziri wetu wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye Tumbaku. Baada ya kuweka wanunuzi, pia wazawa, wamesaidia sana kuhakikisha tumbaku yetu hainunuliwi. Zamani tulikuwa tunawekewa limit kwamba tulime kilo kadhaa tusiongeze kwa sababu hakuna wanunuzi sasa hivi ninapokwambia wanunuzi wapo wanatafuta wakulima, wako wanawa-convince wakulima kwa kila aina ili waweze kulima tumbaku nyingi waweze kupata na wao kununua.
Mheshimiwa Spika, Serengeti na Manyoni walikuwa wameacha kabisa kulima tumbaku kwa sababu wanunuzi walikataa kwenda kununua tumbaku kule, lakini leo hii kwa kazi nzuri inayofanya na Rais wetu wanunuzi wamerudi na wanakwenda kuanzisha Serengeti na Manyoni, kwa hiyo naamini mambo yatakuwa mazuri.
Mheshimiwa Spika,tumetoka kuuza kila dola 1.6 mpaka dola mbili sasa hivi tunauza kwa dola tatu, na kutakuwa na matabaka aina saba ya kuuza kwa dola tatu. Pia tutauza kwa dola mbili tumbaku inayofatia na kuna matabaka 17. Unaweza ukaona zao la tumbaku litaingiza fedha za dola kwenye nchi yetu kwa kiasi gani. Nizidi kuipongeza Serikali, lakini pia nizipongeze kampuni binafsi zilizojitokeza kununua, leo hii kwa kampuni hizo, hasa za wazawa, kuwa nyingi…
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Sasa hivi mnunuzi wa tumbaku akipeleka tumbaku yake sokoni analipa na elfu kumi ya kula.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Jamani taarifa mpaka had Mheshimiwa Spika aseme…
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Munde kuna taarifa kwa Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani.
T A A R I F A
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, kuwepo tu kwa Mheshimiwa Rais kama Rais wa Tanzania kampuni za tumbaku L10F ambayo ni daraja la kwanza ilikuwa ni dola mbili lakini leo tunavyoongea ni dola 3.56, L1F ambayo ilikuwa ni dola 1.04 tunavyoongea leo ni dola 2.99. Pia uzalishaji alivyosema mchangiaji sasa tumetoka kwenye kilo moja wastani wa bei kwa nchi nzima dola 1.4 sasa ni dola mbili ambazo ni fedha nyingi sana kwa Watanzania.
SPIKA: Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah unapokea taarifa hiyo?
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Cherehani na ninamshukuru sana. Niendelee kuwashukuru kampuni binafsi. Fununu zilizopo sasa hivi kampuni moja ya Mkwawa sasa hivi imenunua kilo milioni 45, lakini msimu ujao itanunua kilo milioni 80.
Mheshimiwa Spika, na kwenye ilani yetu ya uchaguzi tunatakiwa kufikia 2025 tununue tumbaku kilo milioni 200, na kwa sasaa hivi tuna kilo 130. Tunaamini ifikapo 2025 tutavuka lengo ambalo limeandikwa kwenye ilani yetu ya uchaguzi. Nawapongeza sana viongozi wetu kwa kuhakikisha zao letu linakwenda vizuri, na tuna imani kubwa sana.
Mheshimiwa Spika,kwa hiyo niombe sasa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo; wakulima wetu wa tumbaku hawakuwahi kupata mbolea ya ruzuku, walau walinunua mbolea imeandikwa ruzuku lakini waliuziwa kwa bei bila ruzuku. Niiombe Serikali, kupitia Wizara ya Kilimo waangalie, mauzo ya mara ya pili wawarudishie fedha zao wakulima wa tumbaku ili nao waweze kunufaika na keki ya nchi hii iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu na waweze kufurahia jambo lao na wao waweze kuwa wamepata mbolea ya ruzuku. Hii ni kwa sababu hawakupata mbolea ya ruzuku ya tumbaku wala ya mahindi kwa sababu tu ni wakulima wa tumbaku. Naiomba sana Serikali watakapokuja ku-wind up watuambie kwamba wako tayari kuwarudishia wakulima pesa zao.
Mheshimiwa Spika,ombi la pili, tunaomba Serikali iwaongezee uwezo wanunuzi wa tumbaku, hasa wanunuzi wazawa, ili wakulima wetu waweze kuuza tumbaku kwa ushindani mkubwa uliopo sasa hivi na uzidi kuendelea. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aingile kati mchakato wa pembejeo za kilimo zifike kwa wakati.
Pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea safari hii imechelewa kuwafikia wakulima. Naamini jambo hili la ruzuku ndiyo tumelianza kipindi hiki kwa msimu wa kwanza kwa hiyo tunaamini changamoto ndogo ndogo lazima zijitokeze. Ninaamini wamezijua na wamezielewa; na ninaamini kipindi hiki cha msimu huu watatuletea ruzuku kwa wakati na pembejeo zote kwa wakati ili wakulima wetu waendelee kulima vizuri.
Mheshimiwa Spika, fununu zilizopo ni kwamba kuna Kiwanda cha Sigara kinatakiwa kujengwa Morogoro, kitu kinauma sana Tumbaku asilimia 60 inalimwa Mkoa wa Tabora viwanda vyote vya kuchakata tumbaku viko Morogoro. Nimwombe Mheshimiwa Waziri na yeye pia ametoka Tabora asikubali kiwanda cha Sigara kijengwe Morogoro. Tunaomba kiwanda cha Sigara kijengwe Tabora ili na sisi watoto wetu wapate ajira, lile jasho la tambuku wanalotoa wazazi wao na wenyewe waweze kuajirika. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aje atupe ahadi hapa kwamba kiwanda hicho kinajengwa Tabora na si Morogoro.
Mheshimiwa Spika, inauma sana tumbaku zote tunazolima, viwanda vyote viko Morogoro, hata sitaki kusema kwa nini. Zamani walikuwa wanasema umeme sasa hivi tuna umeme wa kutosha, walikuwa wanasema maji sasa tuna maji ya kutosha, sijui Mheshimiwa Waziri atakuja atuambie kitu gani ili tuweze kumuelewa.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye miundo mbinu, tuna barabara zetu kubwa za kimkoa. Tunaiomba Serikali itufanyie barabara hizi ambazo zimeandikwa kwenye ilani zaidi ya mara tatu bila matengenezo. Tuna Barabara ya Kahama – Kaliwa – Mpanda, hii imekuwa kwenye ilani tena zaidi ya mara mbili, mara tatu haijatekelezwa. Tuna Ipole – Rungwa ambapo ikijengwa na wewe Mheshimiwa Spika utanufaika, kwa maana ya biashara za Mbeya na Tabora. Tunaomba Barabara ya Tabora – Ulyankulu, tunaomba Barabara ya Puge – Ndaya na Ziba, tunaomba sana Serikali itakapokuja kwenye bajeti yake ituambie nini hatima ya barabara hizi ambazo mmetuahidi mara kadhaa kwenye ilani ya uchaguzi lakini bado hazijatekelezeka.
Mheshimiwa Spika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa sekunde 30 malizia hoja yako, kengele imeshagonga.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, nilikuwa nataka kuongea kuhusu Kaliua, Mbunge aliongea hapa, kaka yangu Kwezi, kuhusu Kata mbili za Usinge na Kakoko. Mheshimiwa Rais alikuja kule akaahidi wananchi wale waongezewe maeneo kwenye vijiji vyao; lakini tunashangaa wananchi wale wanatakiwa wahamishwe wapelekwe sehemu nyingine ilhali kuna kaya 1,300.
Mheshimiwa Spika, unaelewa ukiambia kaya 1,300 kuna akina mama, kuna Watoto na kuna wajane wamejenga; leo unapo mhamisha unampeleka sehemu mpya ilhali Mheshimiwa Rais alisha ruhusu, na tunajua kauli ya Rais ni maelekezo, ni maagizo, haiwezi ikaanza kuchakachuliwa. Mheshimiwa Rais aliagiza waongezewe maeneo pale walipo. Niwaombe sana Serikali wafuate amri ya Mheshimiwa Rais na si vinginevyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)